The chat will start when you send the first message.
1Ee Mwenyezi-Mungu, usinikemee kwa hasira yako;[#6:1 Neno la Kiebrania linalotafsiriwa hapa ni zito zaidi; linajumuisha pia maana ya “kupatiliza”.]
usiniadhibu kwa ghadhabu yako.
2Unihurumie, ee Mwenyezi-Mungu, nimeishiwa nguvu;
uniponye, ee Mwenyezi-Mungu, nataabika mpaka mifupani.
3Ninahangaika sana rohoni mwangu.
Ee Mwenyezi-Mungu, utakawia mpaka lini?
4Unigeukie, ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe;
unisalimishe kwa sababu ya fadhili zako.
5Huko kwa wafu hakuna anayekukumbuka;[#6:5 Yaani kuzimu. Ilifikiriwa kwamba kifo kilimweka mtu mbali na Mungu hata asiweze tena kumwabudu na kumsifu (taz Yobu 10:21-22; Isa 38:18). “Hakuna anayekukumbuka”, yaani kumsifu na kumwomba. Kumkumbuka Mwenyezi-Mungu ni kusimulia mambo aliyowatendea watu wake.]
huko kuzimu ni nani awezaye kukusifu?
6Niko hoi kwa kilio cha uchungu;
kila usiku nalowesha kitanda changu kwa machozi;
kwa kulia kwangu naulowesha mto wangu.
7Macho yangu yamechoka kwa huzuni;
yamefifia kwa kutaabishwa na adui.
8Ondokeni kwangu enyi nyote watenda maovu!
Maana Mwenyezi-Mungu amesikia kilio changu.
9Mwenyezi-Mungu amesikia ombi langu;
Mwenyezi-Mungu amekubali sala yangu.
10Maadui zangu wote wataaibika na kufadhaika;[#6:10 Kitenzi “wataaibika” ni tukio linalofuata adhabu ya Mungu na kushindwa kwa hao maadui.]
watarudi nyuma na kuaibishwa ghafla.