The chat will start when you send the first message.
1Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Nenda ukajinunulie kikoi cha kitani, ukajifunge kiunoni; lakini usikitie majini.”[#13:1 Yaani kilichotengenezwa kwa nyuzi za kitani. Yaonekana kwamba madhumuni ya amri ya kukiweka mbali na maji ni kukiepusha na chochote kinachoweza kukifanya kioze au kuharibika.]
2Basi, nikaenda, nikanunua kikoi kama alivyoniagiza Mwenyezi-Mungu, nikajifunga kiunoni.
3Kisha, neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mara ya pili:
4“Kichukue kikoi ulichonunua na ambacho umejifunga kiunoni, uende kwenye mto Eufrate na kukificha katika pango mwambani.”[#13:4 Kama Yeremia atafuata amri hiyo ingembidi kusafiri karibu kilomita 1200 x 2 mpaka huko kwenye mto Eufrate na kurudi. Ndiyo maana baadhi ya wataalamu wa mambo ya Biblia wanafikiri “Eufrate” (Kiebrania hapa ni “Perat”) si kule Babuloni ila ni mahali paitwapo “Para” (rejea Yos 18:23), karibu na Anathothi. Wengine walifikiri hapa haihusu moja kwa moja kitendo cha ishara, ila maono, mfano au kitendawili kama vile Yer 25:15-29. Wengine wanafikiria juu ya kiigizo (drama) kama kile cha cha Eze 12:1-16; 21:18-22. Lakini muhimu ni ujumbe wote unaohusika hapa katika 6-7 na 8-11.]
5Basi, nikaenda na kukificha kikoi hicho karibu na mto Eufrate, kama Mwenyezi-Mungu alivyoniamuru.
6Ikawa, baada ya siku nyingi, Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Nenda kwenye mto Eufrate, ukakichukue kile kikoi nilichokuamuru ukifiche huko.”
7Basi, nikaenda kwenye mto Eufrate, nikachimbua na kukitoa kile kikoi mahali nilipokuwa nimekificha. Nilipokitoa, nilishangaa kukiona kuwa kilikuwa kimeharibika kabisa; kilikuwa hakifai tena.
8Ndipo neno la Mwenyezi-Mungu likanijia:[#13:8-11 Yaonekana kwamba watu wa Yuda ambao wanawakilishwa na kikoi cha Yeremia wataharibika au kuoza wawapo uhamishoni mbali na Mwenyezi-Mungu ambaye wangepaswa kuambatana naye kama kikoi cha Yeremia.]
9“Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hivi ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikubwa cha Yerusalemu.
10Watu hawa waovu wanakataa kusikia maneno yangu, na badala yake wanakuwa wakaidi na kufuata mawazo yao wenyewe. Wanaifuata miungu mingine, wanaitumikia na kuiabudu. Hao watakuwa kama kikoi hiki ambacho hakifai kitu.
11Kama vile kikoi kinavyoshikamana na kiuno cha mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami watu wa Israeli na watu wa Yuda, ili wajulikane kwa jina langu, wanisifu na kunitukuza. Lakini wao hawakunisikiliza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
12Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliniambia hivi: “Waambie watu wa Israeli kwamba kila mtungi utajazwa divai. Lakini utakapowaambia hivyo, wao watakujibu hivi: ‘Kwani unadhani sisi hatujui kwamba kila mtungi utajazwa divai?’[#13:12 Hiki bila shaka ni kitendawili au methali; madhumuni yake ni kwamba kila mtu atakumbwa na mambo yatakayotukia, au matukio yajayo yatampata kila mtu (Yer 1:13-16), kama aya ifuatayo (13) inavyofichua kidogo zaidi kwa mfano wa kuleweshwa, ambao wahusu hukumu ya Mungu (rejea Isa 51:17; Yer 25:15-29; 49:12; Eze 23:32-34; Ufu 16).]
13Nawe utawaambia kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawalewesha wenyeji wote wa nchi hii; wafalme wanaotawala mahali pa Daudi, makuhani, manabii na wakazi wote wa Yerusalemu.
