1 Nyakati 22

1 Nyakati 22

1Ndipo Daudi akasema, “Nyumba ya Bwana Mungu itakuwa mahali hapa, pamoja na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya Israeli.”

Maandalizi kwa ajili ya Hekalu

2Kwa hiyo Daudi akatoa amri wakusanyike wageni wote walioishi Israeli, na kutoka miongoni mwao, akaweka waashi ili kuchonga mawe kwa ajili ya kujenga nyumba ya Mungu.

3Daudi akatoa chuma tele ili kutengenezea misumari kwa ajili ya mafungo ya malango ya nyumba na shaba tele isiyopimika.

4Pia akatoa magogo ya mwerezi yasiyohesabika, kwa kuwa Wasidoni na Watiro walikuwa wamemletea Daudi idadi kubwa ya mierezi.

5Daudi akasema, “Mwanangu Sulemani bado ni mdogo wa umri na hana uzoefu. Nyumba itakayojengwa kwa ajili ya Bwana inatakiwa iwe yenye uzuri mwingi na sifa na fahari mbele ya mataifa yote. Kwa hiyo nitaifanyia matayarisho.” Daudi akafanya matayarisho makubwa kabla ya kifo chake.

6Kisha akamwita Sulemani mwanawe, akamwagiza kujenga nyumba kwa ajili ya Bwana , Mungu wa Israeli.

7Daudi akamwambia Sulemani: “Mwanangu, nilikuwa na jambo hili ndani ya moyo wangu, kujenga nyumba kwa ajili ya Jina la Bwana Mungu wangu.

8Lakini neno la Bwana likanijia, kusema: ‘Wewe umemwaga damu nyingi na kupigana vita vingi. Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu.

9Lakini utakuwa na mwana ambaye atakuwa mtu wa amani na utulivu, nami nitampa utulivu mbele ya adui zake wote pande zote. Jina lake ataitwa Sulemani, nami nitawapa Israeli amani na utulivu wakati wa utawala wake.

10Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu. Yeye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake. Nami nitakiimarisha kiti chake cha utawala juu ya Israeli milele.’

11“Sasa, mwanangu, Bwana awe pamoja nawe, nawe uwe na mafanikio upate kuijenga nyumba ya Bwana Mungu wako, kama alivyosema utafanya.

12Bwana na akupe hekima na ufahamu wakati atakuweka juu ya Israeli, ili uweze kuishika sheria ya Bwana Mungu wako.

13Ndipo utakapofanikiwa, ikiwa utakuwa na bidii kutii amri na sheria Bwana alizompa Musa kwa ajili ya Israeli. Uwe hodari na ushujaa. Usiogope wala usikate tamaa.

14“Nimejitaabisha sana ili kupata mahitaji kwa ajili ya Hekalu la Bwana : talanta elfu mia moja za dhahabu, talanta milioni moja za fedha, na kiasi kisichopimika cha shaba na chuma, pia mbao na mawe. Nawe unaweza kuviongeza.[#22:14 Talanta 100,000 ni sawa na tani 3,750.; #22:14 Talanta 1,000,000 ni sawa na tani 37,500.]

15Unao wafanyakazi wengi: Wachonga mawe, waashi na maseremala, pamoja na watu walio na ustadi katika kila kazi

16wa kufua dhahabu, fedha, shaba na chuma, mafundi wasiohesabika. Sasa basi anza kazi hii, naye Bwana awe pamoja nawe.”

17Kisha Daudi akawaamuru viongozi wote wa Israeli wamsaidie Sulemani mwanawe.

18Akawaambia, “Je, Bwana Mungu wenu si yuko pamoja na ninyi? Pia si amewapa amani pande zote? Kwa maana amewatia wenyeji wa nchi mkononi mwangu, nayo nchi iko chini ya Bwana na watu wake.

19Sasa itoeni mioyo yenu na nafsi zenu katika kumtafuta Bwana Mungu wenu. Anzeni kujenga Maskani ya Bwana Mungu, ili mweze kulileta Sanduku la Agano la Bwana na vyombo vitakatifu vya Mungu katika Hekalu litakalojengwa kwa ajili ya Jina la Bwana .”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.