The chat will start when you send the first message.
1Kila mwisho wa miaka saba ni lazima mfute madeni.
2Hivi ndivyo itakavyofanyika: Kila mkopeshaji atafuta mkopo aliomkopesha Mwisraeli mwenzake. Hatamtaka Mwisraeli mwenzake au ndugu yake amlipe hilo deni, kwa sababu wakati wa Bwana wa kufuta madeni umetangazwa.
3Unaweza kudai malipo kwa mgeni, lakini lazima ufute kila deni ambalo unamdai ndugu yako.
4Hata hivyo, hapatakuwa na maskini miongoni mwenu, kwa kuwa katika nchi Bwana Mungu wenu anayowapa kuimiliki kama urithi wenu, atawabariki sana,
5ikiwa tutamtii Bwana Mungu wenu kikamilifu na kuwa waangalifu kuyafuata maagizo haya yote ninayowapa leo.
6Kwa kuwa Bwana Mungu wenu atawabariki kama alivyoahidi, nanyi mtawakopesha mataifa mengi lakini hamtakopa kwa yeyote. Mtatawala mataifa mengi lakini hakuna taifa litakalowatawala ninyi.
7Ikiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini.
8Bali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji.
9Jihadhari usijiwekee wazo hili ovu: “Mwaka wa saba, mwaka wa kufuta madeni umekaribia,” usije ukaonesha nia mbaya kwa ndugu yako mhitaji na ukaacha kumpa chochote. Anaweza kumlalamikia Bwana dhidi yako nawe utakuwa umepatikana na hatia ya dhambi.
10Mpe kwa ukarimu na ufanye hivyo bila kinyongo moyoni, ndipo kwa sababu ya hili Bwana Mungu wenu atakubariki katika kazi zako zote na kwa kila kitu utakachokiwekea mkono wako.
11Siku zote watakuwa watu maskini katika nchi. Kwa hiyo ninawaamuru mwe wakarimu kwa ndugu zenu walio maskini na wahitaji katika nchi yenu.
12Kama Mwebrania mwenzako, mwanaume au mwanamke, akijiuza kwako na kukutumikia miaka sita, katika mwaka wa saba ni lazima umwache aende zake akiwa huru.
13Nawe wakati utakapomwachia usimwache aende mikono mitupu.
14Mpe kwa hiari kutoka kundi lako la kondoo na mbuzi, kutoka sakafu yako ya kupuria nafaka, na kutoka shinikizo lako la kukamulia zabibu. Mpe kama vile Bwana Mungu wako alivyokubariki.
15Kumbukeni kuwa ninyi mlikuwa watumwa huko Misri naye Bwana Mungu wenu aliwakomboa. Ndiyo sababu nimewapa agizo hili leo.
16Lakini mtumishi wako akikuambia, “Sitaki kukuacha,” kwa sababu anakupenda wewe na jamaa yako naye anaridhika nawe,
17ndipo utachukua chuma kidogo utoboe sikio lake hadi hicho chuma kiingie kwenye ubao wa mlango, naye atakuwa mtumishi wako wa maisha. Ufanye vivyo hivyo kwa mjakazi wako.
18Usifikiri kuwa kuna ugumu kumwacha mtumishi wako huru, kwa sababu utumishi wake kwako kwa miaka hii sita umekuwa wa thamani mara mbili ya ujira wa mtumishi wa kuajiriwa. Naye Bwana Mungu wenu atakubariki kwa kila kitu utakachofanya.
19Wekeni wakfu kwa Bwana Mungu wenu kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa makundi yenu ya ngʼombe na ya mbuzi na kondoo. Maksai walio wazaliwa wa kwanza msiwafanyize kazi, wala msinyoe manyoya ya wazaliwa wa kwanza wa kondoo.
20Kila mwaka ninyi na jamaa zenu mtapaswa kuwala mbele za Bwana Mungu wenu pale mahali atakapopachagua.
21Kama mnyama ana dosari, akiwa ni kilema au kipofu au kama ana kilema kibaya, kamwe usimtoe dhabihu kwa Bwana Mungu wenu.
22Itawapasa kumla ninyi wenyewe katika miji yenu. Wote walio najisi na waliotakasika mwaweza kula kama vile mnavyokula paa au kulungu.
23Lakini kamwe msile damu; imwageni ardhini kama maji.