Luka 1

Luka 1

1Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu.[#1:1-4 Dibaji hii inafanana na dibaji za kawaida za maandishi fasaha ya wanahistoria Wagiriki wa nyakati hizo. Luka anatamka kusudi au lengo la Injili. Mwandishi ambaye yeye binafsi hakushuhudia matukio hayo, anataja chimbuko la Injili yake au mahali alipopata habari zenyewe, yaani maandishi yaliyotangulia na habari alizopata kwa wale ambao wao wenyewe walishuhudia matukio hayo juu ya Yesu (Ling na Mate 1:1). Luka, tofauti na waandishi wengine, anatuambia kwamba ameandika habari hizo kwa mpango (aya ya 3).; #1:1 Mtu ambaye Luka, kwa heshima yake anaandika kitabu hiki (ling pia Mate 1:1), na ambaye hatuna habari zaidi juu yake. Yamkini alikuwa mkristo aliyeheshimika katika jumuiya. Maana ya Theofilo ni au: .; #1:1-4 Sehemu hii ya Injili ni kama “Dibaji” ya Injili hii. Mwandishi Luka ambaye hakushuhudia kwa macho yake mwenyewe matukio kuhusu Yesu Kristo, anataja alikopata habari za Injili aliyoandika: alizipata kutoka kwa maandishi ya watu wengi waliotangulia kuandika habari hizo na pia mapokeo yaliyokuwa na msingi wake katika watu wale ambao walishuhudia matukio hayo. Rejea Mate 1:1.kwa jumla anamfuata Marko pamoja na marekebisho au mabadiliko kadhaa 3:19-20; 4:16-30; 5:1-11; 6:12-19; 22:31-34. Pia alifuata mapokeo mengine.]

2Waliyaandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona mambo hayo kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo.

3Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango,

4ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa.[#1:4 Ni tafsiri ya neno la Kigiriki ambalo katika fasiri ya neno kwa neno ni “neno”. Lakini katika Biblia “neno” huchukua maana mbalimbali kadiri ya matumizi yake na ni sharti ijulikane hivyo. Pengine na mara nyingi “neno” lafasiriwa barabara kwa neno la Kiswahili ujumbe. Luka 7:17 “neno” ni “habari”.; #1:4 Kwa tafsiri nyingine yamkini: Lakini kama “uliyofundishwa” ni maana yake halisi, itadhihirisha kwamba Theofilo alikuwa mkristo (mwaamini); wengine wadhani alikuwa ofisa fulani maarufu aliyetaka tu kuelezwa habari za Yesu Kristo.]

Ahadi ya kuzaliwa kwa Yohane

5Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha ukuhani cha Abiya. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni.[#1:5 Herode aitwaye Mkuu. Alikuwa mfalme wa eneo lote la Israeli lililokuwa chini ya mamlaka ya Waroma. Alitawala tangu mwaka 37 mpaka 4 K.K. Alikuwa baba yao Arkelao, Herode Antipa na Filipo. Wakati unaotajwa hapa ni wa kukisia tu.; #1:5 Yaani nchi ya Wayahudi pamoja na sehemu ya Galilaya.; #1:5 Kiebrania maana yake “Mwenyezi-Mungu amekumbuka”.; #1:5 Mojawapo ya vikundi vya zamu 24 vya kikuhani (2Nya 24:10). Kila kikundi cha zamu cha kuhudumu hekaluni kilitoa huduma yake mara mbili kwa mwaka kwa juma moja. Zakaria alikuwa wa kikundi cha nane.; #1:5 Luka anaweka habari za Yohane na Yesu sambamba (kuzaliwa kwa Yohane/kuzaliwa kwa Yesu n.k.) ili kudhihirisha umaarufu wake na kulinganisha.]

6Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama.[#1:6 Tafsiri ya neno la Kigiriki lenye maana hiyo au: “wema” au “waadilifu”, “wenye kuzingatia sheria ya Mungu,” kama maneno yafuatayo yanavyoonesha.]

7Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana.[#1:7 Katika Biblia tunakumbana mara kwa mara na kina mama fulani ambao walikuwa tasa wakajaliwa watoto kwa namna ya pekee: Sara (Mwa 21), Rebeka (Mwa 25).]

8Siku moja, ilipokuwa zamu yake kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu,[#1:8 Au:]

9Zakaria alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani.[#1:9 Kulikuwa na makuhani wengi (wapata 1800) ambao kwa jumla kila mmoja alipata nafasi ya kutoa ubani mara moja au mara mbili tu maishani mwake.; #1:9 Luka anatumia neno ambalo laweza kutumika kutaja “mahali patakatifu” ndani ya hekalu palipokuwa na madhabahu, au ndani kabisa palipoitwa patakatifu kabisa, sehemu iliyotenganishwa na hiyo nyingine kwa pazia (taz 23:45). Yamkini ni sehemu hiyo ya kwanza inayomaanishwa hapa, maana sehemu ya pili, ndani, ni kuhani mkuu peke yake aliyeruhusiwa kuingia, tena mara moja kwa mwaka (tazama Ebr 9:6-7).; #1:9 Ubani ulichomwa juu ya madhabahu iliyokuwa mbele ya mahali patakatifu (Kut 30:1-8; 1Fal 7:48-50). Hiyo ilifanyika asubuhi na jioni. Kuweko kwa watu wengi wakati huu (aya 10) kunabainisha kwamba labda wakati huo ulikuwa jioni.]

10Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani.

11Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani.[#1:11 Jina la malaika huyo tunaambiwa katika aya ya 19 kuwa ni Gabrieli. Malaika, ni “mjumbe”, wa Mungu. Mara nyingine katika A.K. malaika na Mungu ni kitu kimoja (taz Mwa 16:7-13 n.k.). Mwanzoni, kuweko kwa malaika kulimaanisha kutokea kwa Mungu mwenyewe; hiyo ilikuwa namna ya kuwaeleza binadamu kuweko kwake Mungu mwenyewe. Lakini baadaye malaika amedhihirika kuwa kiumbe kamili cha mbinguni (Zek 1:11-14).; #1:11 Upande wa kulia ni upande wa bahati njema; ndio kusema tokeo hilo halikuwa la ubaya au la hatari kwa Zakaria!]

12Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.[#1:12 Luka, aghalabu, anapenda sana kuingiza jambo la hofu, juu ya mambo ya kiroho, katika masimulizi yake mengi: 1:29-30,65; 2:9-10; 4:36; 5:8-10,26; 7:16; 8:25,33-37,56; 9:34,43; 24:37; Mate 2:43; 13:10; 5:5,11; 10:4; 19:17]

13Lakini malaika akamwambia, “Zakaria, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane.[#1:13 Namna ya kawaida katika A.K. ya kuwatia moyo wenye kuogopa wanapokumbana na mambo ya mbinguni.; #1:13 Hapa haisemwi sala yenyewe iliombwa nini au ilihusu nini, lakini kutokana na makala hii hapa, licha ya kwamba Zakaria, kama kawaida ya huduma ya makuhani aliomba fanaka ya Israeli, huenda alikuwa ameomba pia ajaliwe mtoto.; #1:13 Kiebrania Yohane maana yake “Mungu amefadhili” au “Mungu hurehemu” au “hufadhili”. Kama majina mengine yanayochaguliwa na viumbe wa mbinguni (taz Mwa 16:11; Isa. 7:14; 1Fal 13:2 n.k.), jina la huyo Yohane lagusia au kudokezea jambo atakalofanya Mungu kwa njia yake; Mungu atawahurumia watu na kukumbuka agano lake (1:72).]

14Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.

15Atakuwa mkubwa mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake.[#1:15 Yaonekana kwamba Yohane alikuwa kama aliyefungwa kwa nadhiri yaani aliyewekewa wakfu kwa Mungu (tazama Hes 6:1-4) kama Samueli (1Sam 1:11). Kama Luka alikuwa akifikiria juu ya habari za Samueli hapa basi, bila shaka, na jambo la huyo Yohane kuwa msemaji wa Mungu, yaani nabii ndilo analogusia hapa pia. Kwa maana kule kunamaanisha hasa kuwa chini ya nguvu au msukumo au uongozi wa nguvu ya Mungu kama manabii; linganisha 1:41,67; Mate 2:4; 4:8,31; 7:55; 9:17; 13:9.; #1:15 Katika Injili yake, Luka anayo nafasi za pekee kwa kazi ya Roho Mtakatifu (1:35,41,67; 2:25-27; 3:16,22; 4:1,14,18; 10:21; 11:13; 12:12; taz pia yaliyosemwa katika utangulizi wa kitabu cha Matendo).]

16Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao.[#1:16 Aya hiyo yaonesha jukumu la Yohane katika maisha yake.]

17Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama ya Elia. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake.”[#1:17 Yohane hakuwa Elia ila alikuwa kama yeye katika mahubiri yake. Katika Malaki 4:5 Elia anasemwa kuwa mjumbe atakayetumwa kabla ya “siku ile kuu ya kutisha ya Mwenyezi-Mungu”.]

18Zakaria akamwambia huyo malaika, “Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu.”

19Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu; nimetumwa niseme nawe, nikuletee hizi habari njema.[#1:19 Mmoja wa malaika watatu wanaotajwa kwa jina katika A.K. (Wengine ni Mikaeli: taz Dan 10:13, na Rafaeli). Jina Gabrieli linamaanisha: “Shujaa ni Mungu”. Katika Dan 8:16-17 na 9:21-27 yeye ni mtangazaji wa wokovu.; #1:19 Yaani na Mungu. Mara nyingi matumizi ya kitenzi katika kauli ya kutendewa ni njia mojawapo ya kuepa kumtajataja Mungu.; #1:19 Luka anatumia hapa kwa mara ya kwanza neno la Kigiriki ambalo latumika kwa maana ya kuhubiri Injili au Habari Njema.]

20Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia.”

21Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakaria huku wakishangaa juu ya kukawia kwake hekaluni.

22Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu.[#1:22 Yamkini ilijulikana kwamba yeye amekuwa bubu kwa vile hakuweza kuwatakia watu baraka ile ya kikuhani ambayo walikuwa wanaingojea kama kawaida. Tena walidhani alikuwa ameona maono maana katika mazingira hayo bila shaka, kama ilivyofikiriwa, huwa mtu amekutana na maono fulani!]

23Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani.[#1:23 Muda wa kushika zamu ya huduma ulikuwa juma moja.]

24Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema:[#1:24 Hatuna habari yoyote juu ya desturi ya jambo la kujificha, ila yawezekana lengo lake ni kuingiza hapa habari za Maria kwenda kumtembelea Elisabeti au kuificha siri hiyo hadi hapo itakapofichuliwa.]

25“Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu.”[#1:25 Kutokupata watoto, au kuwa tasa, kulifikiriwa na Wayahudi kuwa jambo ambalo lilionesha kutopendezwa kwa Mungu na mhusika; na mara nyingi hilo lilisababisha madharau kutoka kwa watu (Mwa 30:23; 1Sam 1:1-18).]

Ahadi ya kuzaliwa kwa Yesu

26Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya,[#1:26 Yaani tangu Elisabeti alipochukua mimba (aya 24).; #1:26 Tazama 1:11,19; #1:26 Wakati huo mji Nazareti ulikuwa na watu wachache katika milima ya Galilaya, kaskazini mwa Palestina.]

27kwa msichana mmoja bikira aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi.[#1:27 Hapa ni tafsiri ya neno la Kigiriki ambalo maana yake ya kawaida ni “bikira” au kwa zamani kidogo “mwanamwali”, yaani mtoto wa kike aliyekwisha balehe lakini hajaolewa na hivyo anachukuliwa kidesturi kuwa bikira. Hivyo, kuzaliwa kwa Yesu kunaoneshwa dhahiri kuwa tukio la pekee.; #1:27 Alikuwa ameposwa. Desturi ya huko Palestina nyakati hizo ilikuwa na hatua mbalimbali za kuoana: (a) Ahadi ya kuoana mbele ya mashahidi ambayo hufanywa na kulipwa kwa mahari (b) Harusi yenyewe ambayo hufanyika kwa kuchukuliwa kwa msichana nyumbani kwa huyo mumewe. Ahadi ya kuoa ikishafanyika mwanamume aliyehusika alikuwa na haki kisheria juu ya huyo mchumba wake ambaye aliitwa wakati huo “mke” wake. Uhusiano huo uliweza kubatilika tu kwa talaka. Baada ya kuchumbiwa huyo msichana aliweza kubaki nyumbani kwa wazazi wake hata kwa mwezi mmoja.; #1:27 Neno kwa neno: nyumba hapa ikimaanisha ukoo.]

28Malaika akamwendea, akamwambia, “Salamu, ewe uliyejaliwa neema na Mungu! Bwana yuko nawe!”[#1:28 Au neno kwa neno: “Furahi”. Katika Kigiriki lilikuwa neno la kawaida la kusalimu.; #1:28 Au: Neno lenyewe latumika pia katika Efe 1:6 na maana ya “kupendelewa”, “kujaliwa neema”. Hapa laweza kuwa limetumika kama kisifa cha Maria: “Mpendelewa”, “Mjaliwa neema”.]

29Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno hayo yanamaanisha nini?

30Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema.

31Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu.[#1:31 Katika aya hii kuna uhusiano na Isa 7:14. Jina la linachukua mahala pa Imanueli. Jina hilo ambalo latokana na Kigiriki (sawa na Kiebrania: “Yeshuah”), lina maana ya “Mwenyezi-Mungu aokoa”. Taz pia 2:11,21; Zab 130:8.]

32Yeye atakuwa mkubwa na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake.[#1:32 Neno kwa neno “Mwana wa Aliye Juu ya Yote”. Maneno “Aliye Juu ya Yote” yanamtaja Mungu, na katika tafsiri hii tumeweka wazi. Katika A.J. latumiwa tu na Luka (Luka 1:35,76; 6:35; 8:28; Mate 7:48; 16:17).]

33Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”

34Maria akamjibu, “Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?”[#1:34 Neno kwa neno: yaani hajakutana na mwanamume kimwili. Hoja ya Maria inasababisha maelezo zaidi kutoka kwa malaika.]

35Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu.[#1:35 Katika A.K. Roho Mtakatifu - Roho wa Mungu ni sawa na Nguvu ya Mungu ambayo huumba viumbe. Hapa basi Roho Mtakatifu na uwezo wake Mungu zinataja kitu kilekile sio vitu viwili Roho na Uwezo! - uwezo wa Mungu ambao hufanya visivyokuwako vikawa.; #1:35 Msemo ambao unagusia sehemu kadha wa kadha za A.K. ambazo zinahusu kutokea kwa Mungu na kuwako kwake kwa mfano wa wingu ambalo hutua juu ya mahala fulani na kupatia kivuli (Kut 40:35). Angalia pia 9:34-35 na sehemu sambamba za Injili.; #1:35 Yaani aliyetengwa au kuwekwa kando kwa ajili ya Mungu; aliyewekwa wakfu (taz pia 2:23).; #1:35 Taz 1:32.]

36Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa.[#1:36 Si dhahiri Maria alikuwa na ujamaa gani na Elisabeti.]

37Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu.”[#1:37 Tafsiri ya Kigiriki “rema” maana yake neno au tamko, nalo latokana na Kiebrania ambako latumika kwa maana kadhaa: “neno, kitu, jambo”.]

38Maria akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema.” Kisha yule malaika akaenda zake.[#1:38 Hali ya chini ambayo mwenyewe yu tayari kufuata matakwa ya Bwana wake. Hapa: “Bwana” ni jina la cheo linalomtaja Mungu (taz Luka 1:48; Mate 2:18 na pia 1Sam 1:11 maneno ya Hana).]

Maria anamtembelea Elisabeti

39Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yudea.

40Huko, aliingia katika nyumba ya Zakaria, akamsalimu Elisabeti.

41Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu,

42akasema kwa sauti kubwa, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa.

43Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?

44Nakuambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha.

45Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokuambia.”

Utenzi wa Maria

46Naye Maria akasema,

“Moyo wangu wamtukuza Bwana,

47roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

48Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu.

Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

49Kwa kuwa Mungu Mwenye Nguvu amenifanyia makuu,

jina lake ni takatifu.

50Huruma yake kwa watu wanaomcha

hudumu kizazi hata kizazi.

51Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:

amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

52amewashusha wenye nguvu kutoka viti vyao vya enzi,

akawakweza wanyenyekevu.

53Wenye njaa amewashibisha mema,[#1:53 Siyo tu mema ya kimwili bali pia mema ya Kristo (tazama pia Zab 107:9 na 1Sam 2:5). Hali hii ya nyakati mpya ya Mungu kujihusisha na maisha ya watu kwa kusimika utawala wake kati yao inasababisha mabadiliko katika maisha yote ya watu.]

matajiri amewaondoa mikono mitupu.

54Amemsaidia Israeli mtumishi wake,

akikumbuka huruma yake,

55kama alivyowaahidia wazee wetu,

Abrahamu na wazawa wake hata milele.”

56Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake.

Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji

57Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume.

58Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye.[#1:58 Yawezekana kwamba mpaka hapo majirani hawakujua kwamba Elisabeti alikuwa mjamzito (1:24).; #1:58 Sawa kama ilivyosemwa awali (1:14) kwamba “watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake”]

59Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakaria.[#1:59 Kwa watu wengi, hata wa kwetu, desturi ni kumpa mtoto jina la babu au mmoja wa babu zake. Jambo la kumpa mtoto jina la baba yake halikuwa jambo la kawaida katika mila na desturi za Wayahudi. Hapa lakini habari hii huenda imetolewa kumshirikisha Zakaria na hivyo kumfungulia ububu wake aweze kusema tena.; #1:59 Watoto wote wa kiume wa Wayahudi walitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa kama alama au ishara ya mkataba au agano kati ya Mungu na Waisraeli (Mwa 17:10-12; Lawi 12:3).]

60Lakini mama yake akasema, “Sivyo, bali ataitwa Yohane.”

61Wakamwambia, “Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?”

62Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani.

63Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: “Yohane ndilo jina lake.” Wote wakastaajabu.

64Papo hapo, midomo na ulimi wake Zakaria vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu.

65Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea.

66Wote waliosikia mambo hayo, waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: “Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.

Utenzi wa Zakaria

67Zakaria, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka unabii huu:[#1:67 Katika tafsiri nyingine “akatoa unabii”, lakini Kigiriki: neno linalotumiwa linamaanisha dhahiri kwamba aliyoyasema Zakaria, aliyasema kwa kuongozwa na Mungu, “akajazwa Roho Mtakatifu”); aliyatamka hayo kama msemaji wa Mungu, yaani nabii.]

68“Atukuzwe Bwana Mungu wa Israeli,

kwani amewajia na kuwakomboa watu wake.

69Ametupatia Mwokozi shujaa,[#1:69 Neno kwa neno: Katika A.K. pembe ni ishara au alama ya uwezo na nguvu kama katika Zab 18:2; 89:24.]

mzawa wa Daudi mtumishi wake.

70Aliahidi hapo kale

kwa njia ya manabii wake watakatifu,

71kwamba atatuokoa mikononi mwa maadui zetu

na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia.

72Alisema atawahurumia wazee wetu,

na kukumbuka agano lake takatifu.

73Alimwapia Abrahamu babu yetu,

kwamba atatujalia sisi

74tukombolewe mikononi mwa maadui zetu,

tupate kumtumikia bila hofu,

75tuwe wanyofu na waadilifu mbele yake,

siku zote za maisha yetu.

76Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu,

utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake;

77kuwatangazia watu kwamba wataokolewa

kwa kuondolewa dhambi zao.

78Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma.

Atatuchomozea mwanga kutoka juu,

79na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo,

aongoze hatua zetu katika njia ya amani.”

80Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionesha rasmi kwa watu wa Israeli.[#1:80 Luka 3:2-3; aya ya 80 inagusia muda upatao miaka 30 hivi tangu kuzaliwa kwake Yohane.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania