The chat will start when you send the first message.
1Basi Eliya Mtishbi, kutoka Tishbi katika Gileadi, akamwambia Ahabu, “Kama Bwana , Mungu wa Israeli ninayemtumikia, aishivyo, hapatakuwa na umande wala mvua katika miaka kadhaa ijayo, isipokuwa kwa neno langu.”
2Kisha neno la Bwana likamjia Eliya, kusema,
3“Ondoka hapa, elekea upande wa mashariki ukajifiche karibu na Kijito cha Kerithi, mashariki mwa Yordani.
4Utakunywa maji kutoka kile kijito, nami nimeagiza kunguru wakulishe huko.”
5Naye akafanya kama alivyoambiwa na Bwana . Akaenda katika Kijito cha Kerithi, mashariki mwa Yordani na akakaa huko.
6Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, naye akanywa maji kutoka kile kijito.
7Baada ya muda, kile kijito kikakauka kwa sababu mvua haikuwa imenyesha katika nchi.
8Kisha neno la Bwana likamjia Eliya, kusema,
9“Ondoka, uende Sarepta ya Sidoni, ukae huko. Nimemwagiza mjane wa huko ili akuhudumie.”
10Hivyo akaenda Sarepta. Alipofika kwenye lango la mji, alimkuta mjane akiokota kuni pale. Akamwita na kumwambia, “Naomba uniletee maji kidogo kwenye gudulia ili niweze kunywa.”
11Alipokuwa anaenda kumletea, akamwita akasema, “Tafadhali niletee pia kipande cha mkate.”
12Akamjibu, “Hakika kama Bwana Mungu wako aishivyo, sina mkate wowote, isipokuwa konzi moja ya unga kwenye chungu, na mafuta kidogo kwenye chupa. Ninakusanya kuni chache nipeleke nyumbani na nikapike chakula kwa ajili yangu na mwanangu, ili tule, kiishe, tukafe.”
13Eliya akamwambia, “Usiogope. Nenda nyumbani ukafanye kama ulivyosema. Lakini kwanza unitengenezee mkate mdogo kutoka vile ulivyo navyo kisha uniletee na ndipo utayarishe chochote kwa ajili yako na mwanao.
14Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Bwana , Mungu wa Israeli: ‘Kile chungu cha unga hakitakwisha wala ile chupa ya mafuta haitakauka hadi siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.’ ”
15Akaondoka na kufanya kama Eliya alivyomwambia. Kwa hiyo kukawa na chakula kila siku kwa ajili ya Eliya, yule mwanamke na jamaa yake.
16Kwa kuwa kile chungu hakikuisha unga na ile chupa ya mafuta haikukauka sawasawa na lile neno la Bwana lililonenwa na Eliya.
17Baada ya muda, mwana wa yule mwanamke mwenye nyumba akaugua. Hali yake ikaendelea kuwa mbaya sana, na hatimaye akaacha kupumua.
18Yule mjane akamwambia Eliya, “Una nini dhidi yangu, ewe mtu wa Mungu? Umekuja ili kunikumbusha dhambi yangu, na kusababisha kifo cha mwanangu?”
19Eliya akamjibu, “Nipe mwanao.” Eliya akampokea kutoka kifuani mwake, akambeba hadi chumba cha juu alipokuwa anaishi, akamlaza kitandani pake.
20Kisha akamlilia Bwana , akasema “Ee Bwana Mungu wangu, je, pia umeleta msiba juu ya mjane huyu ninayeishi kwake, kwa kusababisha mwanawe kufa?”
21Kisha akajinyoosha juu ya kijana mara tatu na kumlilia Bwana , akisema, “Ee Bwana Mungu wangu, nakuomba roho ya huyu kijana imrudie!”
22Bwana akasikia kilio cha Eliya, na roho ya kijana ikamrudia, naye akafufuka.
23Eliya akamtwaa kijana na kumbeba kutoka chumba chake cha juu, akamshusha, akampa mama yake na kusema, “Tazama, mwanao yu hai!”
24Ndipo yule mwanamke akamwambia Eliya, “Sasa ninajua kwamba wewe ni mtu wa Mungu, na kwamba neno la Bwana kutoka kinywani mwako ni kweli.”