Zaburi 130

Zaburi 130

Kuomba msaada

1Toka upeo wa unyonge wangu,

nakulilia, ee Mwenyezi-Mungu.

2Ee Bwana, sikia sauti yangu,

uitegee sikio sauti ya ombi langu.

3Kama, ee Mwenyezi-Mungu ungekumbuka maovu yetu[#130:3 Mwanazaburi anakiri na kuungama kwamba binadamu ni mwenye dhambi na ni kwa wema wa Mungu peke yake binadamu anaweza kusalimika.]

nani, ee Bwana, angeweza kusalimika?

4Lakini kwako twapata msamaha,

ili sisi tukuheshimu.

5Namtumainia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wangu wote;

nina imani sana na neno lake.

6Ninamtumainia Mwenyezi-Mungu

kuliko walinzi wanavyongojea pambazuko;

kuliko walinzi wanavyongojea kuche asubuhi.

7Ee Israeli, umtumainie Mwenyezi-Mungu,

maana kwake Mwenyezi-Mungu kuna fadhili,

kwake kuna nguvu kubwa ya kutukomboa.

8Yeye atawakomboa watu wa Israeli

kutoka katika maovu yao yote.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania