The chat will start when you send the first message.
1Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa ni mwema,
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
2Watu wa Israeli na waseme:
“Fadhili zake zadumu milele.”
3Wazawa wa Aroni na waseme:
“Fadhili zake zadumu milele.”
4Wote wamchao Mwenyezi-Mungu na waseme:[#118:2-4 Vikundi vitatu vinatajwa kana kwamba vinajumuisha jamii yote. Kuhusu wazawa wa Aroni taz 115:10; na 99:6 maelezo.]
“Fadhili zake zadumu milele.”
5Katika taabu yangu nilimwomba Mwenyezi-Mungu,
naye akanisikia na kuniweka huru.
6Mwenyezi-Mungu yuko nami, siogopi kitu;
binadamu ataweza kunifanya nini?
7Mwenyezi-Mungu yuko nami, kunisaidia;
nami nitawaona maadui zangu wameshindwa.
8Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu,
kuliko kumtumainia mwanadamu.
9Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu,
kuliko kuwatumainia viongozi wa dunia.
10Mataifa yote yalinizingira,
lakini kwa jina la Mwenyezi-Mungu nikayaangamiza!
11Yalinizunguka kila upande,
lakini kwa jina la Mwenyezi-Mungu, nikayaangamiza!
12Yalinizunguka, mengi kama nyuki,
lakini yakateketea kama kichaka motoni;
kwa jina la Mwenyezi-Mungu niliyaangamiza!
13Nilishambuliwa mno karibu nishindwe,
lakini Mwenyezi-Mungu alinisaidia.
14Mwenyezi-Mungu ni nguvu yangu kuu;
yeye mwenyewe ndiye wokovu wangu.
15Sauti za furaha ya ushindi zasikika hemani mwao waadilifu:[#118:15 Yaani mahema ya vita au labda mahema ya muda ambamo watu walikusanyika wakati wa ibada. Wengine wanafikiri matumizi yake hapa ni ya jumla kwa maana ya makazi ya watu.]
“Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu!
16Mkono wa nguvu wa Mwenyezi-Mungu umeleta ushindi!
Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu!”
17Sitakufa, bali nitaishi,
na kusimulia matendo ya Mwenyezi-Mungu.
18Mwenyezi-Mungu ameniadhibu sana,
lakini hakuniacha nife.
19Nifungulie milango ya watu waadilifu,
niingie na kumshukuru Mwenyezi-Mungu!
20Huu ndio mlango wa Mwenyezi-Mungu,
watu waadilifu watapitia humo.
21Nakushukuru, ee Mungu kwa kunijibu;
kwa sababu wewe ni wokovu wangu.
22Jiwe walilokataa waashi,
limekuwa jiwe kuu la msingi.
23Hiyo ni kazi yake Mwenyezi-Mungu
nayo ni ya ajabu sana kwetu.
24Hii ndiyo siku aliyoifanya Mwenyezi-Mungu;
tushangilie na kufurahi.
25Tafadhali utuokoe, ee Mwenyezi-Mungu!
Tafadhali utufanikishe, ee Mwenyezi-Mungu!
26Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mwenyezi-Mungu!
Twawabariki kutoka nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu
27Mwenyezi-Mungu ni Mungu;
yeye ametujalia mwanga wake
Shikeni matawi ya sherehe,
mkiandamana mpaka madhabahuni.
28Wewe ni Mungu wangu, nami ninakushukuru;
ninakutukuza, ee Mungu wangu.
29Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema,
kwa maana fadhili zake zadumu milele.