The chat will start when you send the first message.
1Mwenyezi-Mungu alimwamuru Yeremia aende kusimama
2kwenye lango la hekalu lake Mwenyezi-Mungu na kutangaza ujumbe huu: “Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu enyi watu wa Yuda mnaoingia humu kumwabudu Mwenyezi-Mungu.[#7:2 Nabii anaorodhesha vipengele vya maadili vinavyotakiwa ili ibada inavyofanyika mahali patakatifu iwe kweli ya kukubalika kwa Bwana (rejea Zab 15; 24:3-6). Katika Yer 26 yanatajwa mazingira ambamo simulizi hili lilitangazwa najinsi lilivyochukuliwa na wale waliolisikia kwa mara ya kwanza.]
3Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Rekebisheni mienendo yenu na matendo yenu, nami nitawaacha mwendelee kukaa mahali hapa.
4Msitumainie maneno haya ya uongo: ‘Hili ni hekalu la Mwenyezi-Mungu, hekalu la Mwenyezi-Mungu, naam hekalu la Mwenyezi-Mungu.’[#7:4 Maneno haya ya aya 4 ambayo yanarudiwa mara kwa mara yanalaumu tegemeo na tumaini ambalo Waisraeli walikuwa nalo kuhusu hekalu. Ni bure kushikilia kivuli cha mahali patukufu kama mtu hatendi na kutekeleza haki na kushika amri za Bwana.]
5“Ila kama mkibadili mienendo yenu na matendo yenu, mkitendeana haki kwa dhati;
6kama mkiacha kuwadhulumu wageni, yatima au wajane au kuwaua watu wasio na hatia katika nchi hii; kama mkiacha kuabudu miungu mingine na kujiangamiza wenyewe,
7basi mimi nitawaacha daima mkae mahali hapa, katika nchi niliyowapa wazee wenu tangu zamani.
8“Lakini kumbe, mnayaamini maneno ya uongo bure.
9Mnaiba, mnaua, mnafanya uzinzi, mnaapa uongo, mnamfukizia mungu Baali ubani na kuabudu miungu mingine ambayo hamjapata kuijua.[#7:9 Kut 20:13-16; Kumb 5:17-20; Hos 4:2. “Miungu mingine ambayo hamjapata kuijua”: Rejea Kumb 11:28; 13:2,6-9; 28:64; Yer 19:4.]
10Kisha, mnakuja na kusimama mbele yangu, katika hekalu hili linalojulikana kwa jina langu na kusema; ‘Tuko salama,’ huku mnaendelea kufanya mambo hayo yanayonichukiza.
11Je, hekalu hili linalojulikana kwa jina langu limekuwa pango la wanyang'anyi? Jueni kuwa mimi nimeyaona yote mnayofanya![#7:11 Kwa picha hii ya kishairi, usalama wa uongo waliokuwa nao kuhusu hekalu unalaumiwa. Kama vile wezi na wanyang'anyi, mara wakishatenda kosa la jinai hukimbimbilia usalama mapangoni, kadhalika nao Waisraeli walijisikia wamelindwa na mahali patakatifu hekaluni Yerusalemu, mbali na matendo na uhalifu wao. Kuhusu matumizi ya msemo huo katika Agano Jipya rejea Mat 21:13; Marko 11:17; Luka 19:46.]
12Nendeni mahali pangu kule Shilo, mahali nilipopachagua niabudiwe hapo awali, mkaone maangamizi niliyoyafanya huko kwa sababu ya uovu wa watu wangu, Israeli.[#7:12 Mji katika eneo la Efraimu (taz Yos 16:4), yapata kilomita 30 kaskazini ya Yerusalemu. Humo liliwekwa sanduku la agano nyakati za Eli (Taz 1Sam 1:3). Mji huo uliangamizwa labda na Wafilisti ambao walilichukua lile sanduku la agano kama kinyago na kuliweka katika hekalu la miungu yao (rejea 1Sam 4). Taz pia Yos 18:1; Zab 78:60 maelezo; Yer 26:6.]
13Nyinyi mmefanya mambo hayo yote, na hata niliposema nanyi tena na tena hamkunisikiliza. Nilipowaiteni hamkuitika.
14Kwa hiyo, kama nilivyoutendea mji wa Shilo, ndivyo nitakavyolitendea hekalu hili linalojulikana kwa jina langu, hekalu ambalo nyinyi mnalitegemea; naam, mahali hapa ambapo niliwapa nyinyi na wazee wenu.[#7:14-15 Rejea Zab 78:56-67 ambapo kuna uhusiano na simulizi la Efraimu na kuteketezwa kwa hekalu la Shilo.]
15Nitawafukuzeni mbali nami kama nilivyowatupilia mbali ndugu zenu, wazawa wote wa Efraimu.
16“Nawe, Yeremia, usiwaombee watu hawa, usinililie kwa ajili yao, usiwaombee dua wala usinisihi kwa ajili yao, maana sitakusikiliza.[#7:16 Aya inasisitiza kwamba watu hawana hamu kabisa ya kubadili mwenendo wao na hivyo kuwaombea au kumsihi Mungu kwa ajili yao ni kazi bure. Rejea Yer 4:14, 17:1.]
17Je, wewe huoni mambo wanayofanya katika miji ya Yuda na katika mitaa ya Yerusalemu?
18Watoto huokota kuni, akina baba huwasha moto na akina mama hukanda unga ili waoke mikate kwa ajili ya mungu wa kike wanayemwita malkia wa mbinguni. Tena wanaimiminia miungu mingine tambiko ya divai ili kuniudhi.[#7:18 Mungu huyo wa kike aliabudiwa hapo kale kwa uhusiano wake na mambo ya jinsia na vyanzio vya uhai. Huko Mesopotamia aliitwa “Ishtar” na alifikiriwa kuwa sawa na sayari ya “Veno”. Huko Kanaani aliitwa “Ashtaroti” (taz Amu 2:13 maelezo). Kutaja watoto, mama na akina baba hapa yamkini kunaashiria kwamba ibada hiyo ilikuwa ya jamaa. Rejea Yer 44:17-19.]
19Lakini je, wanamwudhi nani? Mimi? Hata kidogo! Wanajiumiza wao wenyewe na kuchanganyikiwa!
20Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitaimwaga hasira yangu na ghadhabu yangu mahali hapa, juu ya wanadamu na wanyama, miti mashambani na mazao ya nchi. Itawaka na wala haitaweza kuzimwa.”
21Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Haya, ongezeni tambiko zenu za kuteketezwa juu ya sadaka zenu na kula nyama yake!
22Maana, siku nilipowatoa wazee wenu nchini Misri, sikuwaambia kitu wala kuwapa amri yoyote juu ya tambiko za kuteketezwa na sadaka.
23Lakini niliwapa amri hii: waitii sauti yangu ili niwe Mungu wao, nao wawe watu wangu. Niliwaamuru pia waishi kama nilivyowaagiza, ili mambo yao yawaendee vema.
24Lakini wao hawakunitii wala kunitegea sikio. Badala yake wakafuata fikira zao wenyewe na ukaidi wa mioyo yao, wakarudi nyuma badala ya kusonga mbele.
25Tangu siku ile wazee wenu walipotoka nchini Misri hadi leo, sijakoma kuwatuma kwenu watumishi wangu, manabii.
26Lakini hamkunisikiliza wala kunitegea sikio, ila mlizidi kuwa wakaidi, mkawa waasi kuliko hata wazee wenu.
27“Basi, wewe Yeremia utawaambia maneno haya yote, lakini wao hawatakusikiliza. Utawaita, lakini hawatakuitikia.
28Utawaambia; ‘Nyinyi ni taifa ambalo halikutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, wala kukubali kuwa na nidhamu. Kwenu uaminifu umekufa; umetoweka kabisa katika maneno yenu.’[#7:28 Au “kukubali kukosolewa”.]
29“Nyoeni nywele zenu enyi wakazi wa Yerusalemu, mzitupe;[#7:29 Neno la Kiebrania lilidokezea hasa nywele za wale waliojulikana kama wanazari ambao waliacha nywele zao zikue kwa kuonesha kwamba wao walikuwa wamewekwa wakfu kwa Mungu (rejea Hes 6:5). Amri hiyo ya kukata nywele zao ina maana: sasa Waisraeli (Yuda) wameacha kuwa watu waliowekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu. Katika mazingira mengine ya maandishi ya Biblia kukata nywele ni alama ya kuomboleza na mara nyingine kutubu. Rejea Yobu 1:20; Isa 15:2; Yer 48:37; Eze 7:18; Mika 1:16.]
fanyeni maombolezo juu ya vilele vya milima,
maana, mimi Mwenyezi-Mungu nimewakataa nyinyi,
mlio kizazi kilichosababisha hasira yangu!
30“Watu wa Yuda wametenda uovu mbele yangu. Wameweka vinyago vyao vya kuchukiza ndani ya nyumba hii ijulikanayo kwa jina langu, wakaitia unajisi.[#7:30 Rejea mambo aliyoyaona Ezekieli katika Eze 8.]
31Wamejenga madhabahu iitwayo ‘Tofethi’ huko kwenye bonde la mwana wa Hinomu, wapate kuwachoma sadaka watoto wao wa kiume na wa kike humo motoni. Mimi sikuwa nimewaamuru kamwe kufanya jambo hilo, wala halikunijia akilini mwangu.[#7:31 Maana ya neno au jina hili si dhahiri lakini ni mahali ambapo kwa wakati na mazingira kadha wa kadha walitambika binadamu. Rejea 2Fal 23:10; Yer 32:35. “Bonde la Mwana wa Hinomu”: Taz Yer 2:23 maelezo. “Sikuwa nimewaamuru … halikunijia akilini mwangu”: Lawi 18:21; Isa 57:5; Yer 19:5.]
32Kwa sababu hiyo, siku zaja ambapo hawataliita tena ‘Tofethi,’ au ‘Bonde la Mwana wa Hinomu,’ bali wataliita ‘Bonde la Mauaji.’ Huko ndiko watakakozika watu, kwa sababu hapatakuwa na mahali pengine pa kuzikia.[#7:32 Yer 19:6. Maadui wa Yuda walisababisha mauaji makubwa na maiti ziliachwa bila kuzikwa kwenye Bonde la Mwana wa Hinomu (rejea aya 32b-33) na hivyo kutia unajisi mahali walipoabudu mungu aitwaye Moloki (rejea 2Fal 23:16).]
33Maiti za watu hao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa porini, na hapatakuwa na mtu atakayewafukuza.[#7:33 Adhabu inayotangazwa hapa ni kali. Kwa Waisraeli kufa na kukosa kuzikwa ilikuwa jambo la kutisha mno miongoni mwa mabaya yaliyompata binadamu. Rejea Kumb 28:26; Yer 8:1-2; 9:22; 16:4; 19:7; 34:20.]
34Nchi itakuwa jangwa na katika miji ya Yuda na mitaa ya Yerusalemu nitakomesha sauti zote za vicheko na furaha, sauti za bwana arusi na bibi arusi, kwa sababu nchi itakuwa ukiwa.