1 Nyakati 20

1 Nyakati 20

Kutekwa kwa Raba

(2Sam 12:26‑31)

1Mwanzoni mwa mwaka mpya, wakati wafalme huenda vitani, Yoabu aliliongoza jeshi. Aliangamiza nchi ya Waamoni, na akaenda Raba na kuuzingira, lakini Daudi alibaki Yerusalemu. Yoabu akashambulia Raba na kuuacha ukiwa magofu.

2Daudi akachukua taji kutoka kwa kichwa cha mfalme wao, lililokuwa na uzito wa talanta moja ya dhahabu, nalo lilizungushiwa vito vya thamani. Likawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Alichukua nyara nyingi kutoka mji huo.[#20:2 au taji la Milkomu (yaani Moleki ); #20:2 Talanta moja ni sawa na kilo 34.]

3Akawatoa watu waliokuwa humo, akawaweka wafanye kazi kwa misumeno, sululu za chuma na mashoka. Daudi akafanya hivi kwa miji yote ya Waamoni. Kisha Daudi na jeshi lake lote wakarudi Yerusalemu.

Vita na Wafilisti

(2Sam 21:15‑22)

4Baada ya muda, kulitokea vita dhidi ya Wafilisti, huko Gezeri. Wakati huo Sibekai, Mhushathi, akamuua Sipai, aliyekuwa mmoja wa wazao wa Warefai, nao Wafilisti wakashindwa.[#20:4 yaani majitu]

5Katika vita vingine na Wafilisti, Elhanani mwana wa Yairi alimuua Lahmi nduguye Goliathi, Mgiti, ambaye mkuki wake ulikuwa na mpini kama mti wa mfumaji.

6Katika vita vingine tena, vilivyopiganwa huko Gathi, kulikuwa na mtu mmoja mkubwa, mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita katika kila mguu: jumla vidole ishirini na vinne. Yeye alikuwa pia mzao wa Mrefai.

7Alipowadhihaki Israeli, Yonathani, mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akamuua.

8Hao walikuwa wazao wa Warefai huko Gathi, nao walianguka kwa mikono ya Daudi na watu wake.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.