Zaburi 69

Zaburi 69

Maombolezo

1Uniokoe, ee Mungu;

maji yamenifika shingoni.

2Ninazama ndani ya matope makuu,

hamna hata mahali pa kuweka miguu.

Nimetumbukia kwenye kilindi cha maji,

nachukuliwa na mawimbi.

3Niko hoi kwa kupiga yowe,[#69:3 Hali ya namna hiyo hiyo inatajwa katika 6:6-7.]

na koo langu limekauka.

Macho yangu yamefifia,

nikikungojea ewe Mungu wangu.

4Watu wengi kuliko nywele zangu ndio wanichukiao bure.[#69:4 Zab 35:19; Yoh 15:25.]

Wana nguvu sana hao wanaotaka kuniua,

hao wanaonishambulia kwa mambo ya uongo.

Je, nirudishe kitu ambacho sikuiba?

5Ee Mungu, waujua upumbavu wangu;

makosa yangu hayakufichika kwako.

6Wanaokutumainia wasiaibishwe kwa sababu yangu,

ee Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi;

wanaokutafuta, wasione fedheha kwa sababu yangu

ee Mungu wa Israeli.

7Kwa ajili yako nimefedheheshwa,[#69:7 Huyu Mwanazaburi haoni kwamba mateso yake yamesababishwa na dhambi zake, ila anateseka kwa ajili ya Mungu. Hali hii inaonesha kwa nini katika A.J. Zaburi hii imechukuliwa kuelezea mateso ya Yesu Kristo ambaye alipatwa na hali ya mateso ya namna hii. Taz pia 22:1.]

aibu imefunika uso wangu.

8Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,

kaka na dada zangu hawanitambui.

9Upendo wangu kwa nyumba yako unanimaliza.

Kashfa zote wanazokutolea wewe zimenipata mimi.

10Nilipojinyenyekesha kwa kufunga,

watu walinilaumu.

11Nilipovaa vazi la gunia kuomboleza,

wao walinidharau.

12Watu wananisengenya mabarabarani;

walevi wanatunga nyimbo juu yangu.

13Lakini mimi nakuomba wewe, ee Mwenyezi-Mungu;

nikubalie ombi langu wakati unaopenda, ee Mungu.

Kwa wingi wa fadhili zako unijibu.

Wewe ni mkombozi wa kuaminika.

14Kwa msaada wako amini uniokoe

nisizame katika matope;

uniokoe na hao wanaonichukia,

unisalimishe kutoka vilindi vya maji.

15Usiniache nikumbwe na mkondo wa maji,

au nizame kwenye kilindi

au nimezwe na kifo.

16Unijibu, ee Mwenyezi-Mungu,

kwa wema na fadhili zako;

unielekee kwa wingi wa huruma yako.

17Usimfiche mtumishi wako uso wako;

unijibu haraka, maana niko hatarini.

18Unijie karibu na kunikomboa,

uniokoe na maadui zangu wengi.

19Wewe wajua ninavyotukanwa,

wajua aibu na kashfa ninazopata;

na maadui zangu wote wewe wawajua.

20Kashfa zimeuvunja moyo wangu,

nami nimekata tamaa.

Nimetafuta kitulizo lakini sikupata,

wa kunifariji lakini sikumpata.

21Walinipa sumu kuwa chakula,

na nilipokuwa na kiu wakanipa siki.

22Karamu zao na ziwe mtego kwao,

na sikukuu zao za sadaka ziwanase.

23Macho yao yatiwe giza wasiweze kuona,

uitetemeshe daima migongo yao.

24Uwamwagie hasira yako,

ghadhabu yako iwakumbe.

25Kambi zao ziachwe mahame,

asiishi yeyote katika mahema yao.

26Maana wanawatesa wale uliowaadhibu,

wanawaongezea majeraha wale uliowajeruhi.

27Uwaadhibu kwa kila uovu wao;

uwakatalie kabisa msamaha wako.

28Uwafute katika kitabu cha walio hai,[#69:28 Taz 40:7 maelezo. Mfano wa kitabu cha Mungu ambamo yameorodheshwa majina ya watu wake wote kinatajwa pia katika 87:6; Kut 32:32-33; Dan 12:1; Fil 4:3; Ufu 3:5; 13:8; 17:8; 20:12.]

wasiwemo katika orodha ya waadilifu.

29Lakini mimi mnyonge na mgonjwa;

uniinue juu, ee Mungu, uniokoe.

30Kwa wimbo nitalisifu jina la Mungu,

nitamtukuza kwa shukrani.

31Jambo hili litampendeza Mwenyezi-Mungu zaidi,

kuliko kumtolea tambiko ya ng'ombe,

kuliko kumtolea fahali mzimamzima.

32Wanyonge wataona hayo na kufurahi;

wanaomheshimu Mungu watapata moyo.

33Mwenyezi-Mungu huwasikiliza fukara;

hatawasahau kamwe watu wake wafungwa.

34Enyi mbingu na dunia msifuni Mungu;

bahari na vyote vilivyomo, msifuni.

35Maana Mungu atauokoa mji Siyoni,

na kuijenga tena miji ya Yuda.

Watu wake wataishi humo na kuimiliki;

36wazawa wa watumishi wake watairithi,

wale wanaopenda jina lake wataishi humo.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania