The chat will start when you send the first message.
1Kisha maadui wa watu wa Yuda na Benyamini waliposikia kwamba watu waliorudi kutoka uhamishoni wanalijenga upya hekalu la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli,[#4:1 Hawa walikuwa watu ambao Waashuru na Wababuloni walikuwa wamewateka na kuwafanya waishi nchini Israeli baada ya kuwapeleka wakazi wake uhamishoni mwaka 722 K.K.]
2walimwendea Zerubabeli na viongozi wa koo, na kumwambia, “Tafadhali tushirikiane katika ujenzi wa hekalu. Sisi kama nyinyi tunamwabudu Mungu wenu, na tumekuwa tukimtolea tambiko tangu zamani za Esar-hadoni, mfalme wa Ashuru aliyetuleta hapa.”[#4:2 Esar-hadoni, mwanawe Senakeribu mfalme wa Ashuru, alitawala Ashuru tangu mwaka 681 mpaka 669 K.K.]
3Lakini Zerubabeli, Yeshua na viongozi wengine wa koo za Israeli wakawaambia, “Sisi hatuhitaji msaada wowote kutoka kwenu ili kuijenga nyumba ya Mungu wetu. Sisi wenyewe tutamjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kama mfalme Koreshi wa Persia alivyotuamuru.”
4Hapo, watu waliokuwa wanaishi mahali hapo wakaanza kuwavunja moyo na kuwatisha Wayahudi ili wasiendelee kama walivyokusudia.[#4:4-5 Upinzani huo uliendelea kwa muda mrefu nao ukasababisha kuacha kwa muda ujenzi huo tangu mwaka 536 mpaka 520 K.K. “Dario” alitawala tangu 522 mpaka 486 K.K.]
5Tena waliwahonga maofisa wa serikali ya Persia wawapinge Wayahudi. Waliendelea kufanya hivyo muda wote wa utawala wa Koreshi, mpaka wakati wa utawala wa Dario.
6Mwanzoni mwa utawala wa mfalme Ahasuero, maadui wa watu waliokaa Yuda na Yerusalemu waliandika mashtaka dhidi yao.[#4:6 Ndivyo anavyoitwa katika makala ya Kiebrania; pengine anaitwa “Kherkhesi”. Alitawala yapata mwaka 485. Taz pia Esta 1:1-2.]
7Tena wakati wa utawala wa Artashasta, mfalme wa Persia, Bishlamu, Mithredathi, Tabeeli na rafiki zao, walimwandikia barua mfalme Artashasta. Barua hiyo iliandikwa kwa herufi za Kiaramu na kutafsiriwa.[#4:7 Au, “Artakherkhesi”. Huyu alitawala baada ya mfalme Ahasuero mwaka 465-424 K.K.; #4:7 Ezra 4:8—6:18 imeandikwa kwa Kiaramu badala ya Kiebrania kama ilivyokuwa kwa vitabu karibu vyote vya A.K. Nini hasa kilichoandikwa katika barua hiyo hatujui kwa uhakika lakini kutokana na mazingira yake bila shaka lilikuwa jaribio la kuzuia ujenzi wa ukuta wa Yerusalemu.]
8Pia mtawala Rehumu na Shimshai, katibu wa mkoa, walimwandikia Artashasta barua ifuatayo dhidi ya Yerusalemu:
9“Kutoka kwa mtawala Rehumu na Shimshai, katibu wa mkoa pamoja na wenzetu, na mahakimu, maofisa wote ambao hapo awali walitoka Ereki, Babuloni na Susa katika nchi ya Elamu,
10pamoja na watu wa mataifa mengine ambao Asur-banipali, mtu mkuu na mwenye nguvu aliwahamisha na kuwaweka katika mji wa Samaria na mahali pengine katika mkoa wa magharibi ya Eufrate.”[#4:8-10 Huyu alitawala Ashuru tangu mwaka 669 mpaka 633 K.K.]
11Barua yenyewe ilikuwa hivi:
“Kwa mfalme Artashasta: Sisi watumishi wako katika mkoa wa magharibi ya Eufrate, tunakutumia salamu.
12Tungependa ufahamu, ewe mfalme, kwamba Wayahudi waliokuja hapa kutoka maeneo mengine ya ufalme wako wamekwenda Yerusalemu na wanaujenga upya mji huo mwasi na mwovu. Wanamalizia kujenga kuta zake na kutengeneza msingi.
13Tungependa ufahamu, ewe mfalme, kuwa mji huu ukijengwa upya na kuta zake zikimalizika, watu hawatalipa kodi, ushuru wala ada, na hazina yako itapungua.
14Sasa, kwa kuwa ni wajibu wetu, ee mfalme, hatungependa kuona ukivunjiwa heshima, ndiyo maana tumeona ni vizuri tukuarifu[#4:14 Maneno haya yanajaribu kutafsiri kile ambacho katika Kiebrania neno kwa neno ni “tunakula chumvi katika ikulu”. Kula chumvi hapa inatumika kimfano kwa maana ya kuwa na maafikiano ya kirafiki, au mapatano kati yao na utawala wa mfalme. Kushiriki katika kula chumvi ni kula mma au kufanya maafikiano rasmi yasiyoweza kubatilishwa. Taz pia Lawi 2:13.]
15ili ufanye uchunguzi katika kumbukumbu za babu zako. Humo utagundua kwamba tangu zamani, mji huu ulikuwa mwasi na umewasumbua sana wafalme na watawala wa mikoa, na kuwa tangu zamani watu wake ni wachochezi sana; ndio sababu mji huo uliangamizwa.
16Kwa hiyo tunakujulisha kwamba ikiwa mji huu utajengwa upya na kuta zake zikimalizika, hutaweza kuutawala mkoa wa magharibi ya Eufrate.”
17Kisha mfalme akapeleka jibu lifuatalo:
“Kwa mtawala Rehumu, kwa Shishai, katibu wa mkoa, pamoja na wenzenu wote wanaoishi Samaria na mahali penginepo katika mkoa wa magharibi ya Eufrate.
18“Barua mliyonitumia imetafsiriwa na kusomwa mbele yangu.
19Nimetoa amri uchunguzi ufanywe na imegunduliwa kuwa ni kweli kwamba tangu zamani mji huu wa Yerusalemu umekuwa ukiwapinga wafalme na kwamba watu wake wamekuwa waasi na wachochezi wakubwa.
20Wafalme wenye nguvu wamepata kuutawala mji huo pamoja na mkoa wa magharibi ya Eufrate wakitoza kodi, ushuru na ada.
21Kwa hiyo, toeni amri watu hao waache kuujenga upya mji huo hadi hapo nitakapotoa maagizo mengine.[#4:21 Katika mwaka 444, mfalme huyo huyo alimruhusu Nehemia kuendelea tena na ujenzi wa Yerusalemu.]
22Tena, angalieni sana msichelewe kufanya hivyo, nisije nikapata hasara.”
23Mara tu waliposomewa barua hii kutoka kwa Artashasta, Rehumu, katibu Shimshai na wenzao waliharakisha kwenda Yerusalemu na kuwalazimisha kwa nguvu Wayahudi waache kuujenga mji.
24Kazi ya kuijenga upya nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu ilisimama, na hali hiyo iliendelea mpaka mwaka wa pili wa utawala wa Dario, mfalme wa Persia.