The chat will start when you send the first message.
1Kisha, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Haiwezekani kabisa kusitokee vikwazo vinavyosababisha dhambi; lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha.[#17:1 Tafsiri ya neno lenye maana ya , yaani mfano wa kitu chenye kuchochea mtu kutenda dhambi au kuacha imani.]
2Ingekuwa afadhali kwake kufungiwa shingoni jiwe kubwa la kusagia na kutoswa baharini, kuliko kumkwaza mmoja wa wadogo hawa.[#17:2 Yawezekana hapa kwamba anawataja hao watoto wadogo, au, kwa jumla, wanafunzi wake Yesu mwenyewe.]
3Jihadharini! Kama ndugu yako akikukosea, muonye; akitubu, msamehe.[#17:3 Kuhusu yaliyosemwa au yanayofuata. Au, kama katika tafsiri hii, onyo la jumla ambalo laambatana na aya ya 2.; #17:3 Yaani kwa upendo na sio kwa hasira au kwa kujiona mwema!]
4Na kama akikukosea mara saba kwa siku, na kila mara akarudi kwako akisema, ‘Nimetubu,’ lazima umsamehe.”[#17:4 Tarakimu ambayo hutumika kwa mfano kusema upeo wa kufanya kitu au kitendo, lakini hapa idadi isiyo na kikomo; tazama Mat 18:21-22.]
5Mitume wakamwambia Bwana, “Utuongezee imani.”
6Naye Bwana akajibu, “Kama imani yenu ingekuwa ndogo hata kama chembe ndogo ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu: ‘Ng'oka ukajipandikize baharini,’ nao ungewatii.[#17:6 Mbegu ya haradali ilifikiriwa kuwa mbegu ndogo kuliko zote. Na matumizi yake katika msemo yamekuwa kama kitendawili cha kuelezea kukua kwa kitu kutoka hali ndogo sana.]
7“Tuseme mmoja wenu ana mtumishi ambaye analima shambani au anachunga kondoo. Je, anaporudi kutoka shambani, atamwambia huyo mtumishi: ‘Haraka, njoo ule chakula?’
8La! Atamwambia: ‘Nitayarishie chakula, ujifunge tayari kunitumikia mpaka nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo nawe ule na kunywa.’
9Je, utamshukuru huyo mtumishi kwa sababu ametimiza aliyoamriwa?
10Hali kadhalika na nyinyi mkisha fanya yote mliyoamriwa, semeni: ‘Sisi ni watumishi tusio na faida, tumetimiza tu yale tuliyotakiwa kufanya.’”
11Yesu akiwa safarini kwenda Yerusalemu alipitia katika mipaka ya Samaria na Galilaya.[#17:11 Taz maelezo ya 9:51—19:27.]
12Alipokuwa anaingia katika kijiji kimoja, watu kumi wenye ukoma walikutana naye, wakasimama kwa mbali.[#17:12-14 Wenye ukoma, kwa vile walikuwa najisi kidini, (Lawi 13), iliwabidi kukaa mbali na kuepa kugusana na watu wengine. Kuponywa kwao kuliwarudishia hadhi yao na kuondolewa hali ya kuwa najisi. Taz Luka 5:12-13 maelezo.]
13Wakapaza sauti wakisema, “Yesu Mwalimu, tuonee huruma!”
14Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajioneshe kwa makuhani.” Basi, ikawa walipokuwa wanakwenda, wakatakasika.[#17:14 Taz Lawi 14:1-32.]
15Mmoja wao alipoona kwamba ameponywa, alirudi akimtukuza Mungu kwa sauti kubwa.
16Akajitupa chini mbele ya miguu ya Yesu huku akimshukuru. Huyo alikuwa Msamaria.
17Hapo Yesu akasema, “Je, si watu kumi walitakaswa? Wale tisa wako wapi?
18Hakupatikana mwingine aliyerudi kumtukuza Mungu ila tu huyu mgeni?”
19Halafu akamwambia huyo mtu, “Simama, uende zako; imani yako imekuponya.”
