The chat will start when you send the first message.
1Mwenyezi-Mungu alimwita Mose na kuongea naye katika hema la mkutano, akamwambia,[#1:1—7:38 Kama inavyoonekana katika sehemu hii, mambo ya matambiko yalikuwa ibada muhimu sana kati ya mambo ya sherehe za kidini katika jumuiya ya kale ya Waisraeli. Sura hizi zinapanga jinsi matoleo, sadaka au matambiko mbalimbali yalivyopaswa kufanyika. Miongoni mwa matambiko au sadaka muhimu zaidi ni zile za kuteketezwa (sura 1), za nafaka (sura 2) na za amani au za muungano (sura 3).]
2“Waambie Waisraeli kwamba kama mtu anapenda kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya mnyama, mnyama huyo atamchagua kutoka kundi lake la ng'ombe, kondoo au mbuzi.[#1:2 Ilikuwa kawaida katika dini za mataifa ya Mashariki ya Kati ya Kale watu kutolea sadaka au kuitambikia miungu yao kama tendo la kuonesha shukrani kwa miungu hiyo au kama tendo lililoambatana na maombi, k.m. ya amani, upatanisho, rutuba, n.k. Desturi hiyo ilikuweko pia katika mataifa mengi hata ya Afrika ambapo sana sana watu waliwatambikia wazee wao waliokufa zamani. Katika Biblia Waisraeli walitahadharishwa wasiitambikie miungu mingine ila Mwenyezi-Mungu peke yake. Agano jipya linaweka kando aina zote za matambiko kwa kumweka Yesu ambaye, kwa kifo chake, amekuwa ndiye tambiko au sadaka iliyotosha kuwapatanisha watu na Mungu (taz Ebr 4:14—5:10). Katika barua hiyo Yesu Kristo ni mtambikaji wetu mkuu naye pia amefanywa kuwa tambiko ambalo kwalo binadamu wanaondolewa dhambi zao.]
3“Kama sadaka anayotoa mtu ni ya kuteketezwa, atamchagua mnyama dume asiye na dosari kutoka kundi lake, atamtolea mbele ya mlango wa hema la mkutano ili apate fadhili ya Mwenyezi-Mungu;[#1:3 Hii ilikuwa sadaka iliyochomwa yote juu ya madhabahu. Sadaka hizo, hapo kale, zilikuwa njia ambayo watu walitaka kurudisha uhusiano kati ya anayetambikia na mungu anayetambikiwa. Kabla ya wakati wa Waisraeli matambiko hayo yalitolewa au kuongozwa na mkuu wa familia au ukoo hasa katika makabila ambayo hayakuwa na kikundi cha makuhani au makasisi ambao walikuwa na wajibu huo.]
4ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mnyama wa sadaka ya kuteketezwa, ambayo itakubaliwa kwa ajili ya kumfanyia huyo mtu upatanisho.[#1:4 Hicho kilikuwa kitendo cha kuashiria kwamba mnyama huyo ametolewa kwa niaba ya anayemtoa. Pengine pia kitendo hicho kilimaanisha kwamba dhambi za mwenye kutambikia ziliwekewa huyo mnyama na kwamba Mungu kwa kukubali hiyo sadaka anamwondolea dhambi mhusika.; #1:4 Dhambi ni kitu kinachosababisha utengano kati ya Mungu na binadamu na ni kuasi sheria ya Mungu. Makuhani wa Waisraeli walitambika wanyama kana kwamba hao wanyama walichukua dhambi za watu na adhabu ambayo watu wangalipaswa kupata (taz pia 4:1-7).]
5Kisha, atamchinja huyo ng'ombe mbele ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani, wazawa wa Aroni, wataichukua damu na kuinyunyizia madhabahu mlangoni mwa hema la mkutano, pande zake zote.[#1:5 Aroni, nduguye Mose, alikuwa kuhani mkuu wa kwanza katika Israeli (Kut 27:21—28:13) na wazawa wake walitazamiwa kuwa makuhani.; #1:5 Damu ilifikiriwa kuwa yenye uhai (taz Mwa 9:4-5); ilichukuliwa kuwa takatifu na ilikuwa marufuku kuila (Lawi 7:26; 17:10-14). Kumtolea Mungu hiyo damu ilikuwa njia ya kumtambua Mungu kama chanzo cha uhai na kwamba viumbe vyote ni vyake (rejea Zab 50:8-14). Ilichukuliwa pia kuwa na nguvu ya kumlinda mtu (Kut 4:25) na ilikuwa ishara ya uhusiano bora kati ya Mungu na watu. Kwa makabila mengine hata ya Afrika damu ilitumiwa kuweka uhusiano kati ya mtu na mtu ambao kwa vingine hawakuwa na uhusiano.]
6Huyo mtu atamchuna huyo mnyama wa sadaka ya kuteketezwa na kumkata vipandevipande.
7Hao makuhani wazawa wa Aroni watazipanga kuni juu ya madhabahu na kuwasha moto.
8Kisha makuhani hao watachukua vile vipande vya nyama, kichwa na mafuta, na kuviweka juu ya kuni juu ya madhabahu.
9Lakini matumbo na miguu ya mnyama huyo mtu ataviosha kwa maji. Kuhani ataiteketeza sadaka yote juu ya madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.
10“Kama sadaka yake ya kuteketezwa ataitoa katika kundi la kondoo au mbuzi, basi, atachagua dume asiye na dosari.
11Atamchinjia upande wa kaskazini wa madhabahu, mbele ya Mwenyezi-Mungu, hao makuhani, wazawa wa Aroni watainyunyizia madhabahu damu pande zake zote.
12Kisha huyo mtu atamkata vipandevipande, akivitenga kichwa pamoja na mafuta yake, na kuhani ataviweka kwenye moto juu ya madhabahu.
13Lakini matumbo na miguu yake ataviosha kwa maji. Kuhani ataiteketeza yote juu ya madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.
14“Ikiwa anamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa ya ndege, basi, ataleta sadaka yake ya hua au kinda la njiwa.
15Kuhani atamleta ndege huyo kwenye madhabahu, atamkongonyoa kichwa chake na kukiteketeza juu ya madhabahu. Damu yake itanyunyiziwa ubavuni mwa madhabahu.
16Kibofu chake pamoja na uchafu wake ataviondoa na kutupa upande wa mashariki wa madhabahu ambako majivu huwekwa.
17Atamshika mabawa na kumpasua, lakini asimkate vipande viwili. Kisha, kuhani atamteketeza kwenye madhabahu, juu ya kuni. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.”