The chat will start when you send the first message.
1Yakobo akawaita wanawe, akasema, “Kusanyikeni pamoja niwaambieni mambo yatakayowapata siku zijazo.
2“Kusanyikeni msikie, enyi wana wa Yakobo,
nisikilizeni mimi Israeli, baba yenu.
3“Wewe Reubeni ni mzaliwa wangu wa kwanza,[#49:3-4 Huyu alikuwa mzaliwa wa kwanza wa Yakobo. Lakini alipokonywa haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa kosa lake lililoathiri maadili ya jamii, yaani kwa kulala na Bilha ambaye alikuwa suria wa baba yake (Mwa 35:22; rejea 29:29).]
nguvu yangu na tunda la ujana wangu.
Wewe wawapita ndugu zako kwa ukuu na nguvu.
4Wewe ni kama maji ya mafuriko.
Lakini hutakuwa wa kwanza tena,
maana ulipanda kitandani mwangu mimi baba yako,
wewe ulikitia najisi;
naam wewe ulikipanda!
5“Simeoni na Lawi ni ndugu:
silaha zao wanatumia kufanya ukatili,
6lakini mimi sitashiriki njama zao;
ee roho yangu, usishiriki mikutano yao,
maana, katika hasira yao, walimuua mtu,
kwa utundu wao walikata mshipa wa ng'ombe.
7Nalaani hasira yao maana ni kali mno,
na ghadhabu yao isiyo na huruma.
Nitawatawanya katika nchi ya Yakobo,
nitawasambaza katika nchi ya Israeli.
8“Wewe Yuda, ndugu zako watakusifu.
Adui zako utawakaba shingo;
na ndugu zako watainama mbele yako.
9Wewe Yuda, mwanangu, ni kama mwanasimba
ambaye amepata mawindo yake akapanda juu.
Kama simba hujinyosha na kulala chini;
simba mwenye nguvu, nani athubutuye kumwamsha?
10Fimbo ya kifalme haitatoka kwa Yuda,
wala bakora ya utawala miguuni pake,
mpaka atakapofika yule ambaye ni yake;
ambaye mataifa yatamtii.
11Atafunga punda wake katika mzabibu
na mwanapunda wake kwenye mzabibu bora.
Hufua nguo zake katika divai,
na mavazi yake katika divai nyekundu.
12Macho yake ni mekundu kwa divai,
meno yake ni meupe kwa maziwa.
13“Zebuluni ataishi sehemu za pwani,[#49:13 Kabila la Zabuloni litafanya biashara ya baharini (Kumb 33:18-19).]
pwani yake itakuwa mahali pa kuegesha meli.
Nchi yake itapakana na Sidoni.
14“Isakari ni kama punda mwenye nguvu,
ajilazaye kati ya mizigo yake.
15Aliona kuwa mahali pa kupumzikia ni pema,
na kwamba nchi ni ya kupendeza,
akauinamisha mgongo wake kubeba mzigo,
akawa mtumwa kufanya kazi za shuruti.
16“Dani atakuwa mwamuzi wa watu wake,
kama mojawapo ya makabila ya Israeli.
17Atakuwa kama nyoka njiani,
nyoka mwenye sumu kando ya njia,
aumaye visigino vya farasi,
naye mpandafarasi huanguka chali.
18“Ee Mwenyezi-Mungu, nangojea uniokoe!
19“Gadi atashambuliwa na wanyang'anyi,
lakini yeye atawafuata nyuma na kuwashambulia.
20“Ardhi ya Asheri itatoa mavuno kwa wingi,
naye atatoa chakula kimfaacho mfalme.
21“Naftali ni kama paa aliye huru,
azaaye watoto walio wazuri.
22“Yosefu ni kama mti uzaao,
mti uzaao kando ya chemchemi,
matawi yake hutanda ukutani.
23Wapiga mishale walimshambulia vikali,
wakamtupia mishale na kumsumbua sana.
24Lakini upinde wake bado imara,
na mikono yake imepewa nguvu,
kwa uwezo wa Mwenye Nguvu wa Yakobo,
kwa jina la Mchungaji, Mwamba wa Israeli;
25kwa Mungu wa baba yako atakayekusaidia,
kwa Mungu mwenye nguvu atakayekubariki;
upate baraka za mvua toka juu mbinguni,
baraka za maji ya vilindi vilivyo chini,
baraka za uzazi wa akina mama na mifugo.
26Baraka za baba yako zishinde baraka za milima ya milele,
ziwe bora kuliko vilima vya kale.
Baraka hizo na ziwe juu ya kichwa cha Yosefu,
juu ya paji lake yeye aliyekuwa ametengwa na ndugu zake.
27“Benyamini ni mbwamwitu mkali;[#49:27 Kabila la Benyamini lilikuwa kabila dogo kuliko makabila mengine. Lakini umaarufu wake ulijitokeza kutokana na wapiganaji wake hodari (rejea Amu 3:15; 5:14; 20:15-16). Mfalme Sauli alitoka katika kabila hili (rejea 1Sam 9:1-2,21; 10:1-2). Taz pia Rom 11:1; Fil 3:5.]
asubuhi hula mawindo yake,
na jioni hugawa nyara.”
28Hayo ndiyo makabila kumi na mawili ya Israeli, na hayo ndiyo maneno aliyowaambia baba yao alipowabariki, kila mmoja wao kama alivyostahili.[#49:28—50:14 Sehemu hii ifuatayo inamalizia na kukamilisha historia ya Yosefu ambayo ilianza katika Mwa 37.]
29Kisha Israeli akawaagiza wanawe hivi, “Mimi karibu nife na kujiunga na watu wangu. Nizikeni pamoja na wazee wangu katika pango lililoko shambani mwa Efroni Mhiti,
30kule Makpela, mashariki ya Mamre, nchini Kanaani. Abrahamu alinunua pango na shamba hilo kwa Efroni, Mhiti, liwe lake la kuzikia.
31Huko ndiko walikozikwa Abrahamu na mkewe Sara; huko ndiko walikozikwa Isaka na mkewe Rebeka; na huko ndiko nilikomzika Lea.
32Shamba hilo na pango lake lilinunuliwa kwa Wahiti.”
33Yakobo alipomaliza kuwausia wanawe, aliirudisha miguu yake kitandani, akatoa roho akajiunga na wazee wake.