The chat will start when you send the first message.
1Wakati ule Bwana aliniambia, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza uje kwangu juu mlimani. Pia utengeneze Sanduku la mbao.
2Nitaandika juu ya vibao maneno yaliyokuwa katika vile vibao vya kwanza, ambavyo ulivivunja. Kisha utaviweka ndani ya Sanduku.”
3Hivyo nikatengeneza Sanduku kwa mti wa mshita, nikachonga pia vibao vya mawe kama vile vya kwanza, kisha nikakwea mlimani nikiwa na vile vibao viwili mikononi mwangu.
4Bwana akaandika juu ya hivi vibao kile alichokuwa amekiandika kabla, Amri Kumi alizokuwa amewatangazia huko mlimani, kutoka kati ya moto siku ile ya kusanyiko. Bwana akanikabidhi.
5Kisha nikashuka kutoka mlimani na kuweka vibao ndani ya Sanduku nililokuwa nimelitengeneza, kama Bwana alivyoniagiza, navyo viko huko sasa.
6(Waisraeli walisafiri kutoka visima vya Bene-Yaakani hadi Mosera. Huko Haruni alifariki na kuzikwa, naye Eleazari mwanawe akachukua nafasi yake kama kuhani.
7Kutoka pale, walisafiri hadi Gudgoda wakaendelea hadi Yotbatha, nchi yenye vijito vya maji.
8Wakati huo Bwana aliteua kabila la Lawi kulibeba Sanduku la Agano la Bwana , kusimama mbele za Bwana ili kutoa huduma, na kutangaza baraka kwa Jina lake, kama wanavyofanya hadi leo.
9Hiyo ndiyo sababu ya Walawi kutokuwa na sehemu wala urithi miongoni mwa ndugu zao; Bwana ndiye urithi wao, kama Bwana Mungu wao alivyowaambia.)
10Basi nilikaa mlimani kwa siku arobaini usiku na mchana, kama nilivyofanya mara ya kwanza, pia Bwana alinisikiliza hata wakati huu. Haikuwa nia yake kuwaangamiza.
11Bwana akaniambia, “Nenda, ukawaongoze watu katika njia yao ili waweze kuingia na kuimiliki nchi ile niliyowaapia baba zao kuwapa.”
12Na sasa, ee Israeli, Bwana Mungu wako anataka nini kwako ila kumcha Bwana Mungu wako, kwenda katika njia zake, kumpenda na kumtumikia Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote,
13na kuyashika maagizo ya Bwana na amri zake ninazokupa leo kwa mafanikio yako mwenyewe?
14Mbingu, hata mbingu za juu sana, dunia na kila kitu kilichomo, ni mali ya Bwana Mungu wako.
15Hata hivyo Bwana alikuwa na shauku na baba zako, akawapenda na akawachagua ninyi, wazao wao, kuliko mataifa yote, kama ilivyo leo.
16Kwa hiyo tahirini mioyo yenu, na msiwe na shingo ngumu tena.
17Kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye uweza na wa kutisha, ambaye hana upendeleo na hapokei rushwa.
18Huwapigania yatima na wajane, humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi.
19Nanyi wapendeni wageni, kwa kuwa ninyi wenyewe mlikuwa wageni huko Misri.
20Mche Bwana Mungu wako na umtumikie yeye. Shikamana naye kwa uthabiti na kuapa kwa jina lake.
21Yeye ni sifa yako; yeye ni Mungu wako, ambaye alikutendea yale maajabu makubwa na ya kutisha uliyoyaona kwa macho yako mwenyewe.
22Baba zako walioshuka kwenda Misri jumla yao walikuwa sabini, na sasa Bwana Mungu wako amekufanya taifa la watu wengi kama nyota za angani.