The chat will start when you send the first message.
1Mimi Paulo na Timotheo, watumishi wa Yesu Kristo, tunawaandikia nyinyi watu wa Mungu huko Filipi ambao mmeunganishwa na Kristo Yesu, pamoja na viongozi na wasaidizi wa kanisa.[#1:1 Taz Mate 16:1. Timotheo alimsindikiza Paulo na Sila wakati kanisa la Filipi lilipoanzishwa na alikuwa pamoja na Paulo wakati alipoandika barua hii. Tunaambiwa kuwa Paulo alikuwa na mpango wa kumtuma kule Filipi baadaye (Fil 2:19-23).; #1:1 Mji wa Makedonia, upande wa kaskazini mwa Ugiriki, ambamo kulianzishwa kanisa la kwanza katika Europa, rejea Mate 16:12.; #1:1 Kigiriki ni “episkopoi” neno ambalo mara nyingine laandikwa katika Kiswahili kama “maaskofu”. Hapa yahusu watu ambao wanasimamia kanisa kidini na kiutawala. Hawa viongozi wanatajwa pia pamoja na kundi lingine ambalo katika tafsiri hii wanaitwa “wasaidizi”, neno ambalo ni tafsiri ya neno la Kigiriki “diakonoi”.; #1:1-2 Kuhusu muundo wa barua za kale taz Rom 1:1-7 maelezo, na pia Utangulizi kwa Barua za A.J.]
2Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.
3Namshukuru Mungu wangu kila ninapowakumbukeni;
4na kila ninapowaombeeni nyote, nasali kwa furaha,[#1:4 Neno hili ni wazo muhimu katika barua hii (taz Fil 1:18 maelezo).]
5kwa sababu ya jinsi mlivyonisaidia katika kazi ya Injili tangu siku ile ya kwanza mpaka leo.
6Basi, nina hakika kwamba Mungu aliyeanza kazi hii njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka ikamilike katika siku ile ya Kristo Yesu.[#1:6 Rejea 1Kor 1:8.]
7Hivyo ndivyo ninavyopaswa kuwafikirieni, kwani nawakumbukeni daima moyoni mwangu. Kwa maana nyinyi nyote mmeshiriki katika fadhili aliyonijalia Mungu ya kutetea na kuithibitisha Injili, sasa niwapo kifungoni na pia pale awali nilipokuwa huru.[#1:7 Paulo aliandika barua hii akiwa kifungoni mahali fulani kwenye mwambao wa mashariki wa Bahari ya Mediteranea au labda kule Roma ambapo alikuwa amewekwa katika kifungo baridi (Mate 28:16,30-31).]
8Mungu anajua kuwa ninasema ukweli ninaposisitiza kwamba, kwa upendo uleule wa Yesu Kristo, natamani sana kuwaoneni.
9Sala yangu ni hii: naomba upendo wenu uzidi kuongezeka zaidi na zaidi pamoja na ujuzi wa kweli na busara ya kila namna,
10ili muweze kuchagua jambo lililo bora. Hapo ndipo mtakuwa safi na bila lawama yoyote ile katika siku ile ya Kristo.
11Maisha yenu yatajazwa mambo yote yaliyo kweli bora, ambayo Yesu Kristo mwenyewe anaweza kuwajalieni, kwa ajili ya utukufu na sifa ya Mungu.
12Ndugu zangu, napenda mfahamu kwamba mambo yote yaliyonipata yamesaidia sana kuieneza Injili.
13Kutokana na hayo, walinzi wote wa ikulu pamoja na wengine wote hapa wanafahamu kwamba niko kifungoni kwa sababu mimi namtumikia Kristo.[#1:13 Rejea Mate 28:30-31. “Ikulu” hapa ilikuwa makao makuu ya mtawala wa Kiroma hapo pamoja na maofisa wake. Huenda Paulo aliwashirikisha hao walinzi wa ikulu habari juu ya Yesu ambayo ndiyo iliyosababishwa kufungwa kwake.]
14Na huku kuweko kwangu kifungoni kumewafanya ndugu wengi kuwa na imani kwa Bwana, hata wanazidi kuwa hodari katika kuutangaza ujumbe wa Mungu bila hofu.
15Kweli, baadhi yao wanamhubiri Kristo kwa sababu wana wivu na ni watu wagomvi; lakini wengine wanamhubiri Kristo kwa nia nzuri.[#1:15-18 Katika aya hizi Paulo anasema juu ya watu ambao walikuwa wanahubiri Habari Njema ya Yesu lakini si kwa nia njema. Ingawa si sawa, Paulo anafurahi kwamba angalau wanahubiri juu ya Yesu, ingawaje kwa faida zao wenyewe.]
16Hawa wanafanya hivyo kwa upendo, kwani wanajua kwamba Mungu amenipa jukumu hili la kuitetea Injili.
17Hao wengine wanamtangaza Kristo kwa mashindano na si kwa moyo mnyofu, wakidhani kwamba wataniongezea mateso yangu kifungoni.
18Haidhuru! Mimi nafurahi ikiwa tu watu wanamhubiri Kristo kwa kila njia, iwe ni kwa nia nzuri au kwa nia mbaya. Tena nitaendelea kufurahi,
19kwani najua kwamba kwa sala zenu na kwa msaada wa Roho wa Yesu Kristo, nitakombolewa.[#1:19 Maneno ambayo yanakumbusha Yobu 13:16 (LXX). Paulo anamtaja Roho Mtakatifu mara kwa mara katika barua hii; hapa “Roho wa Yesu Kristo” ambaye anamsaidia Paulo; Roho ambaye analeta umoja kati ya waumini (2:1), na ambaye huwaongoza wafuasi wa Kristo katika ibada (3:3).]
20Hamu yangu kubwa na tumaini langu ni kwamba kwa vyovyote sitashindwa katika kutimiza wajibu wangu, bali nitakuwa na moyo thabiti kila wakati na hasa wakati huu, ili kwa maisha yangu yote, niwapo hai au nikifa, nimpatie Kristo heshima.
21Kwangu, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida zaidi.
22Lakini, kama kwa kuishi nitaweza kufanya kazi yenye faida zaidi, basi, sijui nichague lipi!
23Nakabiliwa na haya mawili yaliyo sawa. Natamani kuyaacha maisha haya nikakae pamoja na Kristo, jambo ambalo ni bora zaidi;
24lakini ni jambo la maana zaidi kwenu kama nikiendelea kuishi.
25Nina hakika ya jambo hili, na hivyo najua kwamba nitaendelea kuishi pamoja nanyi nyote, ili nipate kuongeza maendeleo yenu na furaha katika imani.[#1:25-26 Hatujui kama tumaini la Paulo la kufunguliwa gerezani na kwenda kuwasaidia Wafilipi lilifanikiwa au la.]
26Basi, nitakapokuwa nanyi tena mtakuwa na sababu ya kuona fahari juu yangu katika kuungana na Kristo Yesu.
27Basi, jambo muhimu ni kwamba mwenendo wenu uambatane na matakwa ya Injili ya Kristo, ili kama nikiweza kuja kwenu au nisipoweza, nipate walau kusikia kwamba mnasimama imara mkiwa na lengo moja, na kwamba mnapigana vita kwa pamoja na mnayo nia moja kwa ajili ya imani ya Injili.
28Msiwaogope maadui zenu, bali muwe hodari daima, na hiyo itawathibitishia kwamba wao watashindwa, nanyi mtashinda kwani Mungu mwenyewe ndiye anayewapeni ushindi.
29Maana nyinyi mmepewa fadhili ya kumtumikia Kristo si tu kwa kumwamini bali pia kwa kuteswa kwa ajili yake.
30Sasa mwaweza kushirikiana nami katika kupigana vita. Vita hivi ni vile mlivyoona nikipigana pale awali na ambavyo bado napigana sasa kama mnavyosikia.[#1:30 Vita vya Paulo hapa labda yahusu hali yake kifungoni akiwa anangojea hukumu yake. Rejea Mate 16:19-40; 1Thes 2:2.]