The chat will start when you send the first message.
1Mwenyezi-Mungu anatawala!
Furahi, ee dunia!
Furahini enyi visiwa vingi!
2Mawingu na giza nene vyamzunguka;
uadilifu na haki ni msingi wa utawala wake.
3Moto watangulia mbele yake,
na kuwateketeza maadui zake pande zote.
4Umeme wake wauangaza ulimwengu;
dunia yauona na kutetemeka.
5Milima yayeyuka kama nta mbele ya Mwenyezi-Mungu;[#97:2-5 Mwanazaburi, kwa ukamilifu kabisa anatumia picha zote za Biblia ambazo zinatumiwa mara nyingi kueleza kuweko au kutokea kwake Mwenyezi-Mungu. Kwa kuwa yeye ni mfalme mkuu na Muumba wa vyote, viumbe vyote na hata visivyo na uhai vinaguswa na hivyo kuonesha uwezo wake mkuu. Taz 18:7-15; 29:3-9; 46:6-7; 83:13-16.]
naam, mbele ya Bwana wa dunia yote.
6Mbingu zatangaza uadilifu wake;
na mataifa yote yauona utukufu wake.
7Wote wanaoabudu sanamu wanaaibishwa,
naam, wote wanaojisifia miungu duni;
miungu yote husujudu mbele zake.
8Watu wa Siyoni wanafurahi;
watu wa Yuda wanashangilia,
kwa sababu ya hukumu zako, ee Mungu.
9Wewe Mwenyezi-Mungu ni mkuu juu ya dunia yote;
wewe watukuka juu ya miungu yote.
10Mwenyezi-Mungu huwapenda wanaochukia uovu,
huyalinda maisha ya watu wake;
huwaokoa makuchani mwa waovu.
11Mwanga humwangazia mtu mwadilifu,[#97:11 Mwanga ni mfano au kielelezo cha wokovu wa Mungu; ni picha ya fadhili na baraka za Mungu ambazo zinamiminiwa watu wake.]
na furaha kwa watu wanyofu wa moyo.
12Furahini kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu;
mshukuruni kwa ajili ya jina lake takatifu.