The chat will start when you send the first message.
1Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, nawaandikia nyinyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salamu![#1:1 Taz Utangulizi.; #1:1 Kwa kawaida maneno makabila kumi na mawili yaliyotawanyika yalitumiwa kuwataja Wayahudi waliotawanyika mahali pengi wakati wa uhamisho wa Babuloni. Lakini hapa, maneno hayo yanatumiwa kuwataja Wakristo wote.]
2Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali,[#1:2 Majaribu hapa ni mwelekeo na fikra za ndani ya mtu (au vishawishi) ambavyo huweza kumfanya mtu aanguke katika dhambi. Taz 1:12-14 maelezo. Lakini neno hilo pengine linaweza pia kuwa na maana ya shida, matatizo au magumu fulani kutoka nje.]
3kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu.[#1:3 Imani hapa inaeleweka kama uthabiti na uaminifu katika mwenendo unaotakiwa na Injili. Pengine neno hili hutumiwa kwa maana mbalimbali kulingana na matumizi katika sehemu tofauti tofauti.]
4Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote.
5Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.
6Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo.[#1:6 Yaani kuomba pamoja na matumaini kamili kuhusu wema na uaminifu wake Mungu; taz Yak 1:3 na 2:14.]
7-8Kwa hiyo mtu aliye na mashaka, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote, asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana.[#1:7-8 Yahusu wale ambao wanayumbayumba na kufuata mara hiki mara kile. Wazo hili ni muhimu katika Yakobo (taz k.m. 2:4, 9, 10, 26; 4:8; rejea pia 1Fal 18:21; Hos 10:2).]
9Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza,[#1:9-10 Mwandishi anafundisha kwamba hali mbalimbali za maisha ya jamii hazipaswi kamwe kuweka tabaka ya wakubwa na wanyonge katika jumuiya ya Wakristo kwa sababu hali hizo hazina thamani mbele ya Mungu. Ndivyo pia alivyofundisha Yesu; nao manabii wa A.K. walipinga sana jambo la kuwapendelea matajiri na kuwapuuza maskini (taz Meth 22:22-23; Amo 8:4-7; Mat 5:3,5; Luka 6:20,24).]
10naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini.
11Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake.[#1:11 Au, “akiwa kwenye shughuli zake”.]
12Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili, atapewa tuzo la uhai ambalo Mungu aliwaahidi wale wanaompenda.[#1:12 Msemo wa kimaandishi ambao katika Biblia unamaanisha, pamoja na mengine, aghalabu hali ya fanaka au baraka ya Mungu au hali yenye kukubalika vema. Pengine ni kinyume cha balaa au laana (taz Mat 5:3 maelezo).; #1:12 Au, “taji”. Rejea 1Kor 9:25 maelezo; 2Tim 4:8; 1Pet 5:4 na Ufu 2:10.; #1:12-14 Neno lilelile la Kigiriki ambalo limetafsiriwa kwa “majaribu” laweza kutafsiriwa pia kwa neno la Kiswahili “vishawishi” kulingana na mazingira ya maandishi.]
13Kama mtu akijaribiwa, asiseme: “Ninajaribiwa na Mungu.” Maana Mungu hawezi kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote.[#1:13 Ingawa sehemu nyingi za Biblia zinatamka kwamba Mungu ndiye anayesababisha kila kitu (Kut 4:21 Rom 9:18), Yakobo anafafanua wazi kwamba Mungu kamwe hamwongozi mtu yeyote kutenda maovu.]
14Lakini mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya.
15Tamaa ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo.[#1:15 Paulo ana picha inayofanana na hii katika Rom 7:7-11.]
16Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike!
17Kila kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu.
18Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe katika nafasi ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake.[#1:18 Neno kwa neno: “matunda ya kwanza”. Matunda ya kwanza yaliwekwa wakfu kwa Bwana na kwa msingi huohuo mwandishi anataka kusema kwamba Wakristo ni mali yake Mungu na ni wa kwanza miongoni mwa viumbe wake. Taz Yer 2:3; Ufu 14:4.]
19Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini si mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika.
20Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki.
21Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea lile neno lililopandwa mioyoni mwenu, ambalo laweza kuziokoa nafsi zenu.[#1:21 Yahusu ule ujumbe kuhusu sheria kamilifu ya Mungu (aya 25) au ile habari njema ya Yesu Kristo ambayo ndiyo njia ya Mungu ya kuwaokoa binadamu wote wanaomwamini Yesu (Rom 1:16).]
22Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo.[#1:22 Wazo hili ni muhimu na linarudiwa tena na tena: Kusikiliza kwa masikio tu haitoshi. Taz hasa 2:14-26; na rejea Ezra 7:10; Mat 7:21,24-27; Luka 11:28.]
23Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo.
24Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo.
25Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya.[#1:25 Sheria hiyo ni Injili kwa vile huweka katika ukamilifu sheria ya A.K. Wazo la Paulo katika Rom 8:2 ni tofauti.]
26Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe.[#1:26 Hili ni wazo linalotajwa mara kwa mara katika maandishi ya hekima. Rejea Zab 34:13; Meth 18:21.]
27Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu.[#1:27 Maneno: “Kuwasaidia yatima na wajane … na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu” yanamtayarisha na kumwongoza msomaji kwa sura ya 2 na ya 4. Rejea Isa 1:16-17.]