The chat will start when you send the first message.
1Kwa wazee walio miongoni mwenu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shahidi wa mateso ya Kristo, na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa:
2lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe; si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika.
3Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali kuweni vielelezo kwa hilo kundi.
4Naye Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtapokea taji la utukufu lisiloharibika.
5Vivyo hivyo, ninyi mlio vijana watiini wazee. Nanyi nyote jivikeni unyenyekevu kila mtu kwa mwenzake, kwa kuwa,
“Mungu huwapinga wenye kiburi,
lakini huwapa wanyenyekevu neema.”
6Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake.
7Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye anajishughulisha sana na mambo yenu.
8Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza.
9Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.
10Nanyi baada ya kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha.
11Uweza una yeye milele na milele. Amen.
12Kwa msaada wa Silvano, ninayemhesabu kuwa ndugu mwaminifu, nimewaandikia waraka huu mfupi ili kuwatia moyo, na kushuhudia kwamba hii ni neema halisi ya Mungu. Simameni imara katika neema hiyo.[#5:12 yaani Sila]
13Kanisa lililoko Babeli, lililochaguliwa pamoja nanyi, wanawasalimu; vivyo hivyo mwanangu Marko anawasalimu.
14Salimianeni kwa busu la upendo.
Amani iwe nanyi nyote mlio katika Kristo.