The chat will start when you send the first message.
1Enyi watawala, je, mwahukumu kwa haki kweli?
Je, mnawahukumu watu kwa adili?
2La! Nyinyi mwafikiria tu kutenda maovu;
nyinyi wenyewe mwaeneza dhuluma nchini.
3Waovu wamepotoka tangu kuzaliwa kwao,
waongo hao, wamekosa tangu walipozaliwa.
4Wana sumu kama sumu ya nyoka;[#58:4-5 Huyu Mwanazaburi anafananisha watawala wabaya na nyoka. “Viziwi”, yaani hawawezi kusikia maonyo. Picha inayotolewa katika aya 4b-5 si rahisi kuielewa na wengi hutoa tafsiri tofauti tofauti. Lakini maana ya kawaida ni kwamba watawala hao ni wakaidi, hukataa kusikiliza mashauri mema.]
viziwi kama joka lizibalo masikio,
5ambalo halisikii hata sauti ya mlozi,
au utenzi wa mganga stadi wa uchawi.
6Ee Mungu, wavunje meno yao,
yang'oe, ee Mwenyezi-Mungu, meno ya simba hao.
7Watoweke kama maji yanayodidimia mchangani,
kama nyasi wakanyagwe na kunyauka,
8watoweke kama konokono ayeyukavyo,[#58:8 Ilifikiriwa kwamba konokono anapoacha ute wa mwili wake nyuma anapojikokota, alikuwa anayeyuka na mwishowe ataishia kabisa. Ndivyo watakavyoishia hao watu wabaya.]
kama mimba iliyoharibika isiyoona kamwe jua!
9Kabla hawajatambua, wang'olewe
kama miiba, michongoma au magugu.
Kwa hasira ya Mungu, wapeperushwe mbali,
wakiwa bado hai.
10Waadilifu watafurahi waonapo waovu wanaadhibiwa;
watatembea katika damu ya watu wabaya.
11Watu wote watasema: “Naam, waadilifu hupata tuzo!
Hakika yuko Mungu anayeihukumu dunia!”