The chat will start when you send the first message.
1Msifuni Mwenyezi-Mungu![#146:1 Zaburi zote 146-150 huanza na kumalizia kwa mwito huo.]
Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu!
2Nitamsifu Mwenyezi-Mungu maisha yangu yote;
nitamwimbia Mungu wangu muda wote niishipo.
3Msiwategemee wakuu wa dunia;[#146:3 Tamko hili ni ujumbe mahsusi kabisa ambao ulitiliwa maanani na Wanazaburi (Zab 118:8-9) na manabii (Isa 2:22; 31:3; Yer 17:5). Lengo lake ni kwamba binadamu lazima aweke tegemeo lake kwa Mungu na sio kwa binadamu, mali, miungu n.k.]
hao ni binadamu tu, hawawezi kuokoa.
4Binadamu akitoa pumzi yake ya mwisho,
anarudi mavumbini alimotoka;
na hapo mipango yake yote hutoweka.
5Heri mtu anayesaidiwa na Mungu wa Yakobo,
mtu aliyeweka tumaini lake kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake,
6aliyeumba mbingu na dunia,
bahari na vyote vilivyomo.
Yeye hushika ahadi yake milele.
7Yeye huwapatia wanaoonewa haki zao,
huwapa wenye njaa chakula.
Mwenyezi-Mungu huwapa wafungwa uhuru,
8huwafungua macho vipofu.
Mwenyezi-Mungu huwainua waliokandamizwa;
huwapenda watu walio waadilifu.
9Mwenyezi-Mungu huwalinda wageni,
huwategemeza wajane na yatima;
lakini huipotosha njia ya waovu.
10Mwenyezi-Mungu atawala milele,
Mungu wako, ee Siyoni, ni mfalme vizazi vyote!
Msifuni Mwenyezi-Mungu!