The chat will start when you send the first message.
1Kauli ya Mwenyezi-Mungu iliyomjia Malaki awaambie Waisraeli.[#1:1 Jina hili lina maana ya mjumbe (rejea 3:1). Na kuhusu mianzo ya vitabu vya manabii taz Isa 1:1 maelezo.]
2Mwenyezi-Mungu asema: “Daima nimewapenda nyinyi”. Lakini watu wa Israeli wanauliza, “Umetupendaje?” Naye Mwenyezi-Mungu asema: “Je, Esau hakuwa ndugu yake Yakobo? Hata hivyo nilimpenda Yakobo
3nikamchukia Esau. Nimeiharibu nchi ya milima ya Esau ambayo ni urithi wake, nikawaachia mbwamwitu wa jangwani. Nao wazawa[#1:2-3 Esau ambaye anaitwa pia Edomu alikuwa babu wa Waedomu (Mwa 25:29-30) maadui wa jadi wa Waisraeli (rejea Mwa 25:22-26; 27; 32:4-21; Hes 20:14-21; Oba aya 10-14; Rom 9:11-13).]
4wa Esau, yaani Waedomu, wanasema kwamba ingawa miji yao imeharibiwa, watajenga upya magofu yake. Lakini, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema kwamba wanaweza kuijenga upya, lakini mimi nitaibomolea mbali. Watu watawaita, ‘Taifa ovu ambalo Mwenyezi-Mungu amelikasirikia milele.’
5Nanyi mtakapoyaona hayo kwa macho yenu, mtatambua na kusema: ‘Ukuu wa Mwenyezi-Mungu wafika hata nje ya mipaka ya nchi ya Israeli.’”[#1:2-5 Habari za ujumbe katika kitabu hiki zina muundo wa kimaandishi sanii unaofanana: nabii anatamka mada ya kujadili na watu nao wanajibu kwa mashaka na vipingamizi; kisha nabii anajibu pingamizi lililotolewa, akionesha kwamba ilikuwa sawa kile kilichosemwa kwanza. Yahusu muundo wa kimaandishi uliotumiwa katika majadiliano ya kisheria na mahakama. Taz utangulizi.]
6Mwenyezi-Mungu wa majeshi anawaambia hivi nyinyi makuhani mnaolidharau jina lake: “Mtoto humheshimu mzazi wake, na mtumishi humheshimu bwana wake. Ikiwa mimi ndiye Baba yenu, mbona mwanivunjia heshima? Ikiwa mimi ni bwana wenu, mbona hamniheshimu? Nanyi mnauliza, ‘Sisi tumekudharauje?’
7Mwanidharau kwa kunitolea madhabahuni pangu tambiko ya chakula najisi. Lakini nyinyi mnauliza, ‘Tumekitiaje najisi?’ Mnakitia najisi kwa kuidharau madhabahu yangu.
8Mnaponitolea tambiko ya mnyama kipofu, au kilema, au mgonjwa, je, huo si uovu? Je, mtawala atapendezwa au kukufanyia hisani ukimpa zawadi ya mnyama kama huyo?”[#1:8 Lawi 22:18-25; Kumb 15:21.]
9Kwa hiyo sasa enyi makuhani, mwombeni Mungu ili atuhurumie. Ikiwa mnamtolea matoleo ya aina hiyo, je, kweli atakuwa radhi nanyi?
10Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema, “Laiti angepatikana mtu mmoja miongoni mwenu ambaye angefunga milango ya hekalu ili msiwashe moto usiokubalika kwenye madhabahu yangu! Sipendezwi nanyi na sitaikubali tambiko yoyote mnayonitolea.[#1:10 Rejea Isa 1:11-13; Amo 5:21-24.]
11Watu wa mataifa kote duniani, toka mawio ya jua hadi machweo yake, wanalitukuza jina langu. Kila mahali wananifukizia ubani na kunitolea tambiko zinazokubalika; maana jina langu linatukuzwa miongoni mwao.[#1:11 Katika malumbano na makuhani, nabii anadhihirisha kwamba Mungu anazikataa ibada ambazo walizifanya hekaluni kule Yerusalemu. Yawezekana pia kwamba nabii kwa kufanya hivyo aligusia nyakati mpya za Masiha ambapo wageni wasio Waisraeli watashiriki ibada kwa Mwenyezi-Mungu (rejea Isa 56:6-7). Hapa anatangaza kurekebishwa kabisa kwa ibada kwa Mungu mahali pa sadaka zilizotolewa na makuhani (aya 7-10).]
12Lakini nyinyi mnalibeza jina langu pale mnapoichafua madhabahu yangu, na chakula mnachotoa juu yake mnakidharau.
13Mnasema, ‘Mambo haya yametuchosha mno,’ na mnanidharau. Mnaniletea tambiko za wanyama mliowapata kwa unyang'anyi, au walio vilema au wagonjwa. Je, nipokee tambiko hizo mikononi mwenu? Mimi Mwenyezi-Mungu nauliza.
14Na alaaniwe mtu yeyote anidanganyaye, ambaye huahidi kwa kiapo kunitolea tambiko mnyama safi kutoka katika kundi lake, lakini hunitolea tambiko mnyama mwenye kilema. Tazama, mimi ni mfalme mkuu, na watu wa mataifa yote hunicha.”