The chat will start when you send the first message.
1Kila mtu anapaswa kuwatii wenye mamlaka katika serikali; maana mamlaka yote hutoka kwa Mungu; nao wenye mamlaka wamewekwa na Mungu.[#13:1 Kutii kunakotajwa hapa ni kule kwa kufuata sheria zilizowekwa na viongozi wa nchi. Ni kama Paulo anakaza kuwa nchi bila sheria haiwezi kuendelea vizuri, amani haiwezi kuwepo.; #13:1 Bila shaka Paulo anamaanisha wale ambao wanatawala kufuatana na matakwa ya Mungu.; #13:1 Yaani hakuna atawalaye bila kuwekwa na Mungu. Swali ni kuhusu wale wabaya wasiotenda matakwa ya Mungu, hao bila shaka ni wale waasi kama mfalme Shauli (taz pia 12:11; ling Tit 3:1; Yoh 19:11; Mit 8:15) ingawa Paulo hajiingizi katika kueleza hao wabaya nani amewaweka.; #13:1 Ni mkazo kuwa hakuna Mungu asilojua. Hapa bila shaka Paulo anawaelekeza hao aliowaandikia akiwashauri ili wasidharau na kutojali viongozi ambao hawakuwa Wakristo. Wakati ule viongozi wa nchi nyingi hawakuwa Wakristo hasa wa dola ya Roma. Yeye Kristo alionesha mfano mwema alipokubali kuwekwa mikononi mwa watawala wa Kiroma (taz Mat 27:11-50; Marko 15:1-37; Luka 23:1-47; Yoh 18:28-30). Na alipoulizwa kuhusu kutoa kodi alijibu kuwa Kaisari alipwe yaliyo yake na Mungu alipwe yaliyo yake (taz Mat 22:15-22; Marko 12:13-17; Luka 20:19-26). Kwa namna fulani Paulo anawashauri Wakristo wafanye kama Kristo.]
2Anayepinga mamlaka ya viongozi anapinga agizo la Mungu; nao wafanyao hivyo wanajiletea hukumu wenyewe.[#13:2-4 Kuelewa kwa Paulo kuhusu viongozi.]
3Maana, watawala hawasababishi hofu kwa watu wema, ila kwa watu wabaya. Basi, wataka usimwogope mtu mwenye mamlaka? Fanya mema naye atakusifu;
4maana yeye ni mtumishi wa Mungu anayefanya kazi kwa faida yako. Lakini ukifanya mabaya, basi, huna budi kumwogopa, maana anao kweli uwezo wa kuadhibu. Yeye ni mtumishi wa Mungu, kuwaonesha ghadhabu yake wale watendao maovu.[#13:4 Maneno haya yamenukuliwa mara mbili katika aya moja. Paulo anamaanisha kuwa mtawala amepewa mamlaka na Mungu kwa hiyo anatenda kazi yake.; #13:4 Anafanya hivyo kwa kuwa huyo ameruhusiwa na Mungu, lakini Mkristo mmojammoja hana ruhusa kujilipiza kisasi au kutoa hukumu kwa kuwa hiyo ni kazi ya Mungu (taz 12:19-21).]
5Kwa hiyo ni lazima kuwatii wenye mamlaka, si tu kwa sababu ya kuogopa ghadhabu ya Mungu, bali pia kwa sababu dhamiri inadai hivyo.[#13:5 Hapa ni marudio ya yale aliyokwisha sema katika aya ya 1.]
6Kwa sababu hiyohiyo nyinyi hulipa kodi; maana viongozi hao humtumikia Mungu ikiwa wanatimiza wajibu wao.[#13:6 Jambo la kulipia ni la tangu zamani. Paulo ni kama anasisitiza yale Yesu aliyokwisha sema kuwa wampe Kaisari yaliyo yake (taz Mat 22:15-22; Marko 12:13-17; Luka 20:19-26); kulipa ya mtu binafsi, wa vitu (Mat 17:25) na kutoa heshima kwa anayestahili ni wajibu wa kila mtu. Kwa hiyo hata hao anaowaambia huko Roma wajue kuwa wanapaswa kufanya vivyo hivyo, ingawa wanajua kuwa Mungu ndiye Mfalme mkuu naye Yesu Kristo anatawala pamoja naye (taz Marko 16:19; Mate 1:6-11). Kwa jumla hapa Paulo haoneshi hali ya kupingana na utawala wa Kiroma ingawa baadaye watumishi wa serikali ya Kiroma watamshika na kumwua (taz 2Tim 1:16-17; 2:9; 4:16-18).]
7Mpeni kila mtu haki yake; mtu wa ushuru, ushuru; wa kodi, kodi; na astahiliye heshima, heshima.
8Msiwe na deni kwa mtu yeyote, isipokuwa tu deni la kupendana. Ampendaye jirani yake ameitekeleza sheria.[#13:8 Yaani maadili yao yapatane na matakwa ya Mungu.; #13:8 k.m. hizo anazotaja katika aya ya 9. Hizi na nyingine zilitolewa na Mungu pale mlimani Sinai (taz Kut 20:3-17; Kumb 5:7-21).]
9Maana, amri hizi: “Usizini; Usiue; Usitamani”; na nyingine zote, zimo katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.”[#13:9 Hapa Paulo aliona yafaa anukuu maneno ya Yesu aliyowaambia wafuasi wake kuwa wapendane (taz Yoh 15:12,17). Naye Yesu Kristo alinukuu maneno ya amri hiyo toka Lawi 19:18 (ling Kut 20:13-17; Kumb 5:17). Mkazo huo wa watu kupendana unasisitizwa pia na Yohana katika barua zake (taz 1Yoh 3:11-18; 4:7-21; 5:1-5; 2Yoh 1:6).]
10Ampendaye jirani yake hamtendei vibaya. Basi, upendo ni utimilifu wa sheria.[#13:10 Ni mafafanuzi ya aya ya 9.]
11Zaidi ya hayo, nyinyi mnajua tumo katika wakati gani: sasa ndio wakati wa kuamka usingizini; naam, wokovu wetu uko karibu zaidi sasa kuliko wakati ule tulipoanza kuamini.[#13:11-14 Onyo kwa waumini kuwa wasitende kinyume cha mapenzi ya Mungu. Kwa maneno mengine Paulo anataka kukaza kuwa Mkristo lazima adumu katika imani.]
12Usiku unakwisha na mchana unakaribia. Basi, tutupilie mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga.[#13:12 Hapa unatajwa kwanza, ndivyo walivyoanza kuhesabu siku, yaani jioni ilipowadia wakaanza kuhesabu kuwa siku mpya imeanza, lakini kwa upande mwingine usiku ulivyo na giza unahesabika kuwa wenye maovu kwa kuwa waovu hutenda yasiyo matakwa ya Mungu kwa kujificha wasionekane. Kwa hiyo usiku hapa unaelezwa kimfano na maelezo yake yamo katika aya ya 13 (ling Gal 4:18,20-21). Matendo ya gizani ni kama yanavyoelezwa katika Gal 5:18-21 kuwa ya mwili.; #13:12 Mchana ni kinyume cha giza kwa hiyo mtu atendapo matendo kufuatana na matakwa ya Mungu mtu huyo ndiye anayetajwa kuwa anatembea kwenye mwanga. Mahali pengine matendo ya namna hiyo Paulo anayataja kuwa ya Roho (taz Gal 5:22-25; ling Efe 5:9).]
13Na tuishi kwa adabu kama inavyostahili wakati wa mchana, na wala sio kwa ulafi na ulevi, uchafu na uasherati, ugomvi na wivu.
14Bwana Yesu Kristo awe vazi lenu; msishughulikie tena tamaa zenu za maumbile na kuziridhisha.[#13:14 Msemo huu ni wa kimfano. Maana yake ni kwamba kama mtu anavyovaa nguo ikasitiri mwili wake, vivyo hivyo na mtu akimwamini Kristo, basi roho yake itasetiriwa dhidi ya yule Mwovu Shetani, naye atashinda tamaa za ulimwengu huu (taz pia Gal 5:19-21) mahali fulani tunasoma kuwa kuvaa vazi jipya ni tendo la heshima; k.m. Mwa 41:42; Kut 28:2-4,41; 29:5; 31:10; 40:13; Hes 20:28; Esta 6:11; 8:15; Luka 15:22; ling Ufu 3:4-5; 15:6; 19:13.]