14Nitawagonganisha wao kwa wao kina baba na watoto. Sitawahurumia, sitawaachia wala sitawarehemu, bali nitawaangamiza.”[#13:14 Katika Yer 19:1-13, Yeremia mwenyewe analivunja gudulia mbele ya watu (aya 10).]
15Enyi Waisraeli, sikilizeni kwa makini,
msiwe na majivuno maana Mwenyezi-Mungu anasema nanyi.
16Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
kabla hajawaletea giza,
nanyi mkajikwaa miguu kwenye milima ya giza.
Nyinyi mnatazamia mwanga,
lakini anaugeuza kuwa utusitusi
na kuufanya kuwa giza nene.
17Lakini kama msiponisikiliza,
moyo wangu utalia machozi faraghani,
kwa sababu ya kiburi chenu.
Nitalia kwa uchungu na kububujika machozi,
kwa kuwa watu wa Mwenyezi-Mungu wametekwa.
18Mwambie mfalme na mama yake hivi:[#13:18 Huyu labda ni Yehoyakini ambaye alitawala Yuda kwa miezi mitatu tu baada ya kifo cha baba yake mnamo mwaka 598 K.K. Yeye alichukuliwa mfungwa hadi Babuloni na hakuwahi kurudi tena nchini Yuda. Rejea Yer 52:31-34. “Mama yake”: Mama wa mfalme katika Israeli alikuwa na heshima zake za pekee (rejea 1Fal 19; 15:13). Kadiri ya 2Fal 24:8 mama yake Yehoyakini aliitwa Nehushta.]
“Shukeni kwenye viti vyenu vya enzi,
maana taji zenu nzuri zimeanguka vichwani mwenu.
19Miji ya Negebu imezingirwa;[#13:19 Eneo kame kati ya Israeli na Misri. Miji ya Negebu ilikuwa Kusini mwa Yuda, hivyo nayo ilishambuliwa na majeshi ya Nebukadneza (rejea 2Fal 24:10).]
hakuna awezaye kufungua malango yake.
Watu wa Yuda wamechukuliwa mateka,
wote kabisa wamepelekwa utumwani.”
20Inua macho yako, ee Yerusalemu!
Tazama! Madui zako waja kutoka kaskazini.
Kundi ulilokabidhiwa liko wapi?
Kundi lako zuri li wapi?
21Utasemaje juu ya wale uliodhani ni rafiki,
wale ambao wewe mwenyewe uliwafundisha,
watakapokushinda na kukutawala?
Je, si utakumbwa na uchungu
kama wa mama anayejifungua?
22Nawe utajiuliza moyoni mwako,
“Kwa nini mambo haya yamenipata?”
Sawa! Kama vazi lako limepandishwa juu,
nawe ukatendewa kwa ukatili mno,
hayo ni matokeo ya makosa yako mengi mno.
23Je, Mwethiopia aweza kubadili rangi yake,[#13:23 Rejea Isa 18:1-2 ambapo Ethiopia au Nubia ni jina la Kushi.]
au chui madoadoa yake?
Ikiwezekana, nanyi pia mnaweza kutenda mema,
nyinyi mliozoea kutenda maovu!
24Mwenyezi-Mungu atawatawanya kama makapi
yanayopeperushwa na upepo kutoka jangwani.
25Mwenyezi-Mungu asema:
“Hayo ndiyo yatakayokupata,
ndivyo nilivyoamua kukutenda mimi Mwenyezi-Mungu,
kwa sababu umenisahau mimi,
ukaamini miungu ya uongo.
26Nitalipandisha vazi lako hadi kichwani
na aibu yako yote itaonekana wazi.
27Nimeyaona machukizo yako:
naam, uzinifu wako na uzembe wako,
na uasherati wako wa kupindukia,
juu ya milima na mashambani.
Ole wako ee Yerusalemu!
Mpaka lini utakaa bila kutakaswa?”