The chat will start when you send the first message.
1Heri mtu asiyefuata shauri la waovu,[#1:1 Tamko ambalo kawaida lamtaja mtu aliyebahatika kwa jambo jema. Tazama Zab 2:12d; 127:5; 128:1; 144:15; 146:5 (rejea pia Mit 14:21; 16:20; 28:14; 29:18 na Mat 5:3-11): Mara nyingi zaidi msemo au tamko hilo linatumiwa zaidi katika maandishi ya hekima. “Heri” inayohusika hapa ni ile ya mtu ambaye anaishi kwa kufuata matakwa ya Mungu. Kwa maneno mengine mtu huyo amebarikiwa na Mungu.]
asiyeshiriki njia za wenye dhambi,
wala kujumuika na wenye dharau;
2bali huifurahia sheria ya Mwenyezi-Mungu,[#1:2 Neno linalotafsiriwa hapa katika Kiebrania ni “tora”; neno ambalo lina mapana yake kimaana: mwongozo, funzo, au agizo la Mungu la kumwongoza binadamu katika mema (rejea Zab 19:7-14; 119).]
na kuitafakari mchana na usiku.
3Huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito,
unaozaa matunda kwa wakati wake,
na majani yake hayanyauki.
Kila afanyalo hufanikiwa.
4Lakini waovu sivyo walivyo;
wao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
5Kwa hiyo watu waovu wataanguka wakati wa hukumu,[#1:5 Mara nyingi katika Biblia inatajwa kuwa Mungu ndiye hakimu, kwa hiyo wakati Mungu atakapowahukumu watu (taz pia Isa 24:1-2; Amo 5:18-20; Sef 2:1-2; Ling Mat 24:36-44; Marko 13:32-37; Luka 17:26-30,34-36).]
wenye dhambi hawatakaa na kusanyiko la waadilifu.
6Maana Mwenyezi-Mungu huziongoza njia za waadilifu;[#1:6 Tafsiri nyingine yamkini: “Mwenyezi-Mungu anazijua njia za waadilifu”, kwa maana ya kwamba anazikubali na hivyo kuziongoza. Neno “kujua” linapotumika katika Biblia kama hapa kwa Mungu huchukua maana yake kulingana na mazingira ya maandishi na sio daima kujua kimaarifa. Na kuhusu matumizi ya “Mwenyezi-Mungu” rejea Mwa 2:4 maelezo.]
lakini njia za waovu zitaishia katika maangamizi.