Walawi 12

Walawi 12

Kuwatakasa wanawake baada ya kujifungua

1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

2“Waambie watu wa Israeli hivi: Mwanamke akipata mimba, akajifungua mtoto wa kiume, atakuwa najisi kwa muda wa siku saba kulingana na siku zake zihusikanazo na hali ya wanawake.[#12:2-6 Mama aliyejifungua mtoto alichukuliwa kuwa si safi kidini na kimila kwa siku saba. Katika aya ya 5 siku za kubaki najisi zimeongezwa ikiwa mtoto ni wa kike lakini sababu ya tofauti hiyo si dhahiri.]

3Mtoto huyo atatahiriwa katika siku yake ya nane.

4Kisha mama mtoto ataendelea kuwa najisi kwa muda wa siku thelathini na tatu. Wakati huo, kamwe asiguse chochote kilichowekwa wakfu wala kuingia mahali patakatifu mpaka siku za kutakasika kwake zitakapotimia.

5Lakini, kama amejifungua mtoto wa kike, basi, atakuwa najisi kwa muda wa majuma mawili kama ilivyo anapokuwa katika siku zake. Ataendelea katika kutakasika kwake kwa muda wa siku sitini na sita.

6“Siku za kutakaswa kwake zitakapotimia, iwe amepata mtoto wa kiume au wa kike, atamletea kuhani mlangoni mwa hema la mkutano mwanakondoo wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na kinda la njiwa au hua, kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi.[#12:6 Sadaka hiyo na matoleo mengine yanayotajwa hapa ambayo yote yanaunganishwa na ibada ya kutakaswa kwake yalimpa mama huyo fursa ya kwenda tena mahali pa ibada. Taz pia Luka 2:24.]

7Kuhani atamtolea mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumfanyia huyo mama ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu. Hivyo huyo mwanamke atakuwa safi kutokana na damu yake. Huo ni mwongozo kuhusu mwanamke yeyote anayejifungua mtoto wa kiume au wa kike.

8“Kama hawezi kutoa mwanakondoo, basi, ataleta hua wawili au makinda mawili ya njiwa; mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuondolea dhambi. Kuhani atamfanyia mama huyo ibada ya upatanisho, naye atakuwa safi.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania