The chat will start when you send the first message.
1Naye Abiya akalala na baba zake, akazikwa katika Mji wa Daudi. Asa mwanawe akawa mfalme baada yake. Katika siku zake, nchi ikawa na amani kwa miaka kumi.
2Asa akatenda yaliyo mema na haki machoni pa Bwana Mungu wake.
3Akaziondoa madhabahu za kigeni na mahali pa juu pa kuabudia, akayavunja yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Maashera.
4Akawaamuru Yuda kumtafuta Bwana , Mungu wa baba zao, na kutii sheria zake na amri zake.
5Akaondoa mahali pa juu pa kuabudia na madhabahu za kufukizia uvumba kwenye kila mji katika Yuda, nao ufalme ulikuwa na amani katika utawala wake.
6Akajenga miji yenye ngome katika Yuda, wakati nchi ikiwa na amani. Hakuna mtu yeyote aliyepigana vita naye katika miaka hiyo, kwa kuwa Bwana alimpa amani.
7Mfalme akawaambia Yuda, “Tuijenge hii miji na tuizungushie kuta, pamoja na minara, malango na makomeo. Nchi bado ni yetu, kwa sababu tumemtafuta Bwana Mungu wetu, tulimtafuta naye ametupatia amani kila upande.” Hivyo wakajenga na wakafanikiwa.
8Asa alikuwa na jeshi la watu elfu mia tatu kutoka Yuda, wenye ngao kubwa na mikuki, na jeshi la watu elfu mia mbili na themanini kutoka Benyamini, wenye ngao ndogo na pinde. Watu hawa wote walikuwa wapiganaji hodari.
9Zera Mkushi akatoka kupigana dhidi yao akiwa na jeshi la watu maelfu ya maelfu na magari ya vita mia tatu, nao wakaja Maresha.
10Asa akatoka kumkabili, nao wakapanga vita katika Bonde la Sefatha karibu na Maresha.
11Kisha Asa akamlilia Bwana Mungu wake na kusema, “Ee Bwana , hakuna yeyote aliye kama wewe wa kuwasaidia wasio na nguvu dhidi ya wenye nguvu. Utusaidie, Ee Bwana , wewe ndiwe Mungu wetu, kwa kuwa tunakutumainia wewe, nasi kwa jina lako tumekuja dhidi ya jeshi hili kubwa. Ee Bwana , wewe ndiwe Mungu wetu, usiwaache wanadamu wakushinde wewe.”
12Bwana akawapiga Wakushi mbele ya Asa na Yuda. Wakushi wakakimbia,
13naye Asa na jeshi lake wakawafuatia hadi Gerari. Idadi kubwa ya Wakushi ilianguka hata wasiweze kuinuka tena, wakapondapondwa mbele za Bwana na majeshi yake. Watu wa Yuda wakachukua nyara nyingi sana;
14wakaangamiza vijiji vyote vya Gerari, kwa kuwa kicho cha Bwana kilikuwa kimewaangukia. Wakateka nyara vijiji hivi vyote, kwani kulikuwa na nyara nyingi huko.
15Pia wakashambulia kambi za wachunga makundi ya wanyama wakachukua na kuyaswaga makundi ya kondoo, mbuzi na ngamia. Kisha wakarudi Yerusalemu.