The chat will start when you send the first message.
1Mfalme Nebukadneza wa Babuloni alimtawaza Sedekia mwana wa Yosia, kuwa mfalme wa Yuda mahali pa Konia mwana wa Yehoyakimu.[#37:1—45:5 Sura ya 37—45 zahusu nyakati za mwisho za utawala wa Yuda. Taz 2Fal 24:18—25:26.]
2Lakini Sedekia na maofisa wake pamoja na wananchi wa Yuda hawakusikiliza maonyo ya Mwenyezi-Mungu aliyotoa kwa njia ya nabii Yeremia.
3Mfalme Sedekia aliwatuma Yehukali mwana wa Shelemia, pamoja na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwa nabii Yeremia, wamwombe awaombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.[#37:3 Linganisha na Yer 38:1 ambapo waliosikia maneno ya Yeremia ni wengine. “Sefania, mwana wa Maaseia”: Yer 21:1-2; 29:24-32.]
4Wakati huo, Yeremia alikuwa bado ana uhuru kutembea miongoni mwa watu, maana alikuwa bado hajatiwa gerezani.
5Tena jeshi la Farao lilikuwa limeondoka Misri, na jeshi la Wakaldayo lililokuwa limeuzingira mji wa Yerusalemu liliposikia habari hizo liliondoka.[#37:5 Jeshi la Misri liliamriwa na Farao Hofra (588-569 K.K.) kuanza safari kuelekea Palestina ili kumsaidia mfalme Sedekia dhidi ya Wakaldayo. Wakaldayo waliacha mashambulizi yao dhidi ya Yerusalemu kwa muda. Rejea Yer 34:21.]
6Ndipo neno la Mwenyezi-Mungu likamjia nabii Yeremia:
7“Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Utamwambia hivi mfalme wa Yuda ambaye amekutuma uniombe kwa niaba yake: Tazama! Jeshi la Farao lililokuja kukusaidia, liko karibu kurudi makwao Misri.
8Na Wakaldayo watarudi kuushambulia mji huu. Watauteka mji na kuuteketeza kwa moto.
9Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kwamba msijidanganye wenyewe na kusema kwamba jeshi la Wakaldayo litaondoka; kweli halitaondoka.
10Hata kama mkilishinda jeshi lote la Wakaldayo wanaopigana nanyi, wakabaki majeruhi tu katika mahema yao, majeruhi hao watainuka na kuuteketeza mji huu kwa moto.”
11Jeshi la Wakaldayo lilipoondoka Yerusalemu kuliepa jeshi la Farao lililokuwa linakaribia,
12Yeremia aliondoka Yerusalemu kwenda nchi ya Benyamini ili kupokea sehemu ya urithi wake.[#37:12 Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania.]
13Alipokuwa katika lango la Benyamini, mlinzi mmoja aitwaye Iriya mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania, alimkamata Yeremia na kumwambia, “Wewe unatoroka uende kujiunga na Wakaldayo!”[#37:13 Labda lango Kaskazini mwa Yerusalemu lililoelekea eneo la kabila la Benyamini (rejea Yer 38:7), nalo si sawa na lango liitwalo kwa jina hilo hilo katika jumba la hekalu (rejea Yer 20:2).]
14Yeremia akamwambia, “Huo ni uongo! Mimi sitoroki na kwenda kujiunga na Wakaldayo.” Lakini Iriya hakusadiki maneno ya Yeremia. Basi akamtia nguvuni na kumpeleka kwa maofisa.
15Maofisa hao walimkasirikia sana Yeremia wakampiga, kisha wakamfunga gerezani katika nyumba ya katibu Yonathani iliyokuwa imegeuzwa kuwa gereza.[#37:15 Rejea Yer 37:20; 38:26.]
16Yeremia alipokuwa amefungwa gerezani kwa muda wa siku nyingi,
17mfalme Sedekia alimwita na kumkaribisha kwake. Mfalme akamwuliza kwa faragha wakiwa nyumbani mwake; “Je, kuna neno lolote kutoka kwa Mwenyezi-Mungu?” Yeremia akamjibu, “Naam! Lipo!” Kisha akaendelea kusema, “Wewe utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babuloni.”[#37:17 Kisa hiki chaonesha kwamba mfalme Sedekia bado alimfikiria Yeremia kuwa nabii wa kweli. Rejea Yer 21:1-2; 37:3.]
18Halafu Yeremia akamwuliza mfalme Sedekia, “Nimekukosea nini, au nimewakosea nini watumishi wako au watu hawa, hata unitie gerezani?
19Wako wapi manabii waliokutabiria wakisema, ‘Mfalme wa Babuloni hatakushambulia wewe wala nchi hii?’
20Sasa nakuomba unisikilize, ee bwana wangu mfalme. Nakusihi sana ulikubali ombi langu. Tafadhali usinirudishe tena gerezani katika nyumba ya katibu Yonathani, nisije nikafia humo.”
21Basi, mfalme Sedekia akatoa amri Yeremia awekwe katika ukumbi wa walinzi akawa anapewa mkate kila siku kutoka kwa waoka mkate mpaka mikate ilipotoweka kabisa huko mjini. Basi, Yeremia alibaki katika ukumbi wa walinzi.