Mika 5

Mika 5

Kiongozi mpya kutoka Bethlehemu

1Mwenyezi-Mungu asema,

“Lakini wewe Bethlehemu katika Efratha,

wewe ni mdogo tu kati ya jamii za Yuda,

lakini kwako kutatoka mtawala

atakayetawala juu ya Israeli kwa niaba yangu.

Asili yake ni ya zama za kale.”

2Hivyo Mungu atawaacha watu wake kwa maadui,

mpaka yule mama mjamzito atakapojifungua.

Kisha ndugu zake waliobakia,

watarudi na kuungana na Waisraeli wenzao.

3Huyo mtawala atawachunga watu wake kwa nguvu ya Mwenyezi-Mungu,

kwa fahari yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wake.

Watu wake wataishi kwa usalama,

maana atakuwa mkuu mpaka miisho ya dunia.

4Yeye ndiye atakayeleta amani.[#5:4 Tafsiri yamkini ya makala ngumu. Rejea Zab 72:7; Isa 9:6; 11:6-9; Zek 9:10. Taz pia Efe 2:14 maelezo.]

Ukombozi na adhabu

Waashuru wakivamia nchi yetu,

na kuupenya ulinzi wetu,

tutapeleka walinzi wawakabili,

naam, tutawapeleka viongozi wetu kwa wingi.

5Kwa silaha zao wataitawala nchi ya Ashuru,

na kuimiliki nchi ya Nimrodi.

Watatuokoa mikononi mwa Waashuru,

watakapowasili mipakani mwa nchi yetu

na kuanza kuivamia nchi yetu.

6Wazawa wa Yakobo watakaobaki hai

wameenea miongoni mwa mataifa mengi,

watakuwa kama umande wa Mwenyezi-Mungu uburudishao,

kama manyunyu yaangukayo penye nyasi

ambayo hayasababishwi na mtu

wala kumtegemea binadamu.

7Wazawa wa Yakobo watakaobaki hai,

wameenea miongoni mwa mataifa na watu wengi

watakuwa na nguvu kubwa

kama simba kati ya wanyama wa porini,

kama mwanasimba miongoni mwa makundi ya kondoo,

ambaye kila mahali apitapo,

huyarukia na kuyararua mawindo yake,

asiwepo mtu yeyote wa kuyaokoa.

8Waisraeli watawashinda adui zao

na kuwaangamiza kabisa.

9Mwenyezi-Mungu asema,

“Wakati huo nitawaondoa farasi wenu,

na kuyaharibu magari yenu ya farasi.

10Nitaiharibu miji ya nchi yenu,

na kuzibomolea mbali ngome zenu.

11Nitatokomeza matendo yenu ya uchawi,

nanyi hamtakuwa tena na wapiga ramli.

12Nitaziharibu sanamu zenu,

na nguzo zenu za ibada;

nanyi mtakoma kuabudu vitu mlivyotengeneza wenyewe.

13Nitazing'oa sanamu za Ashera kutoka kwenu,[#5:13 Au: nguzo za Ashera, mungu wa kike wa watu wa Kanaani ambaye mfano wake ulikuwa nguzo au mti.]

na kuiangamiza miji yenu.

14Kwa hasira na ghadhabu yangu,

nitalipiza kisasi mataifa yote yasiyonitii.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania