Kumbukumbu 19

Kumbukumbu 19

Miji ya makimbilio

(Hes 35:9‑34; Yos 20:1‑9)

1Bwana Mungu wenu atakapokuwa amewaangamiza mataifa ambayo nchi yao anawapa ninyi, wakati mtakuwa mmewafukuza na kuishi katika miji yao na nyumba zao,

2ndipo mtenge miji mitatu iliyopo katikati ya nchi kwa ajili yenu, katika nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa kuimiliki.

3Jengeni barabara katika miji hiyo na kuigawa mara tatu, nchi anayowapa Bwana Mungu wenu kama urithi, ili yeyote amuuaye mtu aweze kukimbilia humo.

4Hii ndiyo kanuni kuhusu mtu amuuaye mwingine na kukimbilia humo kuokoa maisha yake, yaani yeye amuuaye jirani yake bila kukusudia, wala hakumchukia kabla ya hapo.

5Kwa mfano, mtu aweza kwenda msituni na jirani yake kukata miti, naye anapozungusha shoka kuangusha mti, shoka linaweza kuchomoka kutoka mpini na kumpiga jirani yake na kumuua. Yule mtu anaweza kukimbilia katika mojawapo ya miji hii na kuokoa maisha yake.

6Kama sivyo, mlipiza kisasi cha damu anaweza kumfuatilia kwa hasira kali, naye akamkamata na kumuua kama umbali ni mrefu sana hata ingawa hastahili kifo, kwa sababu amemuua jirani yake bila kukusudia.

7Hii ndiyo sababu nimewaagiza ninyi kutenga miji mitatu ya makimbilio kwa ajili yenu.

8Kama Bwana Mungu wenu akipanua nchi yenu, kama alivyoahidi kwa kiapo kwa baba zenu na kuwapa nchi yote aliyowaahidi,

9kwa sababu mmefuata kwa uangalifu sheria zote ninazowaamuru leo, kumpenda Bwana Mungu wenu na kuenenda siku zote katika njia zake, ndipo mtenge miji mingine mitatu.

10Fanyeni hivi ili damu isiyo na hatia isimwagwe katika nchi yenu, ambayo Bwana Mungu wenu anawapa kama urithi wenu, ili msije mkawa na hatia ya kumwaga damu.

11Lakini kama mtu anamchukia ndugu yake, akamvizia, akamshambulia na kumuua, kisha akakimbilia katika mojawapo ya miji hii,

12wazee wa mji wake watatuma ujumbe kwake, kumleta kutoka mji ule na kumkabidhi mlipiza kisasi cha damu kumuua.

13Msimwonee huruma. Lazima mwondoe katika Israeli hatia ya umwagaji damu isiyo na hatia ili mpate kufanikiwa.

14Usisogeze jiwe la mpaka wa jirani yako ambao uliwekwa na wale waliokutangulia katika urithi upokeao katika nchi Bwana Mungu wako anayowapa kuimiliki.

Mashahidi

15Shahidi mmoja hatoshi kumtia hatiani mtu kwa uhalifu au kosa lolote ambalo anaweza kuwa amelitenda. Lazima shauri lolote lithibitishwe kwa ushuhuda wa mashahidi wawili au watatu.

16Kama shahidi mwenye nia ya kumdhuru mwingine akisimama kumshtaki mtu kwa uhalifu,

17watu wawili wanaohusika katika mabishano lazima wasimame mbele za Bwana na mbele ya makuhani na waamuzi ambao wako kazini wakati huo.

18Waamuzi lazima wafanye uchunguzi kwa makini na shahidi akionekana kuwa ni mwongo, akitoa ushuhuda wa uongo dhidi ya ndugu yake,

19basi mtende kama alivyotaka kumtendea ndugu yake. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.

20Watu watakaosalia watasikia hili na kuogopa, uovu kama huo kamwe hautatendeka tena miongoni mwenu.

21Msioneshe huruma, uhai kwa uhai, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.