Yobu 15

Yobu 15

Hoja ya pili ya Elifazi

(15:1—21:34)

1Kisha Elifazi, Mtemani, akajibu:[#15:1 Taz maelezo ya 2:11.; #15:1—21:34 Katika duru ya pili ya mazungumzo (15:1-21:34), kwa mara nyingine tena, tuna mfululizo wa hoja baina ya Yobu na rafiki zake: Elifazi (sura 15), Yobu (sura 16—17), Bildadi (sura 18), Zofari (sura 20), Yobu (sura 21).]

2“Je, mtu wa hekima hujibu kwa maneno ya upuuzi?

Je, mtu huyo amejaa maneno matupu?

3Je, mwenye hekima hujitetea kwa maneno yasiyofaa,

au kwa maneno yasiyo na maana?

4Lakini wewe unapuuza uchaji wa Mungu;

na kuzuia kutafakari mbele ya Mungu.

5Uovu wako ndio unaokifundisha kinywa chako,

nawe wachagua kusema kama wadanganyifu.

6Maneno yako mwenyewe yanakuhukumu, sio mimi;

matamshi yako yashuhudia dhidi yako.

7Je, wewe ni mtu wa kwanza kuzaliwa?[#15:7 Hili ni swali lisilodai jibu. Elifazi anataka kusema Yobu kamwe si mtu wa kwanza kuzaliwa na kushuhudia ulimwengu ukiumbwa na hivyo kujipatia hekima.]

Je, wewe ulizaliwa kabla ya kuweko vilima?

8Je, ulipata kuweko katika halmashauri ya Mungu?[#15:8 Yaani malaika na wengine ambao hukutana kuzungumza mambo na Mungu (taz 1:6; 2:1). Rejea Isa 40:13; Yer 23:18; Rom 11:34.]

au, wewe ndiwe peke yako mwenye hekima?

9Unajua kitu gani tusichokijua sisi?

Unafahamu kitu gani tusichokifahamu sisi?

10Miongoni mwetu wapo wazee wenye hekima,[#15:10 Katika utamaduni wa Waisraeli kama vile pia katika tamaduni nyingi za Kiafrika, uzoefu ambao huandamana na uzee ulichukuliwa kuwa chanzo cha hekima na maarifa (taz 8:8; 12:12-13; Zab 119:100).]

wenye miaka mingi kuliko baba yako.

11Je, faraja anazokupa Mungu ni ndogo mno?

Au je, neno lake la upole kwako si kitu?

12Mbona moyo unakusukuma kukasirika

na kutoa macho makali,

13hata kumwasi Mungu

na kusema maneno mabaya kama hayo?

14Mtu ni nini hata aweze kuwa mwadilifu?

au yule aliyezaliwa na mwanamke hata aweze kuwa mwema?

15Ikiwa Mungu hawaamini hata watakatifu wake,

nazo mbingu si safi mbele yake,

16sembuse binadamu aliye kinyaa na mpotovu

binadamu atendaye uovu kama kunywa maji!

17“Sasa nisikilize, nami nitakuonesha,

nitakuambia yale niliyoyaona,

18mafundisho ya wenye hekima,

mambo ambayo wazee wao hawakuyaficha,

19ambao Mungu aliwapa hiyo nchi peke yao,

wala hakuna mgeni aliyepita miongoni mwao.

20Mwovu atateseka kwa maumivu siku zote,

miaka yote waliyopangiwa wakatili.

21Sauti za vitisho zitampigia kelele masikioni,

anapodhani amestawi mwangamizi atamvamia.

22Mwovu hana tumaini la kutoka gizani;

mwisho wake ni kufa kwa upanga.

23Hutangatanga kutafuta chakula,

akisema, ‘Kiko wapi?’

Ajua kwamba siku ya giza inamkaribia.

24Taabu na uchungu, vyamtisha;

vyamkabili kama jeshi la mfalme anayeshambulia.

25Kwa sababu amenyosha mkono wake dhidi ya Mungu;[#15:25 Kitendo hiki, kama vile mstari wa pili wa aya hii unavyosema dhahiri, ni ishara ya kiburi na majivuno dhidi ya Mungu (rejea Yobu 22:17).]

akadiriki kumpinga huyo Mungu mwenye nguvu;

26alikimbia kwa kiburi kumshambulia,

huku ana ngao yenye mafundo makubwa.

27Uso wake ameunenepesha kwa mafuta,

na kiuno chake kimejaa mafuta.

28Ameishi katika miji iliyoachwa tupu,

katika nyumba zisizokaliwa na mtu;

nyumba zilizotakiwa ziwe lundo la uharibifu.

29Mtu huyo kamwe hatakuwa tajiri;

wala utajiri wake hautadumu duniani.

30Hatalikwepa giza la kifo.

Ndimi za moto zitakausha chipukizi zake,

maua yake yatapeperushwa na upepo.

31Heri aache kutumainia upuuzi na kujidanganya,

maana upuuzi ndio utakaokuwa tuzo lake.

32Atalipwa kikamilifu kabla ya kufa kwake,

na wazawa wake hawatadumu.

33Atakuwa kama mzabibu unaopukutisha zabibu mbichi,

kama mzeituni unaoangusha maua yake.

34Wote wasiomcha Mungu hawatapata watoto,

moto utateketeza mahema ya wala rushwa.

35Wanatunga udanganyifu na kuzaa uovu.

mioyo yao hupanga udanganyifu.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania