Zekaria 13

Zekaria 13

1“Siku hiyo, kutatokea chemchemi ya kuwatakasa dhambi na unajisi wazawa wa Daudi na wakazi wote wa Yerusalemu.[#13:1 Kuhusu picha ya maji au chemchemi inayoweza kutakasa, taz Zab 46:4; Eze 47:1-12; Yoe 3:18. Taz pia Yoh 4:10-14; 7:37-38; Ufu 21:6; 22:1-2.]

2Wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, majina ya vinyago vya miungu nchini nitayaondoa, wala hayatakumbukwa tena. Na wanaojidai kuwa manabii nitawaondolea mbali pamoja na tamaa zao za kuabudu sanamu.

3Mtu yeyote akijidai kuwa nabii, baba na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Unapaswa kufa kwa kuwa unasema uongo kwa jina la Mwenyezi-Mungu’. Na haohao wazazi wake watamchoma kisu akiwa anatabiri.[#13:3 Kuhusu wenye kutabiri uongo kwa jina la Mwenyezi-Mungu, rejea Neh 6:10-12; Yer 23:9-23; Eze 13; Amo 7:10-17; Mika 3:5-7.]

4Siku hiyo, kila nabii atayaonea aibu maono yake anapotabiri. Hawatavaa mavazi ya manyoya ili kudanganya watu,

5bali kila mmoja atasema, ‘Mimi si nabii. Mimi ni mkulima tu; nimeimiliki ardhi tangu ujana wangu’.

6Na mtu akimwuliza mmoja wao, ‘Vidonda hivi ulivyo navyo mgongoni vimetoka wapi?’ Yeye atajibu, ‘Vidonda hivi nilivipata katika nyumba ya rafiki zangu.’”[#13:6 Katika aya hii habari kuhusu vidonda mgongoni mwa wale waliotabiri yamkini yahusu desturi ya manabii wa kale wa Kanaani ambao wakati wa kutabiri na wawapo katika kupagawa walijikatakata mwilini (1Fal 18:28-29; Hos 7:14).]

7Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:

“Amka, ee upanga!

Inuka umshambulie mchungaji wangu;

naam, mchungaji anayenitumikia.

Mpige mchungaji na kondoo watawanyike.

Nitaunyosha mkono wangu,

kuwashambulia watu wadhaifu.

8Theluthi mbili za watu katika nchi zitaangamizwa;

ni theluthi moja tu itakayosalimika.

9Theluthi hiyo moja itakayosalia,

nitaijaribu na kuitakasa,

kama mtu asafishavyo fedha,

naam, kama ijaribiwavyo dhahabu.

Hapo wao wataniomba mimi,

nami nitawajibu.

Nitasema, ‘Hawa ni watu wangu’,

nao watasema, ‘Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu wetu.’”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania