The chat will start when you send the first message.
1Usikie sala yangu, ee Mwenyezi-Mungu!
Ulitegee sikio ombi langu
maana wewe ni mwaminifu;
unijibu kwa sababu ya uadilifu wako.
2Usinitie hukumuni mimi mtumishi wako,
maana hakuna yeyote aliye mwadilifu mbele yako.
3Maadui zangu wamenifuatia;
wameniangusha chini kabisa
wameniketisha gizani kama mtu aliyekufa zamani.
4Nimevunjika moyo kabisa;
nimekufa ganzi kwa ajili ya woga.
5Nakumbuka siku zilizopita;
natafakari juu ya yote uliyotenda,
nawaza na kuwazua juu ya matendo yako.
6Nakunyoshea mikono yangu kuomba;
nina kiu yako kama nchi kavu isiyo na maji.
7Ee Mwenyezi-Mungu, unijibu haraka;
maana nimekata tamaa kabisa!
Usijifiche mbali nami,
nisije nikawa kama wale washukao kwa wafu.
8Asubuhi unioneshe fadhili zako,[#143:8 Wakati wa matumaini mapya baada ya usiku wa giza la kukata tamaa.]
maana nimekuwekea tumaini langu.
Unifundishe mwenendo wa kufuata,
maana nakuelekezea ombi la moyo wangu.
9Uniokoe, ee Mwenyezi-Mungu, kutoka maadui zangu,
maana kwako nakimbilia usalama.
10Unifundishe kutimiza matakwa yako,
maana wewe ni Mungu wangu!
Roho yako nzuri iniongoze katika njia sawa.
11Unifadhili, ee Mwenyezi-Mungu, kwa hisani yako,
uniondoe katika taabu kwa sababu ya uadilifu wako.
12Kwa sababu ya fadhili zako uwakomeshe maadui zangu,
uwaangamize wote wanaonidhulumu;
maana mimi ni mtumishi wako.