The chat will start when you send the first message.
1Ndipo Sulemani akaanza kujenga Hekalu la Bwana katika Yerusalemu juu ya Mlima Moria, pale ambapo Bwana alikuwa amemtokea Daudi baba yake. Ilikuwa katika kiwanja cha kupuria cha Arauna Myebusi, mahali palipotolewa na Daudi.[#3:1 au Ornani kwa Kiebrania]
2Alianza kujenga siku ya pili ya mwezi wa pili katika mwaka wa nne wa utawala wake.
3Msingi aliouweka Sulemani kwa ajili ya kulijenga Hekalu la Mungu ulikuwa na urefu wa dhiraa sitini, na upana wa dhiraa ishirini kwa kipimo cha kale.[#3:3 Dhiraa 60 ni sawa na mita 27.; #3:3 Dhiraa 20 ni sawa na mita 9.]
4Ukumbi wa mbele wa Hekalu ulikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, yaani kuanzia upande mmoja hadi upande mwingine wa upana wa nyumba hiyo, na kimo chake dhiraa thelathini.[#3:4 Dhiraa 30 ni sawa na mita 13.5.]
Akaufunika ndani kwa dhahabu safi.
5Akaufunika ukumbi mkuu kwa mbao za msunobari, na kufunikwa kwa dhahabu safi, na kuupamba kwa michoro ya mitende na minyororo.
6Alilipamba Hekalu kwa vito vya thamani. Hiyo dhahabu aliyotumia ilikuwa dhahabu ya Parvaimu.
7Akazifunika boriti za dari, miimo na vizingiti vya milango, kuta na milango ya Hekalu kwa dhahabu, naye akatia nakshi ya makerubi kwenye kuta.
8Akajenga Patakatifu pa Patakatifu, urefu na upana wake ulikuwa dhiraa ishirini, sawasawa na upana wa Hekalu. Alifunika ndani kwa talanta 600 za dhahabu safi.[#3:8 Talanta 600 ni sawa na tani 21.]
9Misumari ya dhahabu ilikuwa na uzito wa shekeli hamsini. Alivifunika pia vyumba vya juu kwa dhahabu.[#3:9 Shekeli 50 ni sawa na gramu 600.]
10Katika sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu akatengeneza jozi moja ya makerubi ya kuchongwa na kuyafunika kwa dhahabu.
11Urefu wa mabawa ya hao makerubi ulikuwa jumla ya dhiraa ishirini. Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano, nalo liligusa ukuta wa Hekalu; bawa lake lingine lilikuwa pia na urefu wa dhiraa tano, ambalo liligusa bawa la kerubi mwingine.[#3:11 Dhiraa 5 ni sawa na mita 2.25.]
12Vivyo hivyo bawa moja la kerubi wa pili lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na liligusa ukuta mwingine wa pili wa Hekalu, na bawa lake lingine lilikuwa pia na urefu wa dhiraa tano nalo liligusa bawa la kerubi wa kwanza.
13Mabawa ya makerubi hawa yalitanda dhiraa ishirini. Walisimama kwa miguu yao, nyuso zao zikielekea ukumbi mkubwa.
14Akatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na za kitani safi, na kutarizi makerubi juu yake.
15Mbele ya Hekalu Sulemani akatengeneza nguzo mbili, ambazo kwa pamoja zilikuwa na urefu wa dhiraa thelathini na tano kwenda juu, na kila moja ilikuwa na taji juu yake yenye kimo cha dhiraa tano.
16Akatengeneza minyororo iliyosokotwa, na kuiweka juu ya zile nguzo. Pia akatengeneza makomamanga mia moja, na kuyaunganisha kwenye minyororo.
17Akazisimamisha hizo nguzo mbele ya Hekalu, moja upande wa kusini na nyingine upande wa kaskazini. Ile moja ya upande wa kusini akaiita Yakini, na ya upande wa kaskazini akaiita Boazi.[#3:17 maana yake Atathibitisha; #3:17 maana yake Imo nguvu]