The chat will start when you send the first message.
1Adamu akalala na Hawa mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Hawa akasema, “Nimepata mtoto wa kiume kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu!”[#4:1 Jina “Kaini” linatamkika kama kitenzi cha Kiebrania chenye maana ya “nimepata”.]
2Halafu akamzaa Abeli nduguye. Abeli alikuwa mfugaji kondoo na Kaini alikuwa mkulima.[#4:2 Hapa tunapewa kazi mbili zinazotofautiana: mkulima na mfugaji. Inafahamika kwamba kulikuwa na mzozo kati ya wakulima na wafugaji (rejea Amu 6:3-6). Hata hivyo uhasama wa Kaini dhidi ya nduguye Abeli haukuwa kwa vile Abeli alikuwa mfugaji, bali kutokana na kukubaliwa na kukataliwa kwa matambiko yao kwa Mwenyezi-Mungu (rejea aya ya 5).]
3Baada ya muda fulani, Kaini alimtolea Mwenyezi-Mungu sadaka kutokana na mazao ya shambani,
4naye Abeli akamtolea Mungu sadaka ya wazawa wa kwanza wa kondoo wake na nyama nono. Mwenyezi-Mungu akapendezwa na Abeli na tambiko yake,
5lakini hakupendezwa na Kaini wala na tambiko yake. Basi, Kaini akakasirika sana na uso wake ukakunjamana.[#4:4-5 Kisa hiki hakioneshi kwa nini tambiko moja ilikubaliwa na nyingine kukataliwa. Katika Ebr 11:4 mwandishi wa barua hiyo anasema kwamba ni kwa sababu ya imani kwamba tambiko ya Abeli ilikubaliwa.]
6Mwenyezi-Mungu akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika, na kwa nini uso wako umekunjamana?
7Je, ukitenda vyema hutakubaliwa? Na usipotenda vyema, basi, dhambi inakuvizia mlangoni; inakutamani, lakini unapaswa kuishinda.”[#4:7 Kwa mara nyingine simulizi hili la Biblia linaonesha uwezekano wa binadamu kuchagua kwa hiari yake na kwa kuwajibika jambo jema au baya (taz Mwa 2:17 maelezo na pia Kumb 30:15-20). Msomaji anaweza kuona uhusiano uliopo kati ya onyo la Mwenyezi-Mungu kwa Kaini hapa na amri aliyowapa binadamu wa kwanza (Mwa 2:16-17). Kadiri ya simulizi lililotangulia, agizo la Mungu lilivunjwa kwa kutotii; kadiri ya simulizi hili, inahusu kosa la jinai. Kama vile katika kosa la hapo awali na katika kisa hiki, baada ya dhambi Mwenyezi-Mungu anawakabili wote kwa swali (Mwa 3:9 na 4:9), kisha adhabu (3:14-19; 4:11-12) na kufuata kitendo cha ishara cha huruma kutoka kwa Mwenyezi-Mungu ambacho kwa namna moja au nyingine kinapunguza uzito wa hizo adhabu (Mwa 3:21 na 4:15). Hayo ni mambo yanayoonekana kutokana na muundo wa maandishi.]
8Baadaye, Kaini akamwambia Abeli nduguye, “Twende nje shambani.” Basi, walipokuwa shambani, Kaini akamvamia Abeli nduguye, akamuua.[#4:8 Tafsiri kulingana na hati nyingine za kale. Maneno haya hayamo katika makala ya Kiebrania.]
9Mwenyezi-Mungu akamwuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?” Kaini akamjibu, “Mimi sijui! Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”[#4:9 Katika swali hili kuna uhusiano sambamba na swali katika Mwa 3:9. Katika visa hivyo viwili wanaoulizwa wanajaribu kuficha kuwajibika kwao kwa namna moja au nyingine.]
10Mwenyezi-Mungu akasema, “Umefanya nini? Damu ya ndugu yako yanililia kutoka udongoni.[#4:10 Linganisha swali hili na lile la Mwa 3:13.; #4:10 Taz Zab 9:12 maelezo. Uuaji wa mtu bila sababu za kutosha ni jinai na kitendo hicho kinapatilizwa. Rejea Eze 24:7-8.]
11Sasa wewe umelaaniwa! Hutailima tena ardhi yenye rutuba ambayo kama kinywa imeipokea damu ya nduguyo uliyemuua.
12Ukiilima ardhi haitakupatia tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani.”
13Kaini akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Adhabu yangu ni kubwa mno; siwezi kuistahimili.[#4:13 Kaini haoneshi majuto; anaona tu kwamba kosa lake la jinai linamtenga na Mungu na binadamu na kunung'unika kwamba mazingira yake yanamsababisha kutokuwa na usalama na ulinzi.]
14Leo umenifukuza kutoka ardhi yenye rutuba na mbali nawe. Basi, nitakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani, na yeyote atakayeniona ataniua.”
15Lakini Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Sivyo! Atakayekuua wewe Kaini atalipizwa mara saba.” Basi, Mwenyezi-Mungu akamtia Kaini alama ya tahadhari, ili yeyote atakayemwona asimuue.[#4:15 Taz maelezo ya 4:23-24.; #4:15 Katika aya hii haisemwi hiyo ishara au alama ni ya namna gani. Lakini ni dhahiri kwamba alama hiyo ilimweka huyo mhalifu chini ya ulinzi wa Mungu na kuyakinga maisha yake. Rejea Eze 9:4-5. Taz pia Mwa 3:21 maelezo.]
16Kisha Kaini akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawa anaishi katika nchi ya Nodi, upande wa mashariki wa Edeni.[#4:16 Mahali au eneo lisilojulikana. Baadhi ya wafafanuzi wa Maandiko Matakatifu wanadhani jina hili linatumika kama mfano wa kugusia juu ya maisha ya kutangatanga (neno “Nad” Kiebrania lina maana ya “mwenye kutangatanga”).]
17Kaini akalala na mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Henoki. Kaini akajenga mji akauita kwa jina la Henoki mwanawe.
18Henoki akamzaa Iradi, naye Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli, naye Methushaeli akamzaa Lameki.[#4:18 Sehemu ya kwanza ya nasaba hii ina vizazi saba, kuanzia Adamu mpaka Lameki. Idadi hiyo saba bila shaka inatumiwa kama mfano kwa vile huko Palestina na kwa jumla katika Mashariki ya Kati ya Kale idadi saba huwakilisha ukamilifu na utimilifu. Taz maelezo ya Mwa 4:23-24 na Zab 79:12.]
19Lameki alioa wanawake wawili, mmoja aliitwa Ada na mwingine Sila.
20Ada alimzaa Yabali ambaye alikuwa baba yao wafugaji waishio mahemani.
21Ndugu yake alikuwa Yubali; huyo alikuwa baba yao wanamuziki wote wapigao zeze na filimbi.
22Sila naye alimzaa Tubal-kaini, ambaye alikuwa mhunzi wa vyombo vyote vya shaba na chuma. Dada yake Tubal-kaini alikuwa Naama.
23Lameki akawaambia wake zake,
“Ada na Sila sikieni sauti yangu!
Sikilizeni nisemayo enyi wake za Lameki.
Mimi niliua mtu kwa kunijeruhi,
naam, nilimuua kijana kwa kuniumiza.
24Ikiwa Kaini atalipizwa mara saba,
kweli Lameki atalipizwa mara sabini na saba.”
25Adamu akalala tena na Hawa mkewe, naye akazaa mtoto wa kiume, akamwita Sethi akisema, “Mungu amenijalia mtoto mahali pa Abeli aliyeuawa na Kaini.”
26Sethi naye alipata mtoto wa kiume, akamwita Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kumwomba Mwenyezi-Mungu kwa jina lake.[#4:26 Jina hili Kiebrania linatamkika kama neno lenye maana ya “nimejaliwa”.; #4:26 Jina hili katika Kiebrania lina maana ya “mtu”.; #4:26 Taz maelezo ya 2:4. Hapa tunadokezewa kwamba jina hilo la Mwenyezi-Mungu lilikuwa la kale, kabla ya Mose. Taz pia maelezo ya Kut 3:13; 3:14; na 6:3.]