Zaburi 127

Zaburi 127

Bila Mungu kazi ya binadamu haifai

1Mwenyezi-Mungu asipoijenga nyumba,[#127:1 Kujenga nyumba kunaweza kuwa na maana ya nyumba ya kweli ya kuishi humo, au kunaweza kuwa na maana ya kuanzisha familia kama inavyosemwa katika aya 3 na 4.]

waijengao wanajisumbua bure.

Mwenyezi-Mungu asipoulinda mji,

waulindao wanakesha bure.

2Mnajisumbua bure kuamka mapema asubuhi

na kuchelewa kwenda kupumzika jioni,

mjipatie chakula kwa jasho lenu.

Mungu huwaruzuku walio wake hata walalapo.

3Watoto ni riziki kutoka kwa Mwenyezi-Mungu;[#127:3-5 Zamani, hasa katika Mashariki ya Kati ya Kale kuwa na watoto wengi ilikuwa ni baraka. Na watoto wengi (hapa ni watoto wa kiume) ilifikiriwa kwamba wazazi wangekuwa na misaada mingi na kutunzwa nyakati za uzeeni. Shughuli zote za maisha ya siku kwa siku: kazi, familia, mali n.k., zilikuwa na maana kwa vile zilihusiana na Mungu.]

watoto ni tuzo lake kwetu sisi.

4Watoto waliozaliwa wazazi wakiwa bado vijana,

ni kama mishale mikononi mwa askari.

5Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.

Hatashindwa atakapokabiliana na adui mahakamani.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania