The chat will start when you send the first message.
1Ee Mwenyezi-Mungu, wewe ni mwadilifu,
ingawa nakulalamikia.
Lakini ningependa kutoa hoja zangu mbele yako:
Kwa nini waovu hufanikiwa katika mambo yao?
Mbona wote wenye hila hustawi?
2Unawaotesha nao wanaota;
wanakua na kuzaa matunda.
Wanakutaja kwa maneno yao,
lakini mioyo yao iko mbali nawe.
3Lakini wewe ee Mwenyezi-Mungu wanijua;[#12:3 Taz Yer 11:20 ambapo mwanazaburi anatamka kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye mwenye kupima mioyo na akili za watu na hivyo anajua kila kitu.]
wayathibiti maelekeo yangu kwako.
Uwaokote hao kama kondoo wa kuchinjwa,
watenge kwa ajili ya wakati wa kuuawa.
4Mpaka lini nchi itaomboleza kwa ukame,
na nyasi za mashamba yote kunyauka?
Wanyama na ndege wanakufa kwa uovu wa wakazi wake;
wanasema: “Mungu hataona mwisho wetu.”
5Mwenyezi-Mungu asema,
“Ikiwa umeshindana na waendao kwa miguu ukachoka,
utawezaje kushindana na farasi?
Kama unaanguka katika nchi isiyo na vizuizi,
utafanyaje katika msitu wa Yordani?
6Hata ndugu zako, jamaa yako mwenyewe,
nao pia wamekutendea mambo ya hila;
wanakukemea waziwazi.
Usiwaamini hata kidogo,
japo wanakuambia maneno mazuri.”
7Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Nimeiacha nyumba yangu;
nimeitupa mali yangu mimi mwenyewe.
Israeli, mpenzi wangu wa moyo,
nimemtia mikononi mwa maadui zake.
8Wateule wangu wamenigeuka,
wamekuwa kama simba porini,
wameningurumia mimi;
ndiyo maana nawachukia.
9Wateule wangu wamekuwa ndege mzuri
wanaoshambuliwa na kozi pande zote.
Nenda ukawakusanye wanyama wote wakali
waje kushiriki katika karamu.
10Wachungaji wengi wameharibu shamba langu la mizabibu,[#12:10 Rejea Zab 80:8-13. Uvamizi unaotajwa hapa labda ulitukia mwaka 602 wakati makundi ya wavamizi yalipelekwa dhidi ya Yuda kutoka kwa Waaramu, Wamoabu na Waamoni kufuatia uasi wa mfalme Yehoyakimu dhidi ya Nebukadneza, mfalme wa Babuloni (2Fal 24:1-2).]
wamelikanyagakanyaga chini lililo mali yangu;
shamba langu zuri wamelifanya jangwa.
11Wamelifanya kuwa tupu;
katika ukiwa wake lanililia.
Nchi yote imekuwa jangwa,
wala hakuna mtu anayejali.
12Juu ya milima yote jangwani,
watu wamefika kuangamiza.
Upanga wangu unapita kuiangamiza nchi,
toka upande mmoja hadi mwingine,
wala hakuna mtu atakayeishi kwa amani.
13Walipanda ngano, lakini walivuna magugu;
walifanya bidii, lakini hawakupata kitu.
Kwa sababu ya hasira yangu kali,
mavuno watakayoyapata yatakuwa aibu tupu.”
14Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya jirani wabaya wa watu wangu: “Wamekigusa kile kilicho changu, kile nilichowapa watu wangu Israeli! Basi nitawang'oa kutoka katika nchi yao. Hata watu wa Yuda nitawang'oa katika nchi yao.
15Lakini baada ya kuwang'oa, nitawahurumia tena; nitalirudisha kila taifa katika sehemu yake na katika nchi yake.
16Na kama watajifunza njia za watu wangu kwa moyo wote, kama wataapa kwa jina langu kwa kusema, ‘Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu,’ kama vile walivyowafundisha watu wangu kuapa kwa jina la mungu Baali, basi watajengeka miongoni mwa watu wangu.[#12:16 Maneno ambayo ni muhimu kwa watu wa mataifa mengine ambao watakuwa pia watu wa Mungu pamoja na Waisraeli ikiwa wataiacha miungu yao ya uwongo. Rejea Isa 56:3-8; Yer 3:17; 18:7-10.]
17Lakini taifa lolote ambalo halitanitii, nitaling'oa kabisa na kuliangamiza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”