The chat will start when you send the first message.
1Basi, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akakusanya jeshi lake lote. Akifuatana na wafalme thelathini na wawili wakiwa na farasi na magari ya vita, akakwea kuuzingira Samaria na kuishambulia kwa jeshi.
2Akawatuma wajumbe katika mji kwa Ahabu mfalme wa Israeli, kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi:
3‘Fedha yako na dhahabu yako ni vyangu; nao wake zako walio wazuri sana na watoto ni wangu.’ ”
4Mfalme wa Israeli akajibu, “Iwe kama usemavyo, bwana wangu mfalme. Mimi na vyote nilivyo navyo ni mali yako.”
5Wale wajumbe wakaja tena na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: ‘Nimewatuma kutaka fedha yako na dhahabu, wake zako na watoto wako.
6Lakini kesho wakati kama huu, nitawatuma maafisa wangu kukagua jumba lako la kifalme na nyumba za maafisa wako. Watatwaa kitu unachokithamini nao watakichukua.’ ”
7Mfalme wa Israeli akawaita wazee wote wa nchi, akawaambia, “Tazama jinsi mtu huyu anavyochochea matatizo! Alipotuma apelekewe wake zangu na watoto wangu, fedha zangu na dhahabu yangu, sikumkatalia.”
8Wazee na watu wote wakajibu, “Usimsikilize, wala usiyakubali matakwa yake.”
9Kwa hiyo akawajibu wajumbe wa Ben-Hadadi, “Mwambieni bwana wangu mfalme, ‘Mtumishi wako atafanya yote uliyoyadai mwanzoni, lakini dai hili la sasa siwezi kulitekeleza.’ ” Wakaondoka na kupeleka jibu kwa Ben-Hadadi.
10Kisha Ben-Hadadi akatuma ujumbe mwingine kwa Ahabu, kusema, “Miungu waniadhibu vikali zaidi ikiwa vumbi la Samaria litatosheleza konzi moja ya kila mtu ya wale wanaofuatana nami.”
11Mfalme wa Israeli akajibu, “Mwambieni, ‘Yule anayevaa mavazi ya vita asije akajisifu kama yule anayevua.’ ”
12Ben-Hadadi alisikia ujumbe huu wakati yeye na wafalme walikuwa wakinywa katika mahema yao, akawaamuru watu wake, “Jiandaeni kushambulia.” Kwa hiyo wakajiandaa kushambulia mji.
13Wakati huo huo nabii akamjia Ahabu, mfalme wa Israeli na kutangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana : ‘Je, unaona jeshi hili kubwa? Nitalitia mkononi mwako leo, nawe utajua kwamba mimi ndimi Bwana .’ ”
14Ahabu akauliza, “Ni nani atakayefanya hili?”
Nabii akamjibu, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana : ‘Maafisa vijana majemadari wa majimbo watafanya hili.’ ”
Akauliza, “Ni nani atakayeanzisha vita?”
Nabii akamjibu, “Ni wewe.”
15Hivyo, Ahabu akawaita maafisa vijana wapatao mia mbili thelathini na wawili (232) waliokuwa chini ya majemadari wa majimbo. Kisha akawakusanya Waisraeli waliobaki, ambao idadi yao walikuwa elfu saba.
16Wakaondoka wakati wa adhuhuri, Ben-Hadadi na wale wafalme thelathini na wawili walioungana naye walipokuwa katika mahema yao wakilewa.
17Maafisa vijana majemadari wa majimbo waliondoka kwanza.
Wakati huu Ben-Hadadi alikuwa amewatuma wapelelezi, ambao walileta taarifa kusema kwamba, “Askari wanasonga mbele kutoka Samaria.”
18Akasema, “Ikiwa wamekuja kwa amani, wakamate wakiwa hai; ikiwa wamekuja kwa vita, wakamate wakiwa hai.”
19Wale maafisa vijana majemadari wa majimbo wakatoka nje ya mji jeshi likiwa nyuma yao,
20kila mmoja akamuua adui yake. Hii ilisababisha Waaramu kukimbia, huku Waisraeli wakiwafuatia. Lakini Ben-Hadadi, mfalme wa Aramu akapanda farasi na kutoroka pamoja na baadhi ya wapanda farasi wake.
21Mfalme wa Israeli akasonga mbele, akawashinda farasi na magari ya vita ya adui, na kuwasababishia Waaramu hasara kubwa.
22Baadaye nabii akaja kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Jiandae vizuri ufikirie la kufanya, kwa sababu mwakani mfalme wa Aramu atakuja tena kukushambulia.”
23Wakati huo, maafisa wa mfalme wa Aramu wakamshauri, wakamwambia, “Miungu yao ni miungu ya vilimani. Ndiyo sababu walikuwa na nguvu sana kutuzidi. Lakini tukipigana nao katika nchi tambarare, hakika tutawashinda.
24Fanya hivi: Waondoe hao wafalme wote kutoka nafasi zao na uweke maafisa wengine mahali pao.
25Ni lazima pia uandae jeshi lingine kama lile ulilopoteza, farasi kwa farasi, gari la vita kwa gari la vita, ili tuweze kupigana na Israeli katika nchi tambarare. Kisha kwa hakika tutakuwa na nguvu kuliko wao.” Akakubaliana nao naye akashughulika ipasavyo.
26Mwaka uliofuata, majira kama hayo, Ben-Hadadi akawakusanya Waaramu, akaenda Afeki kupigana dhidi ya Israeli.
27Baada ya Waisraeli kukusanywa na kupewa mahitaji, walienda kukabiliana nao. Waisraeli wakapiga kambi mkabala nao kama makundi mawili madogo ya mbuzi, Waaramu wakiwa wameenea katika nchi.
28Yule mtu wa Mungu akaja na kumwambia mfalme wa Israeli, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana : ‘Kwa sababu Waaramu wanafikiri Bwana ni Mungu wa vilimani na sio Mungu wa mabondeni, nitalitia jeshi hili kubwa mkononi mwako, nawe utajua kuwa mimi ndimi Bwana .’ ”
29Kwa siku saba walipiga kambi wakitazamana, na siku ya saba vita vikaanza. Waisraeli wakawajeruhi askari wa miguu wa Waaramu wapatao elfu mia moja kwa siku moja.
30Waliobaki walikimbilia mji wa Afeki ambako elfu ishirini na saba kati yao waliangukiwa na ukuta. Naye Ben-Hadadi alikimbilia mjini na kujificha kwenye chumba cha ndani.
31Maafisa wake wakamwambia, “Tazama, tumesikia kwamba wafalme wa nyumba ya Israeli wana huruma. Twendeni kwa mfalme wa Israeli tukiwa tumevaa gunia viunoni mwetu na kamba kuzunguka vichwa vyetu. Huenda akakuacha hai.”
32Wakiwa wamevaa magunia viunoni mwao na kamba kuzunguka vichwa vyao, wakaenda kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Mtumishi wako Ben-Hadadi anasema: ‘Tafadhali, naomba uniache hai.’ ”
Mfalme akajibu, “Je, bado yuko hai? Yeye ni ndugu yangu.”
33Wale watu wakalipokea jambo lile kama dalili nzuri nao wakawa wepesi kulichukua neno lake wakisema, “Ndiyo, yeye ni ndugu yako Ben-Hadadi!”
Mfalme akawaambia, “Nendeni mkamlete.” Ikawa Ben-Hadadi alipokuja, Ahabu akampandisha katika gari lake la vita.
Ben-Hadadi akajitolea, akisema,
34“Nitairudisha miji ambayo baba yangu aliiteka kutoka kwa baba yako. Nawe utaweka mitaa yako katika Dameski, kama baba yangu alivyofanya kule Samaria.”
Ahabu akasema, “Kwa makubaliano, nitakuacha huru.” Hivyo, akaweka mkataba naye, kisha akamruhusu aende zake.
35Kwa neno la Bwana , mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake, “Nipige kwa silaha yako,” lakini yule mtu akakataa.
36Kwa hiyo yule nabii akasema, “Kwa sababu hukumtii Bwana , mara tu tutakapoachana utauawa na simba.” Na baada ya yule mtu kuondoka, simba akatokea na kumuua.
37Nabii akamkuta mtu mwingine na kumwambia, “Nipige, tafadhali!” Kisha yule mtu akampiga na kumjeruhi.
38Ndipo nabii akaenda na kusimama barabarani akimsubiri mfalme. Akajibadilisha kwa kushusha kitambaa cha kichwani mwake hadi kwenye macho.
39Mfalme alipopita pale, yule nabii akamwita, “Mtumishi wako alienda vitani mahali vilikuwa kali. Mtu mmoja akanijia akiwa na mateka, akasema, ‘Mlinde mtu huyu. Akitoroka, itakuwa uhai wako kwa uhai wake, ama utalipa talanta ya fedha.’[#20:39 Talanta moja ni sawa na kilo 34.]
40Mtumishi wako alipokuwa na shughuli nyingi hapa na pale, yule mtu akatoweka.”
Mfalme wa Israeli akasema, “Hiyo ndiyo hukumu yako. Wewe umeitaja mwenyewe.”
41Kisha yule nabii akajifunua macho yake haraka, na mfalme wa Israeli akamtambua kama mmoja wa manabii.
42Akamwambia mfalme, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana : ‘Umemwacha huru mtu niliyekusudia afe. Kwa hivyo ni uhai wako kwa uhai wake, watu wako kwa watu wake.’ ”
43Kwa uchungu na hasira, mfalme wa Israeli akaenda kwenye jumba lake huko Samaria.