Amosi 5

Amosi 5

Maombolezo na wito wa toba

1Sikia neno hili, ee nyumba ya Israeli, ombolezo hili ninalifanya kuwahusu ninyi:

2“Bikira Israeli ameanguka,

kamwe hatainuka tena,

ameachwa pweke katika nchi yake,

hakuna yeyote wa kumwinua.”

3Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“Mmoja wa miji yako utakapopeleka watu elfu moja vitani kwa ajili ya Israeli,

mia moja tu watarudi;

wakati mji utakapopeleka mia moja,

kumi tu ndio watarudi hai.”

4Hili ndilo asemalo Bwana kwa nyumba ya Israeli:

“Nitafuteni mpate kuishi;

5msitafute Betheli,

msiende Gilgali,

msisafiri kwenda Beer-Sheba.

Kwa maana kwa hakika Gilgali itaenda uhamishoni,

na Betheli itafanywa kuwa ubatili.”

6Mtafuteni Bwana mpate kuishi,

au atafagia nyumba ya Yusufu kama moto;

utawateketeza, nayo Betheli

haitakuwa na yeyote wa kuuzima.

7Ninyi ambao mnageuza haki kuwa uchungu

na kuiangusha haki chini

8(yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni,

ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko

na mchana kuwa usiku,

ambaye huyaita maji ya bahari

na kuyamwaga juu ya nchi:

Bwana ndilo jina lake;

9yeye hufanya maangamizi kwenye ngome

na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa),

10mnamchukia yule akemeaye mahakamani,

na kumdharau yule ambaye husema kweli.

11Mnamgandamiza maskini

na kumlazimisha awape nafaka.

Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari,

hamtaishi ndani yake;

ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu,

hamtakunywa divai yake.

12Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu

na ukubwa wa dhambi zenu.

Mmewadhulumu wenye haki na kupokea rushwa

na kuzuia haki ya maskini mahakamani.

13Kwa hiyo mtu mwenye busara hunyamaza nyakati kama hizo,

kwa kuwa nyakati ni mbaya.

14Tafuteni mema, wala si mabaya,

ili mpate kuishi.

Ndipo Bwana Mungu wa majeshi atakuwa pamoja nanyi,

kama msemavyo yupo nanyi.

15Yachukieni maovu, yapendeni mema;

dumisheni haki mahakamani.

Yamkini Bwana Mungu wa majeshi

atawahurumia mabaki ya Yusufu.

16Kwa hiyo hili ndilo Bwana, Bwana Mungu wa majeshi, asemalo:

“Kutakuwa na maombolezo barabarani zote,

na vilio vya uchungu katika njia kuu zote.

Wakulima wataitwa kuja kulia,

na waombolezaji waje kuomboleza.

17Kutakuwa na kuomboleza katika mashamba yote ya mizabibu,

kwa kuwa nitapita kati yenu,”

asema Bwana .

Siku ya Bwana

18Ole wenu ninyi mnaoitamani

siku ya Bwana !

Kwa nini mnaitamani siku ya Bwana ?

Siku hiyo itakuwa giza, si nuru.

19Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba

kumbe akakutana na dubu,

kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake

na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta,

kumbe akaumwa na nyoka.

20Je, siku ya Bwana haitakuwa giza, na si nuru:

giza nene, bila mwali wowote?

21“Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini;

siwezi kuvumilia makusanyiko yenu.

22Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka,

sitazikubali.

Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani,

sitazitambua.

23Niondoleeni kelele za nyimbo zenu!

Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu.

24Lakini acheni haki itiririke kama mto,

na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka!

25“Je, mliniletea dhabihu na sadaka

kwa miaka arobaini kule jangwani,

ee nyumba ya Israeli?

26Mmeyainua madhabahu ya Sikuthi

mungu wenu mtawala,

na Kiuni mungu wenu wa nyota,

ambao mliwatengeneza wenyewe.

27Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni mbali kupita Dameski,”

asema Bwana , ambaye jina lake ni Mungu wa majeshi.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.