The chat will start when you send the first message.
1Maneno ya mfalme Lemueli. Mawaidha aliyofundishwa na mama yake:[#31:1 Tafsiri nyingine yamkini: “mfalme Lemueli wa Masa”, taz 30:1 “Mawaidha”. Maandishi au mawaidha ya kuwafundisha wafalme vijana jinsi ya kuishi yalikuwa kawaida katika tamaduni za Misri ya kale na Mesopotamia. Hapa mawaidha hayo yanatoka kwa mama.]
2Nikuambie nini mwanangu?
Nikuambie nini mwanangu niliyekuzaa?
Nikuambie nini wewe niliyekuomba kwa Mungu?
3Usimalize nguvu zako kwa wanawake,[#31:3 Kuhusu matatizo na athari za umalaya taz 5:1-23; 7:6-27. Wanawake wa namna hiyo wanaweza kumpotosha mfalme kwa namna mbalimbali.]
usiwape mali yako hao wanaoangamiza wafalme.
4Haifai ee Lemueli, haifai wafalme kunywa divai,[#31:4-7 Pombe inasababisha watawala kusahau majukumu yao, wasiweze kutekeleza haki za jamii hasa wanyonge (Mhub 10:16,17; Isa 5:21-24; 28:7-13). Katika aya 6-7 pombe inaruhusiwa kwa ajili ya kuwapunguzia maumivu walio katika hali mahututi, lakini mwandishi hasemi kamwe kwamba hilo lichukuliwe kama kisingizio cha kuingia katika hali hiyo.]
wala wakuu kutamani vileo.
5Wakinywa watasahau maagizo ya sheria,
na kuwanyima haki wenye taabu.
6Mpe kileo mtu anayekufa,
wape divai wale wenye huzuni tele;
7wanywe na kusahau umaskini wao,
wasikumbuke tena taabu yao.
8Lakini wewe, lazima useme kwa ajili ya wote walio bubu;
na kutetea haki za wote wasiojiweza.
9Sema kwa ajili yao na kuamua kwa haki,
linda haki za maskini na fukara.
10Mke mwema kweli, apatikana wapi?[#31:10 Katika Kiebrania aya 10 mpaka 31 ni utenzi ambao umeundwa kwa kufuatia alfabeti za Kiebrania. Taz Zab 119 (utangulizi) maelezo. Kwa mtindo huo wa pekee wa utenzi mwandishi anafanikiwa kutoa orodha ndefu ya sifa za mke aliye kweli mwema. Mke huyo mwema anafanana na yule mwanamke “Hekima” ambaye anatajwa katika 1:20-33; 8:1—9:12.]
Huyo ana thamani kuliko johari!
11Mumewe humwamini kwa moyo,
kwake atapata faida daima.
12Kamwe hamtendei mumewe mabaya,
bali humtendea mema maisha yake yote.
13Hutafuta sufu na kitani,
na kufanya kazi kwa mikono yake kwa bidii.
14Yeye ni kama meli za biashara:
huleta chakula chake kutoka mbali.
15Huamka kabla ya mapambazuko,
akaitayarishia jamaa yake chakula,
na kuwagawia kazi watumishi wake.
16Hufikiria kununua shamba, kisha hulinunua,
na kulima zabibu kwa faida ya jasho lake.
17Huwa tayari kufanya kazi kwa nguvu
na kuiimarisha mikono yake.
18Hutambua kwamba shughuli zake zina faida;
hufanya kazi hata usiku kwa mwanga wa taa yake.
19Husokota nyuzi kwa mikono yake mwenyewe,
kwa vidole vyake mwenyewe husuka nguo zake.
20Huufungua mkono wake kuwapa maskini,
hunyosha mkono kuwasaidia fukara.
21Hawahofii watu wake ijapo baridi ya kipupwe,
maana kila mmoja anazo nguo za kutosha.
22Hujitengenezea matandiko,
mavazi yake ni ya zambarau ya kitani safi.
23Mume wake ni mtu mashuhuri barazani,[#31:23 Sifa za mumewe zinakwenda sambamba na sifa za mkewe katika 31:31.]
anakoshiriki vikao vya wazee wa nchi.
24Mwanamke huyo hutengeneza nguo na kuziuza,
huwauzia wafanyabiashara mishipi.
25Nguvu na heshima ndizo sifa zake,
hucheka afikiriapo wakati ujao.
26Hufungua kinywa kunena kwa hekima,
huwashauri wengine kwa wema.
27Huchunguza yote yanayofanyika nyumbani mwake,
kamwe hakai bure hata kidogo.
28Watoto wake huamka na kumshukuru,
mumewe huimba sifa zake.
29Husema, “Wanawake wengi wametenda mambo ya ajabu,
lakini wewe umewashinda wote.”
30Madaha huhadaa na uzuri haufai,
bali mwanamke amchaye Mwenyezi-Mungu atasifiwa.
31Jasho lake lastahili kulipwa,
shughuli zake hazina budi kuheshimiwa popote.