The chat will start when you send the first message.
1Samweli akamwambia Sauli, “Mimi ndiye Bwana alinituma nikupake mafuta ili uwe mfalme juu ya watu wake Israeli; basi sasa sikiliza ujumbe kutoka kwa Bwana .
2Hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi: ‘Nitawaadhibu Waamaleki kwa kile walichowatendea Israeli walipowavizia wakati walipanda kutoka Misri.
3Basi sasa nenda ukawashambulie Waamaleki na kuwaangamiza kabisa pamoja na kila kitu kilicho mali yao. Usiwahurumie; waue wanaume na wanawake, watoto na wale wanaonyonya, ngʼombe na kondoo, ngamia na punda.’ ”
4Ndipo Sauli akawaita watu na kuwapanga huko Telaimu, askari wa miguu elfu mia mbili, na elfu kumi kutoka Yuda.
5Sauli akaenda katika mji wa Amaleki na kuwavizia bondeni.
6Kisha akawaambia Wakeni, “Ondokeni, waacheni Waamaleki ili nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao, kwa kuwa ninyi mliwatendea mema Waisraeli wote wakati walipanda kutoka Misri.” Basi Wakeni wakaondoka, wakawaacha Waamaleki.
7Ndipo Sauli akawashambulia Waamaleki toka Havila hadi Shuri, mashariki mwa Misri.
8Akamchukua Agagi mfalme wa Waamaleki akiwa hai, nao watu wake wote akawaangamiza kabisa kwa upanga.
9Lakini Sauli na hilo jeshi wakamhifadhi hai Agagi, na kondoo na ngʼombe walio wazuri, mafahali na wana-kondoo walionona, na kila kitu kilichokuwa kizuri. Hivi vitu hawakuwa radhi kuviangamiza kabisa, bali kila kitu kilichodharauliwa na kilicho dhaifu wakakiangamiza kabisa.
10Kisha neno la Bwana likamjia Samweli kusema:
11“Ninasikitika kwamba nimemfanya Sauli kuwa mfalme, kwa sababu ameacha kunifuata mimi na hakutimiza maagizo yangu.” Samweli akafadhaika, naye akamlilia Bwana usiku ule wote.
12Asubuhi na mapema Samweli akaamka kwenda kukutana na Sauli, lakini akaambiwa, “Sauli ameenda Karmeli. Huko amesimamisha mnara kwa heshima yake mwenyewe, naye ameendelea na kuteremkia Gilgali.”
13Samweli alipomfikia, Sauli akamwambia, “Bwana akubariki! Nimetimiza yale Bwana aliyoniagiza.”
14Lakini Samweli akasema, “Nini basi huu mlio wa kondoo masikioni mwangu? Huu mlio wa ngʼombe ninaousikia ni kitu gani?”
15Sauli akajibu, “Askari wamewaleta kutoka kwa Waamaleki, waliwaacha wale kondoo na ngʼombe wazuri ili kuwatoa dhabihu kwa Bwana , Mungu wako, lakini tuliwaangamiza kabisa wengine wote.”
16Samweli akamwambia Sauli, “Ngoja! Nami nitakuambia lile Bwana aliloniambia usiku huu.”
Sauli akajibu, “Niambie.”
17Samweli akamwambia, “Ingawa zamani ulijiona mdogo machoni pako mwenyewe, Je, hukuwa kiongozi wa makabila ya Israeli? Bwana alikupaka mafuta kuwa mfalme juu ya Israeli.
18Naye akakutuma kwa kazi maalum, akisema, ‘Nenda ukaangamize kabisa wale watu waovu, wale Waamaleki, upigane nao vita hadi utakapowaangamiza kabisa.’
19Kwa nini hukumtii Bwana ? Kwa nini ulivamia nyara na kufanya uovu machoni pa Bwana ?”
20Sauli akasema, “Lakini nilimtii Bwana . Nilikamilisha ile kazi ambayo Bwana alinituma. Niliwaangamiza Waamaleki kabisa na kumleta Agagi mfalme wao.
21Askari walichukua kondoo na ngʼombe kutoka nyara, kutoka kwa wale wazuri sana katika vitu vilivyotengewa Mungu, ili wavitoe kuwa dhabihu kwa Bwana Mungu wako huko Gilgali.”
22Lakini Samweli akajibu:
“Je, Bwana anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu
kama vile kuitii sauti ya Bwana ?
Kutii ni bora kuliko dhabihu,
nako kusikia ni bora
kuliko mafuta ya kondoo dume.
23Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya uaguzi,
nao ukaidi ni kama uovu wa kuabudu sanamu.
Kwa sababu umelikataa neno la Bwana ,
naye amekukataa wewe
kuendelea kuwa mfalme.”
24Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Nimetenda dhambi. Nimevunja amri ya Bwana na maagizo yako. Niliwaogopa watu na kwa hiyo nikafanya walivyotaka.
25Sasa ninakusihi usamehe dhambi yangu, nawe urudi pamoja nami, ili nipate kumwabudu Bwana .”
26Lakini Samweli akamwambia, “Sitarudi pamoja nawe. Umelikataa neno la Bwana , naye Bwana amekukataa wewe, usiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli!”
27Samweli alipogeuka ili aondoke, Sauli akangʼangʼania pindo la joho lake, nalo likararuka.
28Samweli akamwambia, “Bwana ameurarua ufalme wa Israeli kutoka kwako leo, naye ameutia kwa mmoja wa majirani zako, aliye bora kuliko wewe.
29Yeye aliye Utukufu wa Israeli hasemi uongo wala hana kigeugeu; kwa kuwa yeye si mwanadamu, hata abadili nia yake.”
30Sauli akajibu, “Nimetenda dhambi. Lakini tafadhali niheshimu mbele ya wazee wa watu wangu na mbele ya Israeli; rudi pamoja nami, ili nipate kumwabudu Bwana Mungu wako.”
31Hivyo Samweli akarudi pamoja na Sauli, naye Sauli akamwabudu Bwana .
32Ndipo Samweli akasema, “Niletee Agagi mfalme wa Waamaleki.”
Agagi akaja kwake kwa ujasiri, akifikiri, “Hakika uchungu wa mauti umepita.”
33Lakini Samweli akasema,
“Kama upanga wako ulivyofanya wanawake
kufiwa na watoto wao,
ndivyo mama yako atakavyokuwa
hana mtoto miongoni mwa wanawake.”
Naye Samweli akamuua Agagi mbele za Bwana huko Gilgali.
34Kisha Samweli akaenda Rama, lakini Sauli akapanda nyumbani mwake huko Gibea ya Sauli.
35Hadi siku Samweli alipofariki hakuenda kumwona Sauli tena, ingawa Samweli alimwomboleza. Naye Bwana alihuzunika kwamba alimfanya Sauli kuwa mfalme juu ya Israeli.