Waefeso 1

Waefeso 1

Salamu

Baraka za kiroho katika Kristo Yesu

3Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo.

4Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo

5alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kupitia kwa Yesu Kristo kwa furaha na mapenzi yake.

6Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa.

7Ndani yake tunao ukombozi kupitia kwa damu yake, yaani msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake

8aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote.

9Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo,

10ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.

11Katika Kristo sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake,

12ili, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Kristo, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake.

13Ninyi pia mliingia ndani ya Kristo mliposikia neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Baada ya kuamini, mlitiwa muhuri ndani yake, huyo Roho Mtakatifu mliyeahidiwa,

14yeye ambaye ni amana yetu ya kutuhakikishia urithi wetu hadi ukombozi wa wale walio milki ya Mungu, kwa sifa ya utukufu wake.

Shukrani na maombi

15Kwa sababu hii, tangu niliposikia kuhusu imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watakatifu wote,

16sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu.

17Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi.

18Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu

19na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno

20aliyoitumia katika Kristo alipomfufua kutoka kwa wafu, na kumketisha mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho,

21juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia.

22Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake, na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya Kanisa,

23ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.