Marko 3

Marko 3

Yesu anamponya mwenye mkono uliopooza

(Mat 12:9-14; Luka 6:6-11)

1Yesu aliingia tena katika sunagogi na mle ndani mlikuwa na mtu aliyekuwa na mkono uliopooza.

2Humo, baadhi ya watu walimngojea amponye mtu huyo siku ya Sabato ili wapate kumshtaki.[#3:2 Wayahudi walichukulia kitendo cha kumponya mtu siku ya Sabato kuwa ni kufanya kazi, jambo ambalo lilikatazwa kufanya siku ya Sabato.]

3Yesu akamwambia huyo mtu aliyekuwa na mkono uliopooza, “Njoo hapa katikati.”

4Kisha, akawauliza, “Je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao hawakusema neno.

5Hapo akawatazama wote kwa hasira, akaona huzuni kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Kisha akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako!” Naye akaunyosha mkono wake, ukawa mzima tena.

6Mara Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri pamoja na watu wa kikundi cha Herode jinsi ya kumwangamiza Yesu.[#3:6 Hao walikuwa Wayahudi waliomuunga mkono Herode Antipa na ukoo wa kifalme ulioanzishwa na Herode Mkuu (taz pia 12:13 na Mat 22:16 maelezo).]

Umati wa watu kando ya ziwa

7Yesu aliondoka hapo pamoja na wanafunzi wake, akaenda kando ya ziwa, na umati wa watu ukamfuata. Watu hao walikuwa wametoka Yerusalemu, Yudea,

8Idumea, ng'ambo ya mto Yordani, Tiro na Sidoni. Watu hao wengi walimwendea Yesu kwa sababu ya kusikia mambo mengi aliyokuwa ameyatenda.[#3:8 Eneo kusini mwa Yudea ambamo waliishi watu wasio Wayahudi (rejea “Edomu” katika Mwa 32:3). Eneo ng'ambo ya mto Yordani (vingine: “Perea”) lilikuwa kaskazini-mashariki mwa Yudea na kusini mwa Galilaya. Miji ya Sidoni na Turo imo kaskazini-magharibi mwa Galilaya.]

9Yesu akawaambia wanafunzi wake wamtayarishie mashua moja, ili umati wa watu usije ukamsonga.

10Alikuwa amewaponya watu wengi, na wagonjwa wote wakawa wanamsonga ili wapate kumgusa.

11Na watu waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu walipomwona, walijitupa chini mbele yake na kupaza sauti, “Wewe ni Mwana wa Mungu!”[#3:11 Ishara ya kusalimu amri; hao pepo (na si binadamu) walimtambua Yesu kuwa Mwana wa Mungu (taz pia 1:24; 5:7; Luka 4:41).]

12Lakini Yesu akawaamuru kwa ukali wasimjulishe kwa watu.[#3:12 Taz maelezo ya Marko 1:34.]

Yesu anawateua mitume kumi na wawili

(Mat 10:1-4; Luka 6:12-16)

13Yesu alipanda kilimani, akawaita wale aliowataka. Basi, wakamwendea,[#3:13 Ingawaje si dhahiri kwa nini Yesu anasemekana kupanda mlimani (au kilimani) wakati fulani fulani tunaweza kukumbushwa hapa kwamba katika A.K. (kwa mfano Kut 19:3-25; 1Fal 19:8) mlimani ni mahali ambapo Mungu anajidhihirisha kwa watu (taz pia Marko 9:2-13).]

14naye akawateua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume, wakae naye, awatume kuhubiri[#3:14 Labda idadi ya mfano wa makabila kumi na mawili ya Israeli.; #3:14 Baadhi ya hati za kale hazina maneno hayo.]

15na wawe na uwezo wa kuwafukuza pepo.

16Basi, hao kumi na wawili walioteuliwa ndio hawa: Simoni (ambaye Yesu alimpa jina, Petro),

17Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo (Yesu aliwapa hawa ndugu wawili jina Boanerge, maana yake “Wanangurumo”),[#3:17 Jina hili Boanerge laweza kuwa na maana ya “wakali” lakini si yamkini.]

18Andrea na Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Thoma, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkanaani na[#3:18 Kadiri ya mapokeo huyu ni sawa na Nathanaeli (Yoh 1:46).; #3:18 Taz Mat 10:3 maelezo.; #3:18 Jina ambalo limetokana na neno la Kiaramu lenye maana ya mzalendo na ambalo si sawa na jina linalotumiwa kuwataja wakazi wa nchi ya Kanaani. Taz pia Luka 6:15 ambapo anaitwa Zelote.]

19Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu.

Yesu na Beelzebuli

(Mat 12:22-32; Luka 11:14-23; 12:10)

20Kisha Yesu alikwenda nyumbani. Umati wa watu ukakusanyika tena, hata Yesu na wafuasi wake wasiweze kupata nafasi ya kula chakula.

21Basi, watu wa jamaa yake walipopata habari hiyo wakatoka kwenda kumchukua maana walikuwa wanasema kwamba ana wazimu.

22Nao waalimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu, wakasema, “Ana Beelzebuli! Tena, anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo.”[#3:22 Mat 12:24. Beelzebuli ni mkuu wa pepo wabaya na jina lenyewe lachukuliwa kutoka Kiebrania. Baal-zebubu (2Fal 1:2-3) ambapo ni neno linaloeleza jina Waebrania walilotumia kuitaja miungu ya Wakanaani (neno kwa neno: “bwana wa nzi”).]

23Hapo Yesu akawaita, akawaambia kwa mifano, “Shetani anawezaje kumfukuza Shetani?

24Ikiwa utawala mmoja umegawanyika makundimakundi yanayopingana, utawala huo hauwezi kudumu.

25Tena, ikiwa jamaa moja imegawanyika makundimakundi yanayopingana, jamaa hiyo itaangamia.

26Ikiwa basi, utawala wa Shetani umegawanyika vikundivikundi hauwezi kudumu, bali utaangamia kabisa.

27“Hakuna mtu awezaye kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang'anya mali yake, isipokuwa kwanza amemfunga huyo mtu mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kumnyang'anya mali yake.

28“Kweli nawaambieni, watu watasamehewa dhambi zao zote na kufuru zao zote;

29lakini anayesema mabaya dhidi ya Roho Mtakatifu, hatasamehewa kamwe; ana hatia ya dhambi ya milele.” (

30Yesu alisema hivyo kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”)[#3:30 Yaani waliufanya uwezo wa Yesu wa kupambana na kuwashinda pepo wabaya kuwa ni uwezo wa Shetani. Kwa hiyo katika aya ya 29 Yesu anasema juu ya “dhambi isiyosamehewa”. Taz pia 2Thes 1:8-9; Ebr 6:4-6; 10:26-29; 1Yoh 5:16-17.]

Mama na ndugu za Yesu

(Mat 12:46-50; Luka 8:19-21)

31Mama yake Yesu na ndugu zake walifika hapo, wakasimama nje, wakampelekea ujumbe kumwita.[#3:31 Kwa vile baba yake hatajwi hapa, wafafanuzi wa Biblia wanafikiri kwamba wakati huo Yosefu alikuwa amekwisha kufa.]

32Umati wa watu ulikuwa umekaa hapo kumzunguka. Basi, watu wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanataka kukuona.”

33Yesu akawaambia, “Mama yangu na ndugu zangu ni kina nani?”

34Hapo akawatazama watu waliokuwa wamemzunguka, akasema, “Tazameni! Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu.

35Mtu yeyote anayefanya anayotaka Mungu, huyo ndiye kaka yangu, dada yangu na mama yangu.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania