The chat will start when you send the first message.
1Basi, Tobia akamjibu baba yake, “Baba mimi nitatimiza yote uliyoniagiza.
2Lakini nitaipataje hiyo fedha kutoka kwa Gabaeli hali simjui? Nitampa kitambulisho gani aweze kusadiki na kunipatia hiyo fedha? Isitoshe njia ya kwenda Media siijui.”
3Hapo Tobiti akamjibu mwanawe Tobia, “Gabaeli na mimi tuliandika hati ya mapatano na kuweka sahihi zetu. Kisha tukaipasua katikati; nusu moja anayo yeye pamoja na fedha na nusu nyingine ninayo mimi. Tulikabidhiana miaka ishirini iliyopita! Sasa, nenda ukamtafute mtu wa kuaminika atakayekusindikiza hadi Media na kurudi nawe hapa. Mtakaporudi tutamlipa mshahara wake. Lakini ni lazima uipate fedha niliyomwachia Gabaeli.”
4Basi, Tobia akaenda kumtafuta mtu aliyejua njia ya kwenda Media ili wasafiri pamoja. Mara baada ya kutoka nyumbani, Tobia alikutana uso kwa uso na Rafaeli. Tobia hakujua kwamba Rafaeli alikuwa malaika wa Mungu,
5hivi akamwuliza, “Unatoka wapi?” Rafaeli akajibu, “Mimi ni Mwisraeli, mmoja wa jamaa zako wa mbali, na nimekuja hapa Ninewi kutafuta kazi.” Tobia akamwuliza, “Unaijua njia ya kwenda Media?”
6Rafaeli akajibu, “Ndiyo, naijua. Nimekuwa nikienda Media mara nyingi, na barabara zote nazijua vizuri. Kule Media nilikuwa nakaa na jamaa yetu Gabaeli, ambaye anakaa mjini Rage. Rage ni milimani na ni mwendo wa siku kama mbili hadi Ekbatana, mji mkuu wa Media.”[#5:6 Mji uliokuwa kati ya Ninewi na Rage.]
7Basi, Tobia akamwambia Rafaeli, “Ningoje hapa, rafiki yangu; nakwenda kumweleza babangu. Ningependa unisindikize hadi Media, nami nitakulipa kwa safari hiyo.”
8Rafaeli akasema, “Nenda, lakini usikawie sana.”
9Tobia aliingia ndani, na kumwambia baba yake, “Nimempata Mwisraeli mwenzangu atakayenisindikiza katika safari yangu.” Tobiti akajibu, “Mwite aje ndani. Ningependa kujua ni wa jamaa gani na kabila gani, na kama ni mtu wa kuaminika safarini pamoja nawe.”
10Basi, Tobia akatoka nje, akamwita Rafaeli akisema, “Baba yangu anakuita.” Rafaeli alipoingia ndani, Tobiti alianza kumwamkia mgeni huyo. Naye malaika akamwitikia, akimtakia furaha kwa wingi. Lakini Tobiti akamjibu, “Nitakuwaje na furaha tena? Mimi ni kipofu, na sioni kitu. Nimezama gizani kama wafu wasiouona tena mwanga. Inawezekana nimekwisha fariki! Naweza kuwasikia watu wakiongea, lakini siwezi kuwaona.” Malaika akamwambia Tobiti, “Jipe moyo! Mungu atakuponya hivi karibuni. Usihangaike!”
Kisha Tobiti akasema, “Mwanangu Tobia anataka kwenda Media. Je, unaweza kufuatana naye na kumwonesha njia? Nitakulipa, usiwe na wasiwasi.” Rafaeli akajibu, “Bila wasiwasi, naweza kwenda naye. Nimekwenda huko mara nyingi, na nazijua barabara zote za milimani na mabondeni.”
11Tobiti akamwuliza, “Hebu niambie, ndugu yangu, wewe ni wa jamaa gani na ni wa kabila gani?”
12Lakini Rafaeli akamwuliza, “Kwa nini unataka kujua kabila langu?” Naye Tobiti akaendelea kusema, “Nataka kujua kwa hakika wazazi wako ni nani na jina lako ni nani.”
13Rafaeli akajibu, “Jina langu ni Azaria, na ni mwana wa mzee Anania, jamaa yako.”
14Basi, Tobiti akamwambia, “Karibu sana, ndugu! Usikasirike kwa sababu nilitaka kujua ukweli juu yako na jamaa yako. Kumbe, wewe ni wa jamaa yangu, jamaa nzuri inayoheshimika! Nawajua Anania na Nathani, wale wana wawili wa mzee maarufu Shemaya. Tulizoea kwenda pamoja kuhiji Yerusalemu; wao hawajapata kamwe kuiacha njia njema. Jamaa zako ni watu waadilifu; umetoka katika ukoo mwema!”
15Tobiti akaendelea kusema, “Nitakulipa mshahara wa kawaida wa kutwa, na kulipa gharama zako na za mwanangu. Basi, nenda na mwanangu,
16na mkirudi salama nitakuongezea kitu.” Rafaeli akajibu, “Nitakwenda naye, wala usiwe na wasiwasi. Tutakwenda na kurudi salama. Hakuna hatari njiani.”
17Basi Tobiti akasema, “Ndugu, nakutakia baraka za Mungu.” Kisha akamwita Tobia, akamwambia, “Mwanangu, tayarisha kila kitu mnachohitaji kwa safari, uondoke pamoja na ndugu yako. Mungu wa mbinguni awalinde huko ng'ambo, awarudishe kwangu salama salimini. Malaika wake aende nanyi na kuwalinda njiani, mwanangu!”
Kabla ya kuanza safari ya Media, Tobia alimbusu baba yake na mama yake. Tobiti akamwambia, “Safari njema!”
18Ndipo Ana, mama yake Tobia akaanza kulia, akamwambia mumewe, “Unawezaje kumtuma mtoto wetu mbali namna hiyo? Yeye ndiye tegemeo letu akiwa pamoja nasi.
19Usiithamini sana fedha hata kuhatarisha uhai wa mtoto wetu.
20Hali ya maisha tuliyopangiwa na Mungu inatufaa!”
21Lakini Tobiti akamwambia mkewe, “Usiwe na wasiwasi dada. Mtoto wetu atakwenda na kurudi salama. Nawe utamwona tena kwa macho yako. Usiseme tena; wala kuhangaika juu yao, mpenzi! Malaika mwema atakwenda naye. Mtoto wetu atasafiri salama na kurudi mwenye afya njema.”