The chat will start when you send the first message.
1Katika maono mengine, Mwenyezi-Mungu alinionesha kuhani mkuu Yoshua amesimama mbele ya malaika wa Mwenyezi-Mungu, na upande wake wa kulia amesimama Shetani kumshtaki.[#3:1 Rejea Ezra 5:2. Kama vile Zerubabeli, kuhani mkuu Yoshua anatajwa mara kwa mara katika maandishi yanayohusu wakati mara tu Waisraeli waliporudi kutoka uhamishoni Babuloni. Wakati huo Yoshua alikuwa kiongozi wa kidini, naye Zerubabeli alikuwa kiongozi wa kiraia wa jumuiya ya Wayahudi baada ya uhamisho. Taz pia Hag 1:1,12,14; Zek 4:11-14.; #3:1 Kulingana na makala moja ya kale (Peshita). Kiebrania kina “Mwenyezi-Mungu”.]
2Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia huyo Shetani, “Mwenyezi-Mungu na akulaani, ewe Shetani! Naam, Mwenyezi-Mungu aliyeuteua mji wa Yerusalemu na akulaani! Mtu huyu ni kama kinga kilichonyakuliwa kutoka motoni!”[#3:2 Yuda 9.; #3:2 Msemo huu ni kama methali kuelezea kuponea chupuchupu au kama kwa muujiza (Amo 4:11).]
3Kuhani mkuu Yoshua alikuwa amesimama mbele ya malaika, akiwa amevaa mavazi machafu.[#3:3-4 Bila shaka mavazi hayo yalikuwa ni picha ya dhambi ya Yoshua, ya makuhani na hata ya watu wenyewe Waisraeli. Rejea Ufu 19:8. Na kuhusu maneno “nimeiondoa dhambi yako” taz Isa 6:7.]
4Malaika akawaambia watumishi wake, “Mvueni kuhani mkuu Yoshua mavazi yake machafu.” Kisha akamwambia kuhani mkuu Yoshua, “Tazama, nimeiondoa dhambi yako, nami nitakupa mavazi ya thamani.”
5Kisha akawaambia wamvike kilemba safi kichwani. Hivyo, wakamvika kilemba safi na mavazi; naye malaika wa Mwenyezi-Mungu alikuwa amesimama hapo.
6Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwonya kuhani mkuu Yoshua, akamwambia,
7“Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Ukifuata mwongozo wangu na kuyazingatia maagizo niliyokupa, basi, utaisimamia nyumba yangu na nyua zake. Nami nitakuwezesha kuingia katika utumishi wangu kama hawa wanaosimama mbele yangu.
8Sasa sikiliza kwa makini, ewe Yoshua, kuhani mkuu; sikilizeni pia enyi makuhani wenzake mlio pamoja naye, nyinyi mlio ishara ya wakati mzuri ujao: Nitamleta mtumishi wangu aitwaye Tawi.[#3:8 Rejea Isa 42:1; 49:5-6; 52:13; Hag 2:23.; #3:8 Jina hili ni jina la sifa la Masiha au yule mtumishi anayetumwa na Mungu kuwaokoa watu wake (Isa 11:1), jina ambalo kwanza lilitumiwa kwa Zerubabeli ambaye ndiye aliyekuwa mwakilishi halali wa ukoo wa kifalme wa Daudi (rejea Zek 6:12-13). Tafsiri ya Kigiriki ina “mwanga unaochomoza” badala ya “tawi” (rejea Luka 1:78).]
9Kumbukeni kuwa nimeweka mbele ya Yoshua jiwe moja lenye nyuso saba. Nami nitachora maandishi juu yake, na kwa siku moja tu, nitaiondoa dhambi ya nchi hii. Naam, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema.[#3:9 Tafsiri nyingine yamkini “jiwe … lenye pande saba”. Wafafanuzi wa Biblia wanafikiri hapa yahusu jiwe la thamani ambalo kuhani mkuu alilichukua katika kilemba chake (rejea Kut 28:36-38). Wengine wanafikiri nyuso hizo saba ni picha inayotaka kusema juu ya kuweko kwake Mwenyezi-Mungu ambaye kutoka hekaluni anasimamia mambo yote yanayotukia ulimwenguni (rejea Zek 4:10).]
10Siku hiyo, kila mmoja wenu atamwalika mwenzake kufurahia amani na utulivu katika shamba lake la mizabibu na la mitini.’”