Yobu 26

Yobu 26

Jibu la Yobu

1Kisha Yobu akajibu:[#26:1-4 Yobu, kwa mara nyingine tena, anasisitiza kwamba hana hatia. Inawezekana kwamba simulizi hili la Yobu hapa linafuatiwa na lile la 27:1-12.]

2“Aa! Jinsi gani ulivyomsaidia asiye na uwezo!

Jinsi gani ulivyomwokoa asiye na nguvu!

3Jinsi gani ulivyomshauri asiye na hekima,

na kumshirikisha ujuzi wako!

4Lakini umetamka hayo kwa ajili ya nani?

Nani aliyekusukuma kuongea hivyo?” Uwezo mkuu wa Mungu

Bildadi akajibu:

5“Mizimu huko chini yatetemeka,[#26:5-14 Katika makala ya Kiebrania inaonekana kwamba Yobu ndiye anayeongea katika aya hizi; hata hivyo yawezekana kwamba zinapatana zaidi na mazungumzo ya Bildadi katika 25:1-6.]

maji ya chini na wakazi wake yaogopa.

6Kuzimu kuko wazi kabisa mbele ya Mungu.

Abadoni haina kifuniko chochote.

7Mungu hutandaza kaskazini mahali patupu,[#26:7 Kiebrania ni “Safon”, neno ambalo linatumiwa pia katika Zab 48:2 na hasa Isa 14:13.]

na hutundika dunia mahali pasipo na kitu,

8huyafunga maji mawinguni yawe mazito,

nayo mawingu hayapasuki kwa uzito wake.

9Huufunika uso wa mwezi

na kutandaza juu yake wingu.

10Amechora duara juu ya uso wa bahari,

penye mpaka kati ya mwanga na giza.

11Mungu akitoa sauti ya kukemea,

nguzo za mbingu hutetemeka na kustaajabu.

12Kwa nguvu zake aliituliza bahari;

kwa maarifa yake alimwangamiza dude Rahabu.

13Kwa pumzi yake aliisafisha anga;

mkono wake ulilichoma joka lirukalo.

14Yamkini haya ni machache tu ya matendo yake,

ni minong'ono tu tunayosikia juu yake.

Nani awezaye kujua ukuu wa nguvu yake?”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania