The chat will start when you send the first message.
1Kwa hiyo, ndugu zangu, maadamu Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: Mtoleeni Mungu miili yenu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu.[#12:1 Ni maneno yanayotumiwa kuunga mawazo yaliyokwisha tolewa katika sehemu iliyopita na hii sasa inayofuata katika sura hii ya kumi na mbili. Paulo anatumia mtindo wa uandishi wa namna hiyo (taz pia 4:16; 7:12; 8:1,31).; #12:1 Paulo amekwisha sisitiza kuwa Mungu yu tayari kumhurumia mtu yeyote na hii yategemea matakwa yake Mungu mwenyewe, si ya mwanadamu (taz 9:15-18,23). Imani kuwa Mungu ana huruma nyingi unatokana na yale aliyokwisha sema kuwa yeye Mungu huhurumia si Wayahudi tu bali hata wale ambao si Wayahudi (taz 9:15).; #12:1 Yaani wajitoe kikamilifu.; #12:1 Paulo anawakumbusha jinsi hapo awali K.K. walivyotoa sadaka za wanyama kwa niaba yao wenyewe hizo zikateketezwa kwa ajili ya dhambi zao. Sasa Kristo amekwisha kujitoa kwa ajili yao, iliyopo ni wao kutoa maisha yao kwake (ling Ebr 5:1-14; 10:19-23; 13:10-15) kimwili, kiroho na kiakili.; #12:1 Paulo anataka kusisitiza ujumbe wake kama wale manabii wa Agano la Kale wakina Isaya (taz Isa 1:13-20); Hosea (taz Hos 6:6) na Amosi (taz Amo 5:21-27).]
2Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu na kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu.[#12:2 Yaani tabia za kidunia hizo zisizopatana na mapenzi ya Mungu. Katika Biblia mambo ya kiulimwengu yanatajwa kuwa ni kinyume cha yale ya mbinguni. Maana ya kiulimwengu yahesabika kuwa ya mfalme wa ulimwengu - Shetani na ya mbinguni ni ya Mungu Muumba.; #12:2 Mwelekeo kuwa mwenye kufanya mapinduzi ndani ya mwanadamu ni Mungu na si kazi ya mwanadamu mwenyewe; hivyo Myahudi hana budi kumtii na kumtegemea huyo mwenye uwezo mkuu.; #12:2 Yaani mawazo: mawazo mema hutokana na uongozi wa Mungu ndivyo Paulo anavyotaka kusema.]
3Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni nyinyi nyote: msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kadiri ya kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja.[#12:3 Huu ni kama ushuhuda wake Paulo jinsi hapo mwanzoni alivyokuwa mpinzani wa Ukristo hata kuwaua Wakristo, lakini Mungu akageuza maisha yake, akatendewa kwa huruma maana hakustahili; kwa hiyo akiangalia hayo anaona ametendewa kwa neema.; #12:3 Taz maelezo aya ya 2.; #12:3 Kwa mara nyingine mkazo wake Paulo unarudia, kwake, imani hutoka kwa Mungu, kwa hiyo mtu mwingine yeyote hana la kujivunia.]
4Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake.[#12:4 Mfano Paulo anaopenda kuutumia katika barua zake anapotaka kueleza jinsi Wakristo walivyo, yaani kuhusu umoja wao na huduma yao. Anasisitiza kuwa jinsi walivyoitwa na Bwana yuleyule, basi wameunganika pamoja na huduma yao ni ya pamoja.]
5Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake.[#12:5 Ni mkazo kuhusu utumiaji wa au vipawa. Kuhusu neno tafsiri nyingine ni . Vipaji hivyo anavitaja pia katika barua yake ya kwanza kwa Wakorintho ambamo anatoa maelezo marefu (taz 1Kor 12). Sababu ya Paulo kutaja vipaji hivi ni kwamba kulikuwa kumetokea kudharauliana kati ya Wakristo fulani waliojiona kuwa wao ni bora kuliko wengine, kwa zile kazi walizokuwa nazo.]
6Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kadiri ya neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake.
7Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. Mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe.
8Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha.
9Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema.[#12:9-13 Paulo anaelekeza namna ya kutumia vipaji walivyopewa. Utumiaji wa vipaji unatokana na upendo, jambo ambalo anaona ni la maana sana katika Wakristo. Ni sababu upendo haubagui wala haujivuni. Mkazo huu wa utumiaji wa vipaji kwa kusukumwa na upendo unapanuliwa zaidi katika 1Kor 12 kuhusu vipaji na katika 1Kor 13 kuhusu upendo.]
10Pendaneni kindugu; kila mmoja amfikirie kwanza mwenzake kwa heshima.
11Msilegee katika bidii, ila muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana.
12Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida, na kusali daima.
13Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu.[#12:13 Yaani wale walio Wayahudi na wasio Wayahudi. Upendo ni wa kudhihirika kwa kila mtu bila ubaguzi.]
14Watakieni baraka wote wanaowadhulumu nyinyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani.[#12:14 Anaelekeza jinsi upendo unavyopaswa kuoneshwa kwa wengine. Ni maendelezo ya mistari inayotangulia yaani 9-13. Mkazo unagusia mafundisho ya Yesu aliyoyatoa mlimani (taz Mat 5:43-48; ling 5:21-26,34-42). Naye Yesu alionesha mfano wa kupenda maadui alipowaombea waliomtesa (taz Luka 23:34). Na alimwona Stefano akiwaombea hao waliomtesa wakati alipokuwa karibu kufa (Mate 6:8—7:60).; #12:14-21 Maendelezo ya maelezo kuhusu upendo.]
15Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wenye kulia.[#12:15 Mkazo aliokwisha dokeza katika aya ya 12. Na katika baadhi ya barua zake anasisitiza jambo hili (taz 1 Kor 4:12). Kufurahi na wenye kufurahi na kulia na wenye kulia ni matendo yanayoonesha upendo kwa kila aina ya watu katika hali waliyomo - hapa hakuna ubaguzi. Mkazo wa Paulo ni kwamba Mkristo kufanya hivyo ni wajibu wake kwani anapaswa kufanya kama Bwana Yesu alivyofanya.]
16Ishini kwa kupatana vema nyinyi kwa nyinyi. Msijitakie makuu, bali jishughulisheni na madogo. Msijione kuwa wenye hekima sana.[#12:16 Karibu ni marudio ya yale Paulo aliyosema katika aya ya 13 aliposema yaani wasijivune kufuata vipaji walivyonavyo au hali ya kurithi kwao, wote waishi kwa amani.]
17Msilipe ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote.
18Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote.
19Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza, asema Bwana.”[#12:19 Kutolipiza kisasi ni dalili ya kuonesha upendo kwa adui, fundisho ambalo limo katika kumb 32:35; ling Lawi 19:18. Naye Yesu Kristo alikwisha kaza hayo katika mafundisho yake pale mlimani (taz mst 5:39; taz pia maelezo ya aya ya 14).]
20Zaidi ya hayo, Maandiko yasema: “Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake.”[#12:20 Msemo uliotumika kueleza kuwa mtu baada ya muda atajisikia akiumia sana, au kwa maneno mengine, akichomwa rohoni na huenda akatubu. Haya yamenukuliwa toka aya 25:21-22 (ling aya 5:44).]
21Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema.