1 Samweli 7

1 Samweli 7

1Kisha wanaume wa Kiriath-Yearimu wakaja na kulichukua Sanduku la Bwana . Wakalipeleka katika nyumba ya Abinadabu kilimani, na kumweka Eleazari mwanawe wakfu kulichunga Sanduku la Bwana .

2Sanduku la Bwana lilibakia huko Kiriath-Yearimu kwa muda mrefu, jumla ya miaka ishirini.

Samweli awatiisha Wafilisti huko Mispa

Nao watu wote wa Israeli wakamrudia Bwana .

3Naye Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, “Ikiwa mtamrudia Bwana kwa mioyo yenu yote, basi iacheni miungu migeni na Maashtorethi, na kujitoa wenyewe kwa Bwana na kumtumikia yeye peke yake, naye atawaokoa ninyi kutoka kwa mkono wa Wafilisti.”

4Hivyo Waisraeli wakaweka mbali Mabaali yao na Maashtorethi yao, nao wakamtumikia Bwana peke yake.

5Kisha Samweli akasema, “Wakusanyeni Israeli wote huko Mispa, nami nitawaombea kwa Bwana .”

6Walipokwisha kukutanika huko Mispa, walichota maji na kuyamimina mbele za Bwana . Siku hiyo walifunga na wakaungama, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi ya Bwana .” Naye Samweli alikuwa kiongozi wa Israeli huko Mispa.[#7:6 yaani mwamuzi]

7Wafilisti waliposikia kwamba Israeli wamekusanyika huko Mispa, watawala wa Wafilisti wakapanda ili kuwashambulia. Waisraeli waliposikia habari hiyo, waliogopa kwa sababu ya Wafilisti.

8Wakamwambia Samweli, “Usiache kumlilia Bwana , Mungu wetu, kwa ajili yetu, ili apate kutuokoa na mikono ya Wafilisti.”

9Kisha Samweli akamchukua mwana-kondoo anyonyaye na kumtoa mzima kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana . Akamlilia Bwana kwa niaba ya Israeli, naye Bwana akamjibu.

10Samweli alipokuwa anatoa hiyo dhabihu ya kuteketezwa, Wafilisti wakasogea karibu ili kupigana vita na Israeli. Lakini siku ile Bwana alinguruma kwa ngurumo kubwa dhidi ya Wafilisti na kuwafanya wafadhaike na kutetemeka hivi kwamba walikimbizwa mbele ya Waisraeli.

11Wanaume wa Israeli wakatoka mbio huko Mispa na kuwafuatia Wafilisti, wakiwachinja njiani hadi mahali chini ya Beth-Kari.

12Ndipo Samweli akachukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni. Akaliita Ebenezeri, akisema, “Hadi sasa Bwana ametusaidia.”[#7:12 maana yake Jiwe la usaidizi]

13Basi Wafilisti wakashindwa na hawakuvamia nchi ya Israeli tena.

Katika maisha yote ya Samweli, mkono wa Bwana ulikuwa dhidi ya Wafilisti.

14Miji kuanzia Ekroni hadi Gathi, ambayo Wafilisti walikuwa wameiteka kutoka Israeli, ilirudishwa kwake, naye Israeli akazikomboa nchi jirani mikononi mwa Wafilisti. Kukawa na amani kati ya Israeli na Waamori.

15Samweli akaendelea kuwa mwamuzi wa Israeli siku zote za maisha yake.

16Mwaka hadi mwaka aliendelea kuzunguka kutoka Betheli hadi Gilgali na Mispa, akiamua Israeli katika sehemu hizo zote.

17Lakini kila mara alirudi Rama, kulikokuwa nyumbani mwake, huko pia aliamua Israeli. Naye huko alimjengea Bwana madhabahu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.