20Wakati mmoja, Mafarisayo walimwuliza Yesu, “Ufalme wa Mungu utakuja lini?” Naye akawajibu, “Ufalme wa Mungu hauji kwa namna itakayoweza kuonekana.[#17:20-21 Marko 13:21; , au: ; au: .]
21Wala hakuna atakayeweza kusema, ‘Uko hapa’, au ‘Uko pale’. Kwa kweli ufalme wa Mungu uko kati yenu.”
22Halafu akawaambia wanafunzi wake, “Siku zinakuja ambapo mtatamani kuona mojawapo ya siku za Mwana wa Mtu, lakini hamtaiona.[#17:22 Yaonekana kwamba inahusu siku zile ambapo Kristo atatokea pamoja na uwezo na utukufu wake.]
23Na watu watawaambieni: ‘Tazameni, yuko pale!’ au ‘Tazameni, yupo hapa!’ lakini nyinyi msitoke wala msiwafuate.
24Kwa maana kama vile umeme unavyotokea ghafla na kuangaza anga upande mmoja hadi mwingine, ndivyo Mwana wa Mtu atakavyokuwa siku ile yake.[#17:24 Baadhi ya hati nyingine zimeacha maneno hayo.]
25Lakini kabla ya hayo, itambidi ateseke sana na kukataliwa na kizazi hiki.
26Kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Mtu.[#17:26-27 Taz Mwa 6:5-12; 7:6-24. Historia ya Noa na Loti (aya 28-29) zilifikiriwa zote mbili kama matukio mahsusi ya kielelezo cha uokoaji wa waadilifu na kuadhibiwa kwa waovu.]
27Watu waliendelea kula na kunywa, kuoa na kuolewa mpaka wakati ule Noa alipoingia katika safina. Gharika ikatokea na kuwaangamiza wote.
28Itakuwa kama ilivyotokea wakati wa Loti. Watu waliendelea kula na kunywa, kununua na kuuza, kupanda mbegu na kujenga.
29Lakini siku ile Loti alipoondoka Sodoma, moto na madini ya kiberiti vikanyesha kama mvua kutoka mbinguni na kuwaangamiza wote.[#17:29 Kwa aya 28:29 taz Mwa 18:20—19:25. : namna ya madini ya rangi ya manjano ambayo huwaka na kutoa moto mkali wa harufu mbaya.]
30Ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Mtu atakapofunuliwa.
31“Siku hiyo, yeyote atakayekuwa juu ya paa asishuke kwenda nyumbani kuchukua mali yake. Kadhalika, naye atakayekuwa shambani asirudi nyuma.
32Kumbukeni yaliyompata mke wa Loti.[#17:32 Mwa 19:26. anatajwa hapa kuwahimiza watu wasirudi nyuma kuhusu maagizo ya Mungu (aya 31).]
33Yeyote anayetaka kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na yeyote anayeipoteza, ataiokoa.[#17:33 Mat 10:39; 16:25; Marko 8:35; Yoh 12:25; Luka ambaye alikwisha taja msemo huo katika mahala pengine palipotangulia (Luka 9:24) anauunganisha hapa na onyo la aya 31.]
34Nawaambieni, siku ile usiku watu wawili watakuwa wanalala pamoja, mmoja atachukuliwa na yule mwingine ataachwa.
35Wanawake wawili watakuwa wakisaga nafaka pamoja; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.”[#17:35 Hati nyingine zina ziada katika aya hii: , sehemu ambayo imetolewa kutoka Mat 24:40.; #17:35 Aya ya 36 haimo katika hati nyingi za mkono za kale (taz Mat 24:4).]
37Hapo wakamwuliza, “Ni wapi Bwana?” Naye akawaambia, “Palipo mzoga, ndipo tai watakapokusanyikia.”[#17:37 Ling na Yobu 39:30. Hapa, maneno haya yaonekana kuwa jibu lisilo moja kwa moja kwa swali la aya ya 20. Hukumu itafanyika popote itakapohitajika. Hamna sababu ya kuuliza “Itakuwa wapi?”]