Zaburi 10

Zaburi 10

Sala dhidi ya udhalimu

1Ee Mwenyezi-Mungu, mbona wasimama mbali?

Kwa nini wajificha wakati tumo taabuni?

2Kwa kiburi waovu wanawatesa maskini;

njama zao ziwanase wao wenyewe.

3Mwovu hujisifia tamaa zake mbaya,

mtu wa tamaa hulaani na kumkataa Mwenyezi-Mungu.

4Katika majivuno yake husema: “Mungu hatagundua.”

Mawazo yake yote ni: “Hakuna Mungu.”

5Njia za mwovu hufanikiwa daima;

kwake hukumu zako ziko mbali na mawazo yake,

na huwadharau maadui zake wote.

6Huwaza moyoni: “Sitakuwa na wasiwasi;

sitapatwa na dhiki maishani.”

7Kinywa chake kimejaa laana, udanganyifu na dhuluma;

mwepesi kusema maneno ya kuchukiza na maovu.

8Hujificha vijijini huku anaotea,

amuue kwa siri mtu asiye na hatia.

Yuko macho kumvizia mnyonge;

9huotea mafichoni mwake kama simba.

Huvizia apate kuwakamata maskini;

huwanasa kwa mtego wake na kuwachukua.

10Mnyonge huvamiwa na kuangushwa chini;

huangushwa kwa ukatili wa mtu mwovu.

11Mwovu huwaza moyoni mwake: “Mungu amesahau;

ameficha uso wake, haoni kitu!”

12Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwaadhibu;

usiwasahau wanaodhulumiwa.

13Ee Mungu, kwa nini mwovu anakudharau,

na kusema ati hutamfanya awajibike?

14Lakini wewe wawaona wenye dhiki na shida;

nawe daima uko tayari kuwasaidia.

Mnyonge anakutegemea wewe, ee Mungu,

wewe umekuwa daima msaada wa yatima.

15Uzivunje nguvu za mtu mwovu;

ukomeshe uovu wake wote, usiwepo tena.

16Mwenyezi-Mungu ni mfalme milele na milele!

Mataifa yasiyomjua yatatoweka nchini mwake.

17Ee Mwenyezi-Mungu, wapokea dua za mnyonge;

wampa moyo na kumtegea sikio.

18Utawatendea haki yatima na wanaodhulumiwa,

binadamu aliye udongo asiweze tena kuleta hofu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania