2 Wafalme 20

2 Wafalme 20

Ugonjwa wa Hezekia

(2Nya 32:24‑26; Isa 38:1‑8, 21‑22)

1Katika siku hizo, Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Bwana : Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”

2Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana :

3“Ee Bwana , kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu.

4Kabla Isaya hajaondoka katika ua wa kati, neno la Bwana likamjia, akaambiwa:

5“Rudi ukamwambie Hezekia, kiongozi wa watu wangu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana , Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako; nitakuponya. Siku ya tatu kuanzia sasa utapanda kwenda katika Hekalu la Bwana .

6Nitakuongezea miaka kumi na tano katika maisha yako. Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi!’ ”

7Kisha Isaya akasema, “Tengenezeni dawa ya kubandika ya tini.” Wakafanya hivyo na kuiweka kwenye jipu, naye akapona.

8Hezekia alimuuliza Isaya, “Kutakuwa na ishara gani kwamba Bwana ataniponya mimi, na kwamba nitapanda kwenda katika Hekalu la Bwana siku ya tatu tangu leo?”

9Isaya akajibu, “Hii ndiyo ishara ya Bwana kwako kwamba Bwana atafanya kile alichoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele, au kivuli kirudi nyuma hatua kumi?”

10Hezekia akasema, “Ni jambo rahisi kwa kivuli kutangulia mbele hatua kumi, kuliko kukifanya kirudi nyuma hatua kumi.”

11Ndipo nabii Isaya akamwita Bwana , naye Bwana akakifanya kivuli kurudi nyuma hatua kumi ambazo kilikuwa kimeshuka kwenye ngazi ya Ahazi.

Wajumbe kutoka Babeli

(Isa 39:1‑8)

12Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani mfalme wa Babeli, akamtumia Hezekia barua na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua kwa Hezekia.

13Hezekia akawapokea wale wajumbe na kuwaonesha vitu vyote vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha na kila kitu kilichokuwa katika hazina yake. Hapakuwa na kitu katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonesha.

14Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumuuliza, “Watu hao walisema nini, na wametoka wapi?”

Hezekia akamjibu, “Wametoka nchi ya mbali. Walikuja kutoka Babeli.”

15Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?”

Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu. Hakuna kitu katika hazina yangu ambacho sikuwaonesha.”

16Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Bwana :

17Hakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba hadi siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema Bwana .

18Nao baadhi ya wazao wako, mwili wako na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa mateka, nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.”

19Hezekia akamjibu Isaya, “Neno la Bwana ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Si patakuwa na amani na usalama wakati wa uhai wangu?”

20Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Hezekia, mafanikio yake yote, na jinsi alivyotengeneza bwawa na mfereji ulioleta maji katika mji, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?

21Hezekia akalala na baba zake. Naye Manase mwanawe akawa mfalme baada yake.